Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HISIA ZANGU: Albadiri ya Tanga na usela wa Djuma Shaban

Tanga Pic Albadiri ya Tanga na usela wa Djuma Shaban

Wed, 26 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wikiendi hii ilikuwa na mambo matatu yaliyonivutia katika soka letu. Inafurahisha kiasi. Soka letu lina mambo yanayochekesha na wakati mwingine huwa tunasema kwamba ‘Soka letu kivyetuvyetu’. Kuna mambo hautayakuta kwingine.

Tuanzie wapi? Tanga. Wiki moja iliyopita Yanga wakiwa na kikosi chao bora walisafiri kwenda mpaka Tanga kwenda kukipiga na Coastal Union. Yanga walishinda 2-0. Nawajua watu wa Tanga. Nilijua hilo lisingepita bure. Lazima kuna jambo lingefuata.

Wiki nzima watu wa Tanga walikuwa wanashutumiana kuhusu matokeo hayo. Katika makundi ya mitandaoni zilisikika kelele nyingi kwamba Coastal wamehujumiana wenyewe kwa wenyewe na ndio maana timu imefungwa. Nawajua wajomba zangu watu wa Tanga. Ilikuwa lazima atafutwe mchawi.

Baadaye nikasikia kutakuwa na kisomo maalumu cha kuwadhuru wale wote ambao walihujumu timu. Binafsi kwa macho yangu sikuona kama kulikuwa na hujuma yoyote. Namna ambavyo Yanga walifunga mabao yao ungeweza kumsifu Djuma Shaban kwa krosi ambayo Fiston Mayele alifunga.

Ungeweza kumsifu Farid Mussa kwa utulivu alionyesha wakati akiwa amezungukwa na msitu wa walinzi wa Coastal Union lakini bado akampasia Saido Ntibanzokiza aliyefunga bao la pili. Hii ni kwa mujibu wa macho yetu watu wa soka.

Macho ya wengine pale Tanga ilikuwa ni kwamba Coastal ilikuwa imehujumiwa na watu wake wenyewe na ghafla kisomo kikaitishwa kwa ajili ya watu ambao walihujumu katika pambano hilo.

Kabla hatujafika mbali wikiendi hii Coastal wakacheza tena nyumbani na kubabuliwa mabao 1-3 na Namungo. Uwanja huo huo wa Mkwakwani. Unajiuliza vipi kuhusu mechi ya Namungo nayo ilihujumiwa? Hatujasikia hujuma katika mechi hii.

Yanga na timu waliyokuwa nayo msimu huu wanashindwa kuifunga Coastal kihalali? Mbona Coastal huwa inafungwa na timu nyingine katika ligi hii? Kuthibitisha hilo siku chache tu baadaye wamefungwa na Namungo katika uwanja huo huo.

Lakini msimu uliopita Yanga walichapwa na Coastal 2-1 katika uwanja huo huo. Na wakati huo Yanga walikuwa hawajapoteza mechi yoyote ya Ligi. Mbona walikubali na hawakwenda kusoma kisomo? Ina maana matokeo halali ni Coastal kumfunga Yanga tu?

Haya mambo yanatupotezea muda katika soka letu. Neno hujuma limeendelea kupata umaarufu mkubwa bila ya kujali kwamba kitu muhimu ni kuunda timu imara. Makocha na wachezaji wamefukuzwa sana kwa sababu ya neno hujuma lakini timu hizo hizo zimeendelea kupata matokeo mabaya.

Tukiachana na jambo hilo kuna kitu kingine kimetoka Arusha. Yanga walikuwa wanacheza na Polisi pale Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na mlinzi wa kulia wa Yanga, Djuma Shaaban akafanya ujinga wa kumpiga kiwiko staa wa Polisi, Yahaya Mbegu bila ya mpira.

Mwamuzi, Hans Mabena hakuona lakini kama angeona basi Djuma angepewa kadi nyekundu. Inawezekana na wasaidizi wa Mabena hawakuona lakini kama wangeona wangeweza kumshauri Mabena atoe kadi nyekundu.

Tukianza na Djuma mwenyewe, nadhani ameikosea sana klabu yake. Alichofanya kilikosa akili ya kawaida ya mchezaji wa kulipwa. Labda alikanyagwa kwa chini. Angeweza kuanguka na kugaragara kwa ajili ya kumtafutia kadi mwenzake.

Yanga walikuwa wanaongoza bao moja na mechi ilibakia dakika moja pambano kumalizika. Hapo hapo kilikuwa kitu kizuri kwa Yanga kupoteza muda zaidi. Kwanini ageuke nyuma na kumpiga adui kiwiko? Alikuwa ameudhika na nini zaidi?

Matokeo yake kwa sasa Djuma atafungiwa. Kitu kibaya kwa Yanga ni kwamba Shomari Kibwana naye ameumia. Uzuri wa walinzi wa kulia wa Yanga ni kwamba wanaweza kwenda kucheza kushoto. Ubaya ni kwamba kina David Bryson na Yassin Mustapha hawawezi kucheza kulia.

Hii itamlazimu Dickson Job kwenda kucheza kulia na kisha Yannick Bangala kurudi kama mlinzi wa nyuma. Mara nyingi Yanga inakuwa bora zaidi kama Bangala akicheza katika nafasi yake asilia na Khalid Aucho. Wote huu ni uzembe wa Djuma.

Kama unadhani uzembe wa Djuma ulikuwa unasikitisha basi kilichoendelea mitandaoni ndio kitu ambacho kinasikitisha zaidi. wakati watu wakimshambulia Djuma kwa kitendo chake, watetezi wake ambao ni watu wa Yanga walikuwa wanatoa vioja vinavyoanza kuzoeleka zaidi hapa nchini.

Walikuwa wanajaribu kuhalalisha kile ambacho Djuma amefanya kwa kujaribu kuturudishia matukio ambayo wachezaji wa wapinzani wao waliwahi kufanya huko nyuma. Na hata wapinzani wao nao wakawa wanarudishia matukio ambayo wachezaji wa wapinzani wao waliwahi kuyafanya.

Badala ya kujadili kile kilichoendelea kwa Djuma, shabiki au mwandishi analeta hoja na kuuliza “Mbona Wawa alimkanyaga Nchimbi”. Hapo hapo anatokea wa Simba anajibu mapigo tena kwa kuhoji “Mbona Lamine Moro alimkanyaga yule kiungo wa Dodoma City”.

Unajaribu kuwaza na kujiuliza akili za watu wetu. Unatengeneza hukumu kwa kupitia kosa la mtu mwingine? Unaweza kudhani ni habari ya wanasheria na mahakama zao lakini huu ni mpira. Mchezaji ambaye amefanya kosa leo inabidi aadabishwe kwa alichofanya leo.

Matokeo yake wachezaji wetu wakisikia utetezi wetu dhidi yao basi hawaoni kama walichofanya ni cha ajabu sana. Mara zote mchezaji akifanya ujinga kama ambao Djuma ameufanya basi mashabiki husimama upande wa wachezaji wao. Haishangazi kuona matukio haya yakijirudia mara kwa mara.

Na katika matukio kama haya klabu pia husimama na mchezaji. Ni mara moja tu nimewahi kusikia mchezaji akipigwa faini na klabu yake kwa kufanya ujinga. Alikuwa ni Lamine Moro alipotozwa faini kwa ujinga wake alioufanya katika pambano dhidi ya Dodoma.

Mpaka leo sijui ni lini klabu zitaacha kuvumilia ujinga huu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz