Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Gharama za utafiti chanzo wachimbaji kuamini ushirikina

Wanaharakati Wayataka Makampuni Ya Madini Kuwalipa Zaidi Wachimbaji DRC Gharama za utafiti chanzo wachimbaji kuamini ushirikina

Wed, 28 Jun 2023 Chanzo: mwanachidigital

Gharama kubwa za kufanya tafiti za kijiolojia kwenye maeneo ya uchimbaji wa dhahabu imetajwa kuwa moja ya sababu zinazowafanya wachimbaji wadogo kuendelea kuchimba kwa kubahatisha na kutegemea ramli za waganga wa kienyeji.

Akizungumza juni 27, 2023 kwenye mafunzo ya siku tatu yanayotolewa kwa wachimbaji wadogo juu ya upatikanaji na umuhimu wa kutumia taarifa za kijiolojia katika uchimbaji Mjiolojia, Abubakar Kitiku amesema uchimbaji mdogo unasukuma maendeleo vijijini na kupunguza umaskini lakini wachimbaji hawachimbi kwa tija sababu ya gharama kubwa za tafiti.

Kitiku amesema kwa sasa uelewa wa wachimbaji wadogo umebadilika na wengi wameonyesha nia ya kutumia taarifa za kisayansi lakini changamoto inayowakwamisha ni gharama kubwa hivyo, kuwafanya waendelee kuchimba kwa mazoea.

“Yapo maeneo yaliyofanyiwa tafiti za kijiolojia miaka ya nyuma wakitaka kununua taarifa hizo gharama ziko juu, kwa kuwa Serikali sasa inaitambua sekta ya uchimbaji mdogo na kutambua umuhimu wa taarifa za kijiolojia ni vema ikapunguza gharama za kupatata taarifa kwa kuwa zipo tayari ili wachimbaji waweze kuchimba kisasa,”amesema Kitiku

Kitiku amesema takwimu zinaonyesha tani 400 hadi 600 za dhahabu huzalishwa na wachimbaji wadogo duniani ambapo kwa Tanzania wachimbaji wadogo huzalisha asilimia 40 ya madini yote yanayopatikana nchini.

Amesema ukosefu wa taarifa za kijiolojia ni changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo nchini na kwamba endapo wachimbaji watatumia taarifa hizo wataongeza ufanisi na kuzuia uharibifu wa mazingira.

Awali Meneja Mradi wa miradi ya Dhahabu Tanzania kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Solidaridad, Winfrida Kanwa amesema mradi wa upatikanaji wa taarifa za kijiolojia kwa wachimbaji wadogo umelenga kuwasaidia kujua njia za kijiolojia zitakazowasaidia kujua eneo dhahabu ilipo badala ya kuchimba kimazoea.

Mradi huo wa FVO unaofadhiliwa na Wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi utawawezesha wachimbaji wadogo kuboresha uzalishaji na kuepuka kupoteza rasilimali muda na pesa kwa kuwekeza eneo lisilo na dhahabu.

Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la The Impact Facility, Godwin Zimba amesema Shirika hilo limeanza kutoa elimu ya utaalamu kwa wachimbaji wadogo na kutoa mikopo ya vifaa kwa gharama nafuu kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba kisayansi na kuachana na uchimbaji wa kubahatisha.

Columnist: mwanachidigital