Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

George Foreman mwanaume wa chuma

Ali Vs George George Foreman akipokea ngumi kutoka kwa Muhammad Ali

Sun, 1 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Alipokuwa kijana alivuma katika ndondi na sasa akiwa na miaka 74 ni maarufu kwa kuhimiza upendo anapohutubia kanisani na yakizungumzwa mapishi ya nyama za kuchoma kwa kutumia mashine iliyopewa jina lake.

Huyu ni aliyekuwa mpiganaji maarufu wa ndondi duniani, George Foreman wa Marekani, mwenye asili ya Kiafrika.

Foreman aliyekuwa bingwa wa dunia wa masumbwi kwa uzito wa juu ameweka kumbukumbu ya kipekee katika masumbwi.

Aliporudi katika masumbwi, baada ya kustaafu kwa miaka 10, miongoni mwa waliomsihi akiwa mzee wa kanisa kubadili uamuzi ni waumini wa kanisa lake, familia, marafiki na aliowahi kupigana nao.

“Masumbwi ni mchezo wa vijana...kizee usitutafutie balaa. Pumzika kanisani. George tunakupenda na kama unatupenda usikaribie ulingo wa masumbwi,” liliandika gazeti la kwao Atlanta, Marekani.

Foreman alikuwa na miaka 38 na baada ya wiki chache za mazoezi alikwenda California kupambana na Steve Zouski na kumdunda katika raundi ya nne.

Wengi walitegemea Foreman aliyekuwa na uzito wa ratili 270 na matatizo ya kunyanyua miguu angelikung’utwa.

Lakini Foreman alishinda mapambano manne huku uzito wake ukipungua na kuwa mwepesi kama kijana.

Katika mwaka 1988, akiwa na miaka 39, alishinda mapambano tisa na wapo waliosema alizaliwa upya. Kilichovutia ni ijapokuwa alipoteza madoido ya ujana, makonde yake yalikuwa mazito na hachoki.

Aliendelea na mazoezi, biashara na kuhubiri kanisani na kumtembelea rafiki yake Muhammad Ali aliyemsihi asipigane kwa vile ni mzee.

Baada ya kushinda mapambano manne alikutana na Gerry Cooney 1990 na kudhibitiwa, lakini katika raundi ya pili Foreman aliyekuwa na miaka 41 alishambulia kama simba aliyejeruhiwa na kumshinda kwa KO.

Foreman alipanda chati ya wapiganaji wa uzito wa juu, kama ilivyokuwa kabla hajastaafu miaka 13 nyuma.

Katika mwaka 1991 alipambana na bingwa wa dunia, Evander Holyfield. Foreman, akiwa na miaka 42 na hakutarajiwa kuhimili makonde ya Holyfield aliyekuwa mdogo wake kwa miaka 17.

Pambano lilipoanza Foreman alijihami na mashabiki walimwambia: “Leo utapata unachokitafuta”.

Baadaye alisukuma makonde ya uhakika, lakini pambano lilipomalizika Holyfield alitangazwa mshindi kwa pointi. Foreman alisema: “Nusu ya ndoto yangu ya kuonyesha hata ukiwa na miaka 40 unaweza kupigana raundi 12. Naahidi mtashangaa.”

Baadaye alipambana na Alex Stewart, ambaye katika pambano lake la mwisho alidundwa na Mike Tyson. Foreman alimuangusha Stewart mara mbili raundi ya pili, lakini Stewart hakusalimu amri. Pambano lilikwenda hadi raundi ya 10 na Foreman alichapwa vibaya na uso kulowa damu.

Watu wengi walimtaka astaafu, lakini alikataa na kusema alikuwa na deni kwa mashabiki na kilichobakia ni kutimiza nusu ya ndoto yake.

Katika mwaka 1993 alikutana na mpiganaji chipukizi Tommy Morrison na Norrison alishinda kwa pointi.

Marafiki zake walipomwambia jua limetua aliwaambia mambo bado na katika mwaka 1994 alitaka awanie ubingwa wa dunia aliouachia alipostaafu miaka 15 nyuma.

Mashirika ya kimataifa ya ndondi, IBF na WBA, yalipomkatalia alikwenda mahakamani na kudai alibaguliwa kwa sababu ya umri mkubwa.

Alishinda na kupewa nafasi ya mwisho ya kupigania ubingwa wa dunia uliokuwa wazi. Nayo ni kurudiana na Morison Las Vegas, Nevada.

Moorer aliongoza na alimdhibiti Foreman, lakini mambo yaligeuka raundi ya 10 Foreman alipomtwanga Moorer konde la kulia kwenye kidevu kilichodata na kumwaga damu. Moorer alishindwa kuinuka.

Wengi hawakuamini Foreman kuuchukua tena ubingwa wa dunia na kuweka rekodi ya kuwa bingwa akiwa na miaka 45, mpiganaji mkongwe kushika wadhifa huo.

Siku chache baadaye alizungumzia kupambana na Mike Tyson, lakini WBA walimtaka apambane na Tony Tucker. Foreman alikataa na akavuliwa ubingwa.

Baadaye alipambana na Axel Schulz wa Ujerumani kutetea ubingwa wa IBF na alishinda. IBF ilipanga warudiane Ujerumani, lakini Foreman alikataa na kuvuliwa ubingwa.

Katika mwaka 1966, akiwa na miaka 47, alikwenda Tokyo na kumshinda chipukizi Crawford Grimsley. Mwaka uliofuata alipigana na Lou Savarese na kushinda na WBA walipomuona kiboko walimkutanisha na Shannon Briggs ili mshindi apambane na bingwa wa WBC, Lennox Lewis.

Foreman alipoteza kwa pointi, uamuzi uliotiliwa shaka kwa kuonekana Foreman angekuwa bingwa kwa mara ya tatu ndondi ingepoteza ladha. Hii ilimfanya Foreman kustaafu.

Siku hizi anawafundisha ndondi vijana, hutangaza mashindano katika televisheni na anahubiri kanisani.

Alipokuwa kijana alitumia muda mwingi vituo vya polisi kwa kufanya fujo na alipewa kazi ya askari, lakini aliachishwa kutokana na kuwapiga wenzake.

Alipata umaarufu akiwa na miaka 19 aliposhinda medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 1968. Alianza ngumi za kulipwa 1969 na alipigana mara 13 na kushinda mapambano yote, mara 11 kwa kuwatoa wapinzani (KO).

Cookie Wallace, alimalizwa sekunde 23 baada ya kuanza pambano na 1973 alikutana na aliyekuwa bingwa, Joe Frazier, bondia ambaye alikuwa hajawahi kupoteza pambano. Akamdunda Frazier kwa KO ya raundi ya pili kwa kumsukumia zaidi ya makonde 10 mfululizo. Akatwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya kwanza.

Baadaye katika kuutetea ubingwa alikwenda Venezuela 1974 kukutanana na Ken Norton aliyemshinda Muhammad Ali kwa pointi.

Kisha alikutana na Muhammad Ali nchini Zaire (sasa Congo) 1974 katika pambano maarufu lililopewa jina la Rumble in the Jungle. Ali alikwepa makombora kwa kwenda kwenye kamba na kuitumia kurudi ulingoni kwa kasi kumchapa Foreman ambaye ilipofika raundi ya sita alichoka.

Katika raundi ya nane Ali alimsakama Foreman kwa makonde mazito na mwamuzi kumtangaza Ali mshindi. Foreman akapoteza pambano lake la kwanza. Akaamua kupumzika mwaka mzima na aliporudi alikuwa imara kama chuma.

Sasa anafanya biashara za nyama za kuchoma zinazomuingizia dola 150 milioni kwa mwaka, mara tatu ya fedha alizopata alipokuwa bondia.

Vile vile ni mshirika wa kampuni ya mashine za kuchoma nyama ziitwazo George Foreman, anauza nguo na anazo hisa katika kampuni za magari.

Anao watoto 10, wanawake watano na wanaume watano. Watoto wote wa kiume wanaitwa George na mmoja wa kike, Freeda, ambaye ni mpiganaji mashuhuri wa ngumi.

Columnist: Mwanaspoti