Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Garikubwa: Nimezifanyia makubwa Yanga, Simba lakini...

Gari Kubwa Yanga Simba nyota wa zamani wa timu za Yanga, Simba na Taifa Stars, Willy Martin ‘Garikubwa’

Thu, 16 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

“NIMETELEKEZWA”. Ni neno alilotamka nyota wa zamani wa timu za Yanga, Simba na Taifa Stars, Willy Martin ‘Garikubwa’ wakati akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu nyumbani kwake jijini hapa.

Garikubwa baada ya kuamua kustaafu soka, kwa sasa anaishi mtaa wa Kikuba, Kijiji cha Lubaga, wilayani Kyela, mkoani Mbeya akiwa na familia ya mke mmoja na watoto watano.

Enzi zake nyota huyo alifanya makubwa akiacha rekodi na historia kwa timu alizopitia kwani nje ya Yanga na Simba, alikipiga pia Boma FC, Ushirika ya Moshi na Majimaji ya Songea kwa mafanikio makubwa.

Mwanaspoti lilimtembelea mkongwe huyo ambaye ni mgonjwa nyumbani kwake na ni baada ya kufanyiwa upasuaji wa utumbo tangu mwaka 2004 alipotundika daruga wakati wa mazoezi akiwa na Wekundu wa Msimbazi na sasa hana shughuli yoyote.

Beki huyo ameeleza mengi kuhusu maisha yake akiwa mchezaji na uhalisia wa sasa huku akitoa ujumbe kwa vigogo wa soka nchini, Yanga na Simba na serikali kwa jumla.

MAISHA YAKE

Kiuhalisia maisha ya staa huyo si mazuri sana na katika kuthibitisha hilo, mwenyewe anasema kile alichokifanya akiwa na nguvu ndani ya nchi ni tofauti na alivyo sasa.

“Stars niliitumikia miaka sita, ukizingatia enzi hizo hatukuwa na malipo yoyote, nikaenda Ushirika Moshi, Yanga, Majimaji na nikastaafia Simba na kote kila mmoja alinufaika na mimi.

“Lakini ukiangalia kazi niliyofanya kwa miaka 18 yote na uhalisia wa maisha yangu ya sasa unaweza usiamini kilichobaki ni jina tu mtaani kwamba alikuwa staa asiye na kitu,” anasema Garikubwa.

Mkongwe huyo anasema pamoja na changamoto za magonjwa lakini anasikitika kutoona kiongozi yeyote wa Yanga, Simba au wa serikali kumtembelea na kumfariji katika hali ya kutambua mchango wake.

AWALILIA MO NA HERSI

Katika kilio chake mkongwe huyo anasema baada ya kustaafu soka alijiendeleza na elimu ya ukocha hivyo anatamani vigogo wa Simba kupitia Mwekezaji wao Mohamed ëMoí Dewji na rais wa Yanga, Hersi Said kumpa mtaji.

Anasema kama sehemu alipo akipata nafasi ya kuandaa kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalishia vipaji kwa Simba na Yanga inaweza kumsaidia kuendeshea maisha yake na familia.

“Nimekuwa nahodha wa timu hizo ikiwa ni rekodi na historia pekee kwa mchezaji hapa Tanzania, lakini ni kama nimesahaulika kwao, nikipata mtaji nitaanzisha kituo cha michezo kwa ajili ya vijana.”

“Kwa sasa sifanyi shughuli nzito, wanipe japo tenda ya kuuza jezi zao huku Mbeya sehemu yoyote wasiishie kuwajali wale wa Dar es Salaam tu, mimi nimepambana kwa kiasi kikubwa na hizi timu,” anasema staa huyo.

SIRI YA UNAHODHA

Beki huyu mwenye elimu ya uhasibu aliyopata Chuo cha Ushirika Moshi, anatoboa siri ya kuwa nahodha kwa timu zote alizopitia ikiwa ni rekodi ya kipekee hadi sasa.

Alianza kuwa nahodha wa Ushirika Moshi, Yanga, Majimaji, Simba na Stars na alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakisikilizwa sana na viongozi na wachezaji.

Anabainisha ufanisi, nidhamu na kuheshimu mawazo ya kila mmoja ndio siri kubwa iliyompa uaminifu na wala siyo ‘kizizi’ kilichomfanya kungíara kila alipoenda.

“Jiulize kutoka Yanga nikiwa nahodha nikaenda Simba nikapewa kitambaa, kama haitoshi Stars napo wakaniamini wakanivisha uongozi, sawa na Ushirika na Majimaji, haikuwa ishu nyepesi bali ufanisi wangu,” anasema.

Anaongeza kilichompa heshima hiyo ni kutokana na misimamo yake, kudai haki kwa ajili ya wenzake lakini kushauri viongozi wa timu namna bora ya kujenga.

AJITOA KAFARA YANGA

Anasema haikuwa rahisi kuondoka Yanga, lakini alifikia uamuzi wa kung’atuka kutokana na mgogoro uliokuwepo na kuamua kujitoa kafara ili kuinusuru timu hiyo.

Mwaka 1991 Yanga ilikuwa ikipewa nguvu na Abbas Gulamali ambaye alikuwa mfadhili akisaidia mambo mengi timu hiyo katika uendeshaji na waliishi vizuri.

Anasema mwaka 1995 wakati Yanga inaenda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Gulamali alisafiri nje ya nchi kwa shughuli zake binafsi na timu kubaki katika wakati mgumu. Baada ya kushauriana kikosini walimwendea Reginald Mengi kumwomba nauli kwenda Afrika Kusini kucheza mechi yao ya marudiano dhidi ya Moroka Swallows japokuwa walifungwa mabao 2-1 na kutupwa nje.

“Mengi alikubali kutupa nauli, lakini akashauri badala ya kumtegemea mtu mmoja, timu iwekwe kwenye mfumo wa kampuni badala ya ule wa wanachama ili kuondoa changamoto kama hizi.”

“Ushauri huo niliuona wa msingi sana kwa sababu Mengi huyo aliahidi kujenga uwanja, hosteli, zahanati kwa ajili ya wachezaji na akaomba baada ya ujenzi huo apewe kwa miaka mitano kuendesha kisha akabidhi.”

“Tulikubaliana naye na kipindi hicho nikawa kwenye mipango ya muda mrefu lakini baadaye akarejea Gulamali akaleta fitina kuanza kuweka pingamizi kushawishi baadhi ya wanachama kudhoofisha mpango huo,” anasema Martin.

Anasema Gulamali alianza kutembeza pesa kuhamisha wachezaji kambi kwani kuna siku alimkabidhi Sh2.2 milioni ili awape wachezaji na kuwahamisha mtaa na kuwapeleka Kibaha.

“Mimi niliwaita wachezaji nikawapa msimamo Yanga lazima iwe kampuni, lakini Gulamali akaanza kutumia njia zake kushawishi baadhi ya wanachama kupinga huo mfumo.”

“Akaniita siku moja akanikabidhi Sh2.2 milioni niwape wachezaji kila mmoja laki moja, akatuhamisha mtaa kutupeleka Kibaha na lengo lake ilikuwa ni kuiuza hiyo timu nje ya nchi.”

Anasema baada ya kuona mambo yanazidi kuwa makubwa akaamua kubeba begi lake mgongoni kuondoka Yanga na siku hiyo taarifa zilisambaa na kulifanya jeshi la polisi kuzingira kambi na kuwakamata baadhi ya viongozi.

“Kwanza nilikumbuka kauli ya Nyerere (Hayati Mwl Julius) Yanga ilichangia pakubwa kupatikana Uhuru wa Tanzania, nikajiuliza nikihusika kwenye huu mgogoro timu ikauzwa nitaenda wapi.”

“Nikasimama nikawaambia askali pale kwamba mimi simo na hapa ninayo begi langu mgongoni naondoka, wakatupakiza kwenye basi na wachezaji tukaondoka wakawakamata viongozi,” anasema Garikubwa.

KUHUSU DIMBA

Anaeleza mwishoni mwa mwaka 1999 alijiunga na Wekundu akitokea Majimaji FC ambapo pamoja na kucheza soka, lakini aliaminiwa kwa kupewa majukumu makubwa kabla ya kupatwa majeraha na kuondoka.

Anasema kipindi hicho Simba ikiongozwa na aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alifikia hatua ya kumpa majukumu ya kuiongoza timu hiyo kama mweka hazina, katibu na mengine.

Kipindi hicho Simba ilikuwa na mgogoro wa uongozi hadi wakafikia hatua ya kumkabidhi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Yusuf Makamba lakini wachezaji walimshauri anipe majukumu,î

ìKwahiyo nikajikuta mimi ndio Mwenyekiti, Katibu, Mhasibu, Meneja na mambo yote, haikuwa kazi rahisi lakini nilipambana kumudu nikawa nashirikiana na Juma Amir na hapo tukawa na udhamini wa Mo Dewji wa Sh 105 milioni kwa miaka mitatu,î anasema.

Anasema wakati wakiendelea na mapambano ni kama mzimu wa Yanga ulihamia Simba kwani uliamka upya mgogoro baina ya wanachama wakitaka kufanyika uchaguzi kupata viongozi wapya.

ìKwahiyo hekaheka zikawa nyingi mvutano wa hapa na pale wakisema viongozi muda wao umeisha ufanyike uchaguzi mpya ndio akachaguliwa Hassan Dalali nikamuachia kiti,î anasema Martin.

Garikubwa aliziingiza Simba na Yanga vitani akiwa Ushirika. Unajua vita hiyo ya usajili ilimalizikaje na uamuzi wake mwenyewe na ishu nyingine kwenye klabu hizo mbili alizozichezea?

Columnist: Mwanaspoti