Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Gadiel Michael alikuwa na milango mingi mbele yake

Gadiel Michael Simba SC Gadiel Michael

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Beki mmoja maarufu wa kushoto nchini, Gadiel Michael alivyojutia kuondoka Yanga na kujiunga na Simba. Wakati akiwa Yanga alikuwa Roberto Carlos wao. Lazima acheze. Halafu ikatokea akaaminiwa katika kikosi cha Taifa Stars. Lazima acheze.

Ukatokea mgawanyiko wa mawazo kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Nani zaidi? Yeye au Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Gadiel akasifiwa kwa kukaba, Tshabalala akasifiwa kwa kushambulia. Mkataba wake na Yanga ukakata roho. Hapa ndipo ambapo hata mimi nimegawanyika kimawazo.

Mpira wetu ndio ulivyo. Kipesa umetengenezwa kwa ajili ya Simba na Yanga, halafu na Azam imejivuta. Kimapenzi umejengwa kwa Simba na Yanga pekee. Hakuna mchezaji anayetamani kucheza Azam au Namungo kwa mapenzi. Atacheza kwa ajili ya pesa.

Wakati huo Yanga haikuwa na GSM. Yalikuwa maamuzi rahisi kwa Gadiel kwenda Simba. Nadhani Azam haikuwa na mpango naye tena lakini pia alikuwa ameonja radha ya kucheza timu kubwa. Ukicheza timu kubwa unapendwa sana. Gadiel akaangalia kwanza mezani Simba kuna nini. Pesa ilikuwa inaongea.

Haya yalikuwa maamuzi ya kwanza ya mchezaji wa kisasa wa kulipwa. Kutazama pesa. Ndiyo, hii ni kazi kama kazi nyingine. Tunatazama pesa. Wanadamu ndivyo tulivyo. Tunatazama maslahi. Gadiel hakuwa mwanadamu wa kwanza kufanya hivyo. Na wala hatakuwa wa mwisho kufanya hivyo. Pesa. Ndiyo pesa. Pesa. Pesa.

Maamuzi mengine yangekuwa kumkwepa Tshabalala kwenye nafasi yake. Nani amechukua maamuzi haya? Yahaya Mbegu wa Singida Big Stars. Alitakiwa na Simba dirisha kubwa lililopita. Akawaambia wazi marafiki zake kwamba amejipima kwa Tshabalala lakini akaona hatoshi. Akakwepa pesa za Simba na kwenda zake Singida. Viongozi wa Simba mpaka sasa wanaamini Tshabalala na Shomari Kapombe wanaelekea mwisho kwahiyo wanatafuta warithi wao wa kudumu.

Kinachonishangaza ni kwamba wakati huu Gadiel analalamika ukweli ni kwamba alipenda pesa kuliko maamuzi ya rafiki yetu Mbegu. Kwanini? Ilitokea nafasi ya kumkwepa Tshabalala baada ya kumalizika mkataba wake Simba lakini akaongeza mwaka mwingine katika mkataba wake. Lazima aliwekewa pesa mezani. Kipi bora kuliko pesa? Aliwahi kuuliza James Hardley Chase katika kitabu chake cha What’s better than Money.

Gadiel angeweza kuchagua kukwepa. Lakini pia alikuwa na mlango mwingine mbele yake. Kupambania namba na Tshabalala. Sidhani kama alikuwa tayari. Wakati ule akiwa Yanga ilionekana hata kama kuna pengo kati yake na Tshabalala basi lilikuwa sio kubwa sana. Alipopewa nafasi katika baadhi ya mechi za Simba pengo likawa kubwa zaidi.

Ukweli ni kwamba tangu Gadiel atue Simba kiwango cha Tshabalala kiliongezeka zaidi na kumfanya awe mmoja kati ya mabeki bora zaidi wa upande wa kushoto upande huu. Nilichopenda ni kwamba hata nyakati hizi afadhali Gadiel anaijutia nafsi yake kwa kuhama Yanga kuliko labda angedai kwamba Tshabalala alikuwa anapendelewa na makocha. Hilo nimelipenda kutoka kwa Gadiel.

Lakini ushindani ni ushindani tu. Gadiel alipaswa kupambana kweli kweli kwa sababu hata Yanga asingeihodhi hii nafasi mpaka leo. Si leo tunaona wamekuja kina Joyce Lomalisa ambao viwango vyao ni vya hali ya juu. Vita haichagui silaha na wakati mwingine unapaswa kuwa tayari na adui yeyote yule.

Nini kifanyike kwa mfano huu wa kauli ya Gadiel? Kuna mambo mawili. La kwanza kabisa ni kwa kutafuta namna ya kuziongezea klabu zetu nyingine uwezo wa kipesa. Kuna wachezaji wanakwenda Simba, Yanga au Azam wakijua kabisa hawawezi kupata nafasi lakini wanakwenda kwa sababu uchumi wa klabu nyingine ni mdogo.

Kule nje mchezaji anaweza kuikataa nafasi ya kwenda Manchester City halafu akaangukia West Ham au Newcastle United. Hata hivyo, licha ya kuangukia huko lakini uwezo wa kipesa wa klabu hizo ni mzuri tu na watamlipa mshahara mzuri tu. Kama na City angelipwa Pauni 150,000 kwa wiki basi West Ham anaweza kulipwa Pauni 90,000 kwa wiki. Bado tajiri.

Tanzania pengo la walionacho na wasionacho ni kubwa. Mchezaji akikataa mshahara wa shilingi milioni sita wa Simba basi ataangukia katika mshahara wa shilingi laki nane wa Coastal Unioni au Mtibwa Sugar. Badala ha kupanda ndege kwenda Kigoma kucheza na Mashujaa yeye atapanda basi na wenzake. Safari ya siku mbili. Naambiwa Saidoo Ntibanzokinza alikuwa anajilipia nauli yake ya ndege kwa ajili ya kusafiri wakati akiwa Geita Gold. Pengo ni kubwa.

Fikiria timu kubwa kama Yanga ilijikwaa kidogo tu kipesa na haikumudu kupambania saini ya Gadiel alipomaliza mkataba wake licha ya kwamba ilimtaka. Inanikumbusha wachezaji kama Haruna Niyonzima, Ben Kakolanya na Ibrahim Ajibu. Kuna wakati walivuka boda kwenda Msimbazi kwa sababu mifuko ya Jangwani ilikuwa haieleweki. Ofa ya Simba ilikuwa nono zaidi. GSM hakuwepo. Labda angekuwepo angewazuia. Kama Yanga ikiteteleka kidogo bila ya mdhamini inakwama, vipi kwa Coastal Union?

Tukiachana na hilo la kwanza lakini pia wachezaji wetu waweke malengo ya mbali. Waangalie mbali zaidi. Gadiel aliona timu za kuchezea ni tatu tu. Azam, Yanga kisha Simba. Wenzetu wanaweka malengo ya mbali yanayopunguza mapato ya ndani. Ndio ukweli huu.

Nonda Shaban hakujuta kuwekwa benchi na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ au James Tungaraza ‘Boli Zozo’ wakati huo akicheza Yanga. Kumbe aliweka malengo ya mbali zaidi. Akajikuta anacheza Vaal Professional, kisha FC Zurich ya Uswisi, halafu Rennes ya Ufaransa, kisha AS Monaco ya hapohapo na baadaye Blackburn, Roma na Galatasaray.

Sisi mchezaji wetu anajuta kuhama Yanga kwa sababu malengo yake yapo hapa hapa mjini tu. Anajuta kuhamia mjini kwa sababu malengo yake yako hapa hapa nchini tu. Novatus Dismas hakuwa kuwa mchezaji tegemeo Azam lakini sidhani kama anajuta kusaini Azam. Leo anacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ligi za Afrika Magharibi ni mbovu. Wachezaji hawalipwi vizuri na ndio maana kina Pacome Zouzoua wako hapa. Mashirikisho la Afrika Magharibi pamoja na klabu yameshindwa kubadili mienendo na ndio maana chaguo la kwanza la kina Pacoume ni kuondoka. Sio lazima kwenda Ulaya tu lakini wameelekeza macho yao kokote ambako watalipwa vizuri nje ya mipaka.

Wakati mwingine huwa naamini Simba na Yanga haziharibu wachezaji wetu.

Wanajiharibu wenyewe tu na malengo ya muda mfupi na kutazama karibu. Ni tofauti na wachezaji wa nchi za wenzetu ambao wao daima mbele nyuma mwiko. Gadiel alikuwa na milango mingi ya kuchungulia katika maisha yake ya soka kuliko kujilaumu kuhama Yanga au kuhamia Simba.

Nilichopenda ni namna tu alivyokiri hadharani kuhusu kinachoisibu nafsi yake. Labda anaweza kubadilisha mawazo ya vijana wenzake wanapopata fursa kama yake.

Hauwezi kujua. Wakati mwingine kauli za watu maarufu zinaweza kubadili mitazamo ya watu katika jamii. Nimeongezea tu baadhi ya machache lakini lazima umpongeze kwa kukiri kilichomtokea

Columnist: Mwanaspoti