Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Fungate la Nabi Jangwani linakaribia mwisho

NABI KOCHA MKUU YANGA FD Nasreddine Nabi

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hauhitaji kuwa mtabiri mzuri kujua kwamba siku chache zijazo huenda kocha, Nasreddine Nabi asiwe kocha wa Yanga. Tunaweza kusikia ile kauli maarufu ya kwamba ‘pande zote mbili zimefikia makubaliano’.

Kama anahitaji kuendelea katika nafasi yake basi Yanga watalazimika kufanya maajabu nchini Tunisia kwa kuitoa Club Africain katika pambano la marudiano kufuzu makundi michuano ya Shirikisho. Kwanini wanahitaji maajabu? Naam, itakuwa maajabu haswa.

Katika mechi tatu kali za kimataifa zilizopita za Yanga, nikimaanisha dhidi ya Al Hilal nyumbani na ugenini, na kisha pambano lililopita dhidi ya Watunisia hawa, Yanga walifanikiwa kufunga bao moja tu la juhudi binafsi za Fiston Mayele. Pambano lililopita dhidi ya Watunisia Yanga wangeweza kucheza dakika 300 bila ya kufunga bao.

Tatizo ni ubora wa wapinzani au ubutu wa Yanga? Bahati mbaya mashabiki wameondoka na hilo jibu la pili. Wanaamini kwamba Yanga wapo butu kwa sababu ya mbinu za Nabi. Kama kuna kitu watu wa Yanga waliamini mwanzoni mwa msimu ni kwamba wana timu ya kucheza na kina Al Ahly au Wydad Casablanca achilia mbali hawa kina Al Hilal.

Yanga ya ndotoni mwa kila shabiki wa Yanga ni hii hapa. Walikuwa wanazungumza, “hapa kuna Mayele pale kuna Stephane Aziz Ki, kule kuna Bernard Morrison huku kuna Fei Toto kwa Mkapa hatoki mtu”. Sasa hivi hadithi hii haipo, Yanga wameshikilia roho zao katika michuano ya pili kwa ukubwa barani Afrika ngazi ya klabu.

Kwanza wametolewa Ligi ya Mabingwa halafu sasa hivi wanakaribia kutolewa Shirikisho. Yote haya ni katika hatua ya awali. Hapo katikati kulikuja na uvumi kwamba huenda Nabi angepigwa mkono wa kwaheri lakini Yanga wakapoza upepo baada ya kugundua kwamba isingekuwa sawa kuachana naye kwa wakati huo. Walimuhitaji katika mechi za Shirikisho.

Kwa upepo ulivyo sasa ni wazi kwamba hali ni ngumu kwa Nabi. Wakati ule ulipokuja uvumi kwamba anaweza kuondolewa mashabiki waligawanyika. Lakini majuzi baada ya pambano la Jumatano kundi la wale ambao walikuwa wanamuhitaji limemeguka zaidi. Wamejiunga na wale ambao walikuwa hawamtaki tangu baada ya matokeo ya Al Hilal.

Ndani ya uwanja katika mechi hizi Yanga wanashindwa kucheza kama timu lakini pia kwa wachezaji mmoja mmoja hakuna ambaye yupo katika ubora wake, labda golikipa Djigui Diarra. Yanga pia haionyeshi udharura wowote wa kusaka matokeo. Hawachezi katika kiu ya juu ya kujaribu kupata matokeo. Wachezaji kama kina Tuisila Kisinda wamekuwa wabinafsi tu bila ya kujua umuhimu wa mechi.

Tatizo katika mchezo huu hauwezi kuondoa wachezaji wote. Unamuondoa kocha. Inawezekana Injinia Hersi Said na watu wake labda wanamkubali Nabi lakini presha ambayo watapata kutoka kwa mashabiki itakuwa kubwa na sioni mtu wa kuhimili presha hiyo hasa ukizingatia kwamba na wenyewe ni wachanga katika kuendesha timu hizi.

Kinachowaumiza Wanayanga ni mambo mawili. Kwanza wameshathibitisha ubora wao katika kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Iweje wao ambao ni mabingwa huku wakisadikika kuwa na wachezaji bora kuliko wapinzani wao washindwe kusonga mbele halafu wapinzani wao ambao walishika nafasi ya pili waendelee kupeta hadi hatua ya makundi?

Lakini hapo hapo Yanga wanajikumbusha tu kwamba kutwaa ubingwa kwao sio habari mpya. Tayari walishatwaa ubingwa mara 27 kabla ya Nabi kufika. Inawezekana wanamshukuru kwa kuwapa taji la 28 lakini ubingwa sio habari kubwa Jangwani.

Katika dunia ya leo ya utandawazi Yanga wanataka kuiona timu yao ikifanya vema kimataifa. Watu washazoea kuzifuatilia timu mbalimbali za Ulaya na Afrika katika michuano ya ndani na ya nje. Kwanini isiwe kwa Yanga? Ndicho ambacho mashabiki wa Yanga wanaumia.

Lakini hapo hapo kinachowakoroga mashabiki wa Yanga ni namna ambavyo timu yao imekuwa ikimtawala mtani wake Simba katika miaka ya karibuni. Inakuwaje wanakuwa bora katika mechi dhidi ya mtani halafu wanadorora katika mechi za kimataifa. Yanga wameanza kuchoshwa na hali hii. Wanaamini kwamba akili ya maandalizi dhidi ya Simba inapaswa kwenda katika kiwango kile kile wanapocheza mechi za kimataifa.

Kwa staili hii sidhani kama Nabi atapona. Atakumbukwa kwa ubingwa ambao Yanga wameupata baada ya mtani kuuchukua mara nne mfululizo, lakini atakumbukwa pia kwa kumsumbua mtani mara nyingi. Tangu afike nchini April 2021 Nabi amefungwa mara moja tu na Simba pale Kigoma. Lakini haya yote hayatamsaidia pale litakapokuja suala la mechi za kimataifa.

Mechi hii dhidi ya Club Africain inabakia kuwa moja kati ya mechi muhimu ambazo Nabi amewahi kusimamia katika maisha yake ya soka. Sijui atazichanga vipi karata zake lakini ndani ya uwanja anaweza kupata unafuu fulani kama wachezaji wake wakichangamka zaidi.

Katika pambano la kwanza wapinzani wao walicheza soka la kujihami kwa umakini mkubwa zaidi. Walimzunguka Mayele na kukata huduma zote ambazo zingemfikia. Lakini pia walicheza kwa lengo la kupoteza muda zaidi ambapo muda mwingi wa mchezo wachezaji wao waliishia kujiangusha.

Wakiwa kwao Club Africain watacheza tofauti. Hawatajihami wala kujiangusha. Watacheza kwa kasi na kuishambulia Yanga kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo mpaka ya mwisho. Yanga watapimwa kwa mambo mawili. Kwanza uwezo wao wa kuhimili presha na mashambulizi ya haraka ya wapinzani.

Baada ya hapo watahitajika kujibu mapigo ya kupishana na wapinzani wao. Hii itakuwa fursa kwao kwa sababu wana wachezaji wa pembeni wenye kasi ya kuanzisha mashambulizi hayo. Kitu kikubwa ni namna ya kudhibiti kwanza mashambulizi ya wapinzani wao.

Suluhu waliyoipata nyumbani sio mbaya. Hawakufungana. Hii ina maana kwamba sare yoyote ya mabao ugenini inaweza kuipitisha Yanga. Je wataweza kuwazuia Club Africain wasifunge? Na kama wataweza kufanya hivyo bado wanaweza kujipatia bao la ugenini kama wapinzani wao wakipata bao?

Nabi na wachezaji wake wanaweza kutupa majibu lakini vyovyote ilivyo hii ni mechi ambavyo imeshikilia hatima ya Nabi pale Jangwani. Matokeo yoyote ambayo ni kinyume na Yanga kupitia basi tutasikia tu kwamba ‘pande zote mbili zimefikia makubaliano ya kuachana’. Ukisikia hivyo ujue mtu amefukuzwa.

Columnist: Mwanaspoti