Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Franco Bares Kisiki cha Kitaliano kilichoacha heshima Milan

Franco Baresi Franco Bares Kisiki cha Kitaliano kilichoacha heshima Milan

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Italia ilipokosa nafasi ya kucheza fainali za Kombe Dunia nchini Qatar mwaka jana lilikuwa ni tukio ambalo lililowashangaza wengi na gazeti moja la nchini humo lilitoka na uchambuzi uliokuwa na suala lililowachekesha mashabiki wa kandanda wa nchi hiyo.

Nalo ni kuwauliza wachezaji mashuhuri wa zamani Paolo Maldini, Franco Baresi, Roberto Baggio, Gianluigi Buffon, Fabio Cannavaro, Francesco Totti, Gianni Rivera, Giuseppe Meazza na Paolo Rossi "kwa nini walizaliwa mapema na sasa wakongwe hawawezi kuitetea Italia katika soka?"

Gazeti hilo liliamini Baresi, mlinzi mahiri wa Italia wa miaka ya 1990 ambaye sasa ana miaka 63, licha ya uzee angeilinda Italia isifungwe kuliko vijana waliopambania tiketi ya fainali za kwenda Qatar.

Baresi alisifika kwa utii wake kwa AC Milan na kuwa nayo tangu akiwa kijana hadi alipostaafu tofauti na wachezaji wa sasa wanaoweka mbele pochi na sio ushindi au mapenzi kwa klabu. Baresi alichezea AC Milan kwa miaka 19 kutoka 1978 hadi alipostafu 1987.

Alikataa vishawishi vya kujiunga na klabu zingine za Italia na nje na kusema kuiacha AC Milan ilikuwa sawa na mtu kumkimbia mzazi wake. Aliteremka nayo uwanjani mara 444 katika Ligi Kuu na iliposhuka madaraja alisema hata kama AC Milan ingekufa angebaki nayo kama yatima au kuzikwa nayo.

"Kila siku ningeliangalia kwa huzuni jengo la klabu hii ninayoipenda kama nifanyavyo kwa kaburi la mama yangu,” aliwahi kusema mchezaji huyo enzi zake wakati akiitumikia. Mapenzi yake kwa AC Milan yalimfanya hata mtoto wake wa kiume kumpa jina la utani la Milano.

Alipostaafu klabu iliamua namba 6 jezi namba aliyoivaa isivaliwe na mchezaji mwingine wa klabu hiyo kuonyesha heshima kuwa hakuna atakayefanana na Baresi.

Rais wa zamani AC Milan na mmiliki wa klabu hiyo, Silvio Berlusconi alipokuwa Waziri Mkuu wa Italia alitoka bungeni kwenda kuangalia mchezo wa kumuaga Baresi alipostaafu. Zaidi ya watu 50,000 walihudhuria na Baresi alifunga bao lililosababisha mamia ya watazamaji kutokwa na machozi.

Baresi amabaye aliitwa “beki mwenye miguu ya chuma” alikuwa mkakamavu licha ya umbo hafifu na alipambana na wachezaji wa miraba minne waliohaha kutafuta mabao. Kukubalika mtu dhaifu kuwa beki Italia lilikuwa jambo la ajabu katika nchi hiyo inayopenda mchezo wa kujihami kwa kutumia wachezaji wenye kuhimili ubabe, lakini licha ya kuwa dhaifu Baresi aliwakaba washambuliaji vizuri. Aliusoma mchezo vyema. Aliuhodhi mpira kwa ustadi na kutoa pasi za uhakika.

Alisubiri hadi 1990 kuingizwa katika kikosi cha Italia kilichocheza Kombe la Dunia, miaka 12 baada ya kuanza kucheza Ligi Kuu ya Italia (Series A). Alikuwemo katika kikosi cha Italia kilichobeba Kombe la Dunia 1982, lakini hakucheza kwa sababu kocha Enzo Bearzot aliwapendelea zaidi mabeki wa Juventus kina Cabrini, Gentile na Scirea.

Aliposhiriki fainali za Kombe la Dunia 1990 aliumia katika mchezo wa kwanza Italia ilipokutana na Norway, lakini alirudi katika mchezo wa fainali wiki nne baada ya kupasuliwa goti. Mchezo wake ulivutia na wengi hawakuamini mtu aliyepasuliwa goti wiki chache zilizopita kucheza kwa ujasiri kama alivyowabana kina Romario na Bebeto wa Brazil kwa dakika 120.

Kwa bahati mbaya alikuwa mmoja wa wachezaji waliokosa penalti baada ya mchezo kumalizika sare dakika 120 na Brazil ikabeba kombe. Jina la eneo alilozaliwa Mei 8, 1960 linaitwa Travagliao, likiwa na maana ya usumbufu na lilikuwa na uhusiano wa karibu na maisha ya utotoni ya Baresi.

Mama yake alifariki dunia akiwa na miaka minne na yeye na kaka yake, Giussepe walilelewa na dada yao Lucia katika hali ngumu. Kila shida zilipozidi alikwenda kwenye kaburi la mama yake na kumwambia: "Usisikitike. Haya ndio maisha na tutafanikiwa. Pumzika kwa amani."

Kumbe alikataliwa

Katika mchezo Baresi alikabiliana na matatizo kabla ya kupata nafasi ya kuonyesha umahiri wake. Mara mbili alijaribu kujiunga na AC Milan na kukataliwa kutokana na udhaifu wa mwili wake.

Marafiki zake walimtaka aisahau AC Milan, lakini alijaribu kwa mara ya tatu na kupokewa akiwa na miaka 14 kwa kumuonea imani kuwa aliipenda klabu.

Akiwa na miaka 18 aliichezea AC Milan kwa mara ya kwanza na msimu uliofuata alitoa mchango mkubwa uliochangia kuchukua ubingwa mara 10. Alipoifungia AC Milan bao lake la kwanza, Baresi alilia kwa furaha na kusema lilikuwa zawadi ya mama yake ambaye japokuwa hakuwepo duniani alikuwepo moyoni mwake.

Mwaka uliofuata AC Milan iliteremshwa daraja kwa kashfa ya rushwa. Wachezaji wengi walihama, lakini Baresi alibaki akisema alikuwa Milan na Milan ni yeye. "Nimezaliwa karibu na San Siro. Nitabaki hapa na namuomba Mungu nimalizie maisha yangu hapa,” alisema.

Baresi na wenzake waliirudisha AC Milan Series A na alikuwemo katika kikosi cha Italia kilichobeba Kombe la Dunia 1982, lakini alikuwa pembeni kwa vile nafasi yake ilihodhiwa na Gaetano Scirea.

“Siombi Gaetano aumie au augue, lakini ikitokea kucheza mtaelewa nani zaidi mimi au yeye,” alikaririwa akisema akiwa katika benchi la wachezaji wa akiba. Baada ya michezo 716 kwa klabu na 81 Italia alisema basi.

Siku alipoagwa alisema: "Najua mnataka niendelee. Sijabadilika kwa jina au mapenzi yangu kwa AC Milan na Italia, lakini uwezo wa kucheza umepungua na umri unakataa. Ni vizuri mkanibeba kwenda nyumbani kupumzika badala ya kunichukua uwanjani na kunipeleka hospitali au kaburini.”

Alipostaafu alikwenda Uingereza kufundisha kwa muda mfupi Fulham iliyokuwa inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Kiarabu, Mohamed Al Fayed. Pia alifundisha timu ya wanawake na alipotakiwa kuifundisha timu ya wanaume alisema anawapenda wanawake kwa vile mama yake na mke wake ni wanawake. Baadaye alirudi Italia na sasa ni mmoja wa washauri wa AC Milan.

Columnist: Mwanaspoti