Sakata la nyota wa soka Tanzania, Feisal Salum Abdallah 'Fei Toto', na klabu ya Yanga bado halijapata ufumbuzi na mamlaka za soka nchini zinaendeleza danadana zake.
Aprili 12 kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ilitakiwa kukutana kulijadili tena sakata hilo katika muktadha tofauti kidogo...safari hii yalikuwa maombi ya Feitoto kuvunja mkataba. Lakini kamati ikaahirisha kulisikiliza shauri hilo hadi Mei 4.
Wakati tarehe hiyo inasubiriwa, Jumamosi ya Aprili 15, Feisal mwenyewe aliposti kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akinukuu vifungu vya FIFA na hatua zinazopaswa kuchukuliwa panapotokea sakata kama lake.
Feitoto alinukuu kifungu cha 17(1) cha sheria za hadhi na uhamisho wa wachezaji cha shirikisho la soka la kimataifa, FIFA.
Katika mashauri yote, upande utakaokiuka mkataba utatakiwa kulipa fidia. Halikadhalika, endapo kamati itabaini kwamba mchezaji alikiuka mkataba kwa kuuvunja pasipo kufuata taratibu za kisheria kabla haujaisha, hatua pekee ambayo kamati inapaswa kuchukua ni kumlipisha fidia.
Sehemu ya tatu ya kifungu hiki inasema mchezaji halazimishwi kubaki kwenye klabu asiyoitaka.
Wakati wa kuzingatia hatua za kuchukua kwa kuvunjika kwa mkataba, mchezaji halazimishwi kuendelea kuajiriwa na klabu ambayo mkataba wake umevunjika kwa namna yoyote( iwe umevunjika kwa njia halali au njia zisizo halali) na pia klabu hailazimishwi kumuajiri mchezaji wa aina hiyo.
Upande wowote wa mkataba ukiamua kuuvunja, iwe kihalali isiwe kihalali, mkataba unahesabiwa umeshavunjika. Kinachofuata baada ya hapo ni kwa hatua za kuchukuliwa ikibainika uvunjaji haikuwa kihalali.
Kifungu hiki ni kirefu na kina maelelzo mengi sana huko mbele yenye kufafanua zaidi juu ya sakata kama hili.
Nimechukua maelezo hayo mafupi ili kutoa mwanga wa kile kinachoendelea.
Kinachofafanuliwa na sheria hii hapa ndicho kinachomhusu Feitoto na kimsingi kinafanana na sakata la Rafael Leao, nyota wa sasa wa klabu ya AC Milan ya Italia.
Mchezaji huyo raia wa Ureno aliyekulia kwenye akademi ya klabu ya Sporting, aliingia mgogoro na klabu hiyo iliyomlea na kuvunja mkataba wake 2018.
Kisa cha kuvunja mkataba wake ni shambulio walilofanyiwa wachezaji na mashabiki wa klabu hiyo walipokuwa mazoezini.
Mei 15, 2018, kundi la mashabiki takribani 40 walivamia mazoezi ya timu hiyo na kuwashambulia kwa vipigo wachezaji.
Leao na wenzake nane wakavunja mikataba yao kwa sababu za kiusalama. Yeye akatimkia klabu ya Lille ya Ufaransa kama mchezaji huru, halafu kutokea hapo akauzwa kwenda AC Milan ya Italia 2019, aliko hadi sasa.
Lakini klabu yake ya zamani, Sporting, haikuridhika na namna mchezaji huyo alivyovunja mkataba, ikapeleka malalamiko yake FIFA na CAS.
Baada ya shauri kusikilizwa, ikaonekana kwamba Leao alivunja mkataba kinyume na taratibu, akatakiwa kulipa fidia ya takribani dola milioni 15.
Hicho ndicho alichokinukuu Feisal kwenye sheria za hadhi na uhamisho wa wachezaji ya FIFA.
Mchezaji anapobainika kukiuka mkataba ikiwemo kuuvunja pasi na kufuata taratibu, anatakiwa aadhibiwe...alipe fidia kwa kukiuka mkataba.
Rafael Leao hakuambiwa arudi kwenye klabu yake eti kwa sababu hakufuata taratibu kwenye kuvunja mkataba. Kama hakufuata taratibu maana yake alikiuka, na kama alikiuka maana yake alifanya makosa, na kama alifanya makosa maana yake anastahili adhabu...na adhabu yake ni kulipa fidia.
Sijui kwanini kamati zetu hazioni hayo ambayo yako wazi kabisa na sijui kwa nini kambi ya Fei bado anahangaika hapa hapa nchini na kamati ile ile ambayo imeshindwa kuyaona yaliyo wazi tangu mwanzo.