Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Fabrizio Romano, Mwandishi anayeteka Soko la Usajili barani Ulaya

Fabrizio Romano Maajabu Fabrizio Romano, Mwandishi anaesifika kwa tetesi za usajili Barani Ulaya

Sun, 17 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nilikuwa katika hoteli ya Royal Palm jijini Accra Ghana Februari 2007. Nisikilize vema. Sikuwa nimefikia hotelini hapo kabla. Nilikuwa nakwenda kumtembelea Rais wa wakati huo wa TFF, Leodeger Tenga ambaye alikuwa mmoja kati ya watu wazito CAF. Michuano ya Afcon ilikuwa ikiendelea Ghana.

Katika hoteli hii walikuwa wamefikia watu wazito. Jose Mourinho, ambaye alikuwa amefukuzwa na Chelsea. David Dein, Makamu wa Rais wa Arsenal. Issa Hayatou, aliyekuwa Rais wa CAF. Na vigogo wengine mbalimbali wa soka Afrika na duniani.

Bahati iliyoje, nikiwa nimekaa katika kochi na baadhi ya waandishi wa nchi mbalimbali za Afrika akaingia Abeid Ayew Pele. Sijui alikuja kufanya nini. Nilimtazama kwa jicho la husuda. Abeid, bishoo kama alivyo. Alikuwa ana hereni mbili katika masikio yake. Mwili wake ulikuwa umetakata. Mavazi nadhifu. Hakuonekana kama mstaafu miongoni mwa wastaafu tuliowazoea barani Afrika.

Umri ulikuwa umemtupa lakini alionekana kama baharia. Hakutaka kuzeeka. Nje alikuwa amepaki gari la aina ya Hammer. Kila mtu alimuita kwa jina lake. ‘Peleee’. Mwingine aliita ‘Abeid’. Kuna kitu kilinishangaza zaidi.

Ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona ‘live’ Abeid Pele. Kwanini nisipige naye picha? Kwanini hasa? Nilinyanyuka nikamfuata. Tukapiga picha. Kilichonishangaza ni kwamba nilijikuta ni peke yangu ambaye nilikuwa nimepiga picha na Abeid.

Waandishi wengine walikuwa wanapiga naye soga za kawaida huku wakimtania. Mwandishi mmoja alikuwa akimlalamikia Abeid kwanini hawakuonana jana usiku. Nikagundua kitu. Kitu ambacho kimenifanya nimfikirie Mwandishi maarufu wa habari za uhamisho wa mastaa wa soka wanaotamba duniani kwa sasa, Fabrizio Romano.

Romano mwenye umri wa miaka 29 ana wafuasi 8.3 milioni katika mtandao wa Twitter peke yake. Ana wafuasi 7.8 milioni katika mtandao wa Instagram. Anabakia kuwa Mwandishi anayeaminika zaidi katika katika masuala ya uhamisho wa wachezaji barani Ulaya na duniani kote.

Romano anaonekana kufanya maajabu katika masuala ya habari ya soko la uhamisho duniani. Kila mara yupo. Kila taarifa anayo. Bahati nzuri taarifa zake ni za uhakika. Nitaanza kukupa silaha moja moja ambazo Romano anazitumia kufanikisha mambo yake.

‘Here we go’ ni kauli yake maarufu ambayo haiji bure. Nimekuletea mfano wa mimi na Abeid Pele kujaribu kuanza kukuelewesha namna ambavyo waandishi wenzetu wana mahusiano makubwa na mastaa. Wanaishi nao kila siku na wamewazoea.

Binafsi akili yangu ilinituma kupiga picha na Abeid Pele, lakini waandishi wenzangu wanakutana na Abeid Pele kila kukicha. Wanakutana na Abeid Pele katika michuano mbalimbali ya soka, wanakutana naye katika mikutano ya uchaguzi, wanakutana naye katika makongamano na semina. Wanakutana na Abeid kila mahala na hawana mpango wa kupiga naye picha tena.

Miongoni mwa waandishi wa namna hii yupo Fabrizio Romano. Achilia mbali Abeid Pele yeye atakutana na Fransesco Totti, Ronaldo de Lima, Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Kylian Mbappe na wengineo. Haya ndio maisha yake ya kila siku.

Romano alipoamua kujikita katika masuala ya uhamisho wa mastaa wa soka ni kwamba sababu anafahamiana na wachezaji, mawakala, wazazi wa wachezaji, mabosi watendaji, wafanyakazi wa hoteli na kila mtu. Hapa ndipo kazi yake inapokuwa rahisi.

Kwa mfano, ni rahisi kwa Romano kumuuliza Abeid Pele kuhusu hatma ya Jordan Ayew katika kikosi cha Crystal Palace na akapata habari za ndani. Pele hawezi kufunguka kwangu kwa sababu ndio kwanza ameniona. Hawezi kuniamini. Lakini anaweza kumuamini Romano ambaye amebadilishana namba miaka sita iliyopita na wamekuwa wakichati mara nyingi.

Pele anaweza tu kumwambia Romano kwamba kuna ofa ya Atletico Madrid kwenda kwa mwanae. Akampa maelezo kwamba wameshakubaliana kuhusu mshahara na baadhi ya vipengele vipengele vingine.

Uzuri wake ambao unamjengea imani kutoka kwa watoa taarifa wengine (Sources) ni kwamba Romano haaniki watoa taarifa wake hadharani. Umewahi kuona Romano anataja mahala alipopata hizo taarifa? Hapana!

“Arsenal are confident on Youri Telemans to join the club as the next signing. Official bid will be improved in order to reach full agreement with Leicester City”.

Unajua ni wapi ambapo Romano anaweza kuwa ameipata hii habari? Nimekupa chanzo cha kwanza kabisa. Wazazi au ndugu wa mchezaji mwenyewe. Inawezekana akawa na urafiki wa karibu na mchezaji au ndugu ambaye anamuelezea dili lilipofikia.

Wakati mwingine inakuwa ngumu kwa klabu zote mbili kumueleza Romano habari zozote za maana, lakini leo nimekupa chanzo cha kwanza cha Romano. Ndugu. Ni kama ambavyo nimekupa uhusiano niliouona kati ya Abeid Pele na Waandishi wa Habari. Kuna mtu ambaye anaweza kujua nyendo za Jordan na Andre Ayew zaidi ya baba yao mzazi? Tofauti ni kwamba wazazi wa mastaa wengi wa soka la Tanzania huwa hawana uhusiano wa karibu na watoto wao. Walau siku hizi kuna Mameneja au mawakala ambao Romano angeweza kufanya nao kazi Tanzania lakini maelfu ya wanasoka walio Tanzania hawana mawakala wala Mameneja.

Ni ngumu kwa Romano kushughulikana na wazazi wa wachezaji kwa sababu wanakuwa hawajui chochote kinachoendelea katika mazungumzo ya watoto wao na klabu zao au klabu wanazotarajiwa kuhamia. Nimekudokeza kidogo kuhusu maajabu ya mtu anaiyeitwa Fabrizio Romano ambaye ameiteka dunia ya soka katika suala la uhamisho wa wachezaji.

Unataka nikupe maajabu mengine ya Fabrizio Romano? Hakuna maajabu sana. Simu yake inaweza kuwa na namba 2,000 za watu mbalimbali duniani. Lakini kuna namba ‘ameisevu’ kwa jina la Jorge Mendes.

Kuna namba ameisevu kwa jina la Mino Raiola. Kuna namba ameisevu kwa jina la KIA Joorbachian. Usidhani amewapachika watu fulani majina ya uongo. Ni majina ya mawakala maarufu duniani. Mawakala wakubwa na wadogo.

Hapa kuna kamchezo kanaendelea kati ya Romano na mawakala. Ni marafiki wa karibu. Bahati nzuri wote wanasaidiana. Huyu akifanya kazi yake vizuri basi anamsaidia mwenzake.

Romano anaweza kutulia katika mgahawa wa Enrico Bartloni jijini Milan. Ghafla simu yake ikalia. Jina linaonekana Jorge Mendes. Nyuma ya pazia kuna mazungumzo ambayo yanafanyika.

Jorge anamwambia Romano mteja wake, Cristiano Ronaldo anaweza kuondoka Manchester United kama atapata ofa sahihi kwingineko.

Dakika moja baadaye atamwambia Roma wameonyesha nia na wamempigia simu. Kwa nini Mendes anamwambia Romano.

Sio tu kwa sababu ya urafiki wao, lakini anajua Romano akienda kuandika Twitter, klabu nyingine zitasoma habari yake na zinaweza kuonyesha nia kwa Ronaldo.

“Ronaldo is open to quit Manchester United this summer and AS Roman have shown the interest.” Romano anakuja kwetu kutuandikia hivi.

Hii ni habari njema kwa Jorge Mendes kwa sababu anajua kuna timu zitataka kuipiga kumbo Roma kwa ajili ya kumpata mteja wake.

Hapa Romano anakuwa amemsaidia Mendes, pia Mendes anakuwa amemsaidia Romano kuipata habari ambayo wengine hawana. Na baada ya hapa unajua kinachofuata? Ghafla simu ya Mendes itaita. Kutoka wapi? Chelsea.

Wanamwambia wafahamishwe kuhusu maendeleo ya Ronaldo na uwezekano wake wa kuondoka katika dirisha.

Hapo Chelsea wanakuwa wameipata habari hii kutoka kwa Romano. Mtu wa kwanza kupewa mrejesho wa ofa ya Chelsea kutoka kwa Mendes atakuwa Romano.

“Chelsea wamepiga simu ya kuulizia kama Ronaldo anapatikana katika dirisha hili.”

Ikifika hapa, Romano anarudi kwetu tena na kutuambia “Here we go again, Chelsea are on race to sign Ronaldo if he will decide to quit Old Trafford.” Uzuri ni Romano anafanya kazi kwa uaminifu na hatuambii chanzo chake. Anaishia hapo hapo.

Hawezi kutuambia chanzo chake ni wakala wa Ronaldo. Lakini kila maendeleo ya Ronaldo na masuala ya uhamisho Romano anakuwa wa kwanza kuripoti kwa sababu ya chanzo chake cha uhakika ambacho ni Mendes.

Wakala gani hatataka kufanya kazi na Romano? Anawasaidia kufanya kazi zao za udalali. Romano hawezi kuwa kila mahala, lakini ana namba za simu za mawakala wa mastaa wa Afrika, Amerika Kusini, Ulaya, Amerika Kaskazini na kwingineko.

Kumbuka wakati akifanya hivyo na Mendes, simu yake nyingine inafanya hivyo kwa Raiola ambaye anakuwa anamfahamisha kila maendeleo kuhusu Romelu Lukaku. Simu aliyotumia kuongea na Mendes ikikatika inaingia simu ya wakala wa David Luiz, Giuliano Bertolucci.

Simu yake inapata joto kila dakika. Kuna habari ambazo anazitafuta na kuna habari ambazo zinamtafuta kwa ajili ya kuongeza thamani za wachezaji. Katika biashara ya kisasa, mchezaji hapaswi kuwindwa na klabu moja tu. Ili wakala apate dili zuri mchezaji anapaswa kuwindwa na klabu nyingi.

Mtu anayeaminika zaidi kwa sasa ni Romano. Anaaminika kuliko hata Skysport au BBC. Hivyo ni rahisi kwa wakala kuisaka namba ya Romano kuliko yeye kusaka namba za mawakala. Uzuri ana namna ya kuchuja habari hizi na kutozithibitisha kama hana uhakika.

Wakala ndiye ambaye anamwambia mchezaji anakwenda kupimwa afya keshokutwa. Ingawa klabu hazipendezwi na kuvuja kwa habari hizi, lakini wanakuwa hawana jinsi kwa sababu wanashindwa kudhibiti urafiki wa wakala na Romano.

Lakini hapo hapo ni ngumu kwa klabu kujua habari za usajili zimevuja wapi kwa sababu Romano anaweza kuwa na uhusiano wa karibu na watu wa ndani ya klabu kama ambavyo nitaelekeza katika mtiririko huu.

Katika uhamisho wa mchezaji kuna watu wengi wanahusika. Wanasheria, maskauti, wafanya mazungumzo (negotiators).

Ni ngumu kwa klabu kujua ni wapi habari yao imevuja, ingawa kila siku klabu huwa zinafanya siri suala la uhamisho wa mastaa kwa sababu ya kuogopa upinzani kutoka katika klabu nyingine ambao utaongeza dau la mchezaji.

Jaribu kuangalia namna ambavyo Arsenal ilifanya siri kuinasa saini ya Fabio Vieira. Imekuja ghafla tu, lakini hata hivyo dakika za mwisho ilivuja. Sio mchezaji ambaye sakata lake lilidumu kwa muda mrefu.

Unaweza kuona namna ambavyo sakata la Gabriel Jesus lilizungumzwa kwa muda mrefu kabla yake.

Ni nadra pia kwa wakala kumdanganya Romano kwa sababu anajua atamhitaji tena katika biashara za siku za usoni.

Kama Mendes akimdanganya Romano kuhusu dili yake moja, ni rahisi kwa Romano kulalamika ameingizwa chaka.

Siku nyingine simu ya Mendes ikilia katika simu ya Romano kujaribu kumweleza kuhusu dili fulani kwa lengo la kumpandisha bei, Romano anaweza kukataa huku akitoa shutuma za namna alivyoingizwa chaka katika uhamisho fulani uliopita.

Uaminifu kati Romano na mawakala ndio huu ambao kila siku umekuwa ukitupa habari za uhakika ambazo zimemfanya Romano atambe kwa kiasi kikubwa.

Ni uhakika huu huu ambao unamfanya aweze kuandika kwamba ‘Dili limekamilika kwa asilimia mia”.

Romano amewekeza katika namba za simu za mawakala kwa kiasi kikubwa. Endelea kumuamini. Hana maajabu ya kuota dili fulani limekamilika. Hayupo kila mahala ila simu yake inaitwa kila mahala.

Kwa jinsi ambavyo amejijengea mtandao wake ilikuwa rahisi kwake kuaminika kwa kiasi kikubwa kuliko vyombo vingine vya habari.

Alikuwa anajua nini anakitaka wakati akianza kusaka habari hizi. Nitakunong’oneza kitu kingine ambacho kinamfanya Romano aonekane anafanya maajabu.

Wazungu wana misemo mbalimbali inayovutia. Celine Dion aliwahi kuimba wimbo uliosema ‘Kama kuta zingeongea’‚ Halafu James Hardley Chase, mwandishi mahiri wa vitabu wa zamani aliwahi kuandika kitabu kilichosema ‘Fanya mzoga utembee’. Chase huyo huyo aliwahi kuandika kitu kilichoitwa ‘Weka sikio ardhini usikilize’.

Katika ubora wao, kuna baadhi ya watu wanasababisha kuta ziongee. Wanasababisha mzoga utembee. Lakini ni wachunguzi kiasi kwamba wanawema kutega sikio ardhini kwa utulivu mkubwa kiasi cha kusikia mazungumzo yanayoendelea chini ya ardhi.

Katika uandishi wa habari kuna habari ambayo lazima ipatikane. Ni lazima na hakuna mjadala. Unatumia mbinu zozote za ujasusi kupata habari hizo. Unapata mazungumzo ya watu wakati haukuwapo. Unasikiliza mazungumzo ya watu wakati haukuwapo.

Wakati mwingine yote haya yanatokana na pesa. Msukumo wa pesa unasababisha haya. Fabrizio Romano ana mtandao mkubwa kutoka kwa baadhi ya watu wa makao makuu wa klabu zote kubwa na ndogo barani Ulaya na kwingineko.

Inasemekana wote hawa wapo katika malipo yake. Romano anajua ambacho kinaendelea katika Headquarters za Manchester United pale jijini Manchester. Inawezekana katika mzunguko ule ule wa watu ambao nimewataja. Labda mwanasheria, labda mwakilishi wa mazungumzo, labda daktari wa klabu ambaye atahusika kumpima afya mchezaji mtarajiwa.

Fanya hawa watu waongee ukweli wao. Kuna habari ambayo Mendes anaweza kumwambia Romano kuhusu mteja wake, lakini kuna habari ambazo hawezi kujua hasa ile ambayo inahusu fikra za mabosi wa timu husika.

Kwa mfano, inawezekana kabisa Manchester United inamtaka mteja wa Mendes. Lakini inawezekana pia inamtaka mchezaji anayemilikiwa na Mino Raiola. Inawezekana kuna nafasi moja tu baina ya wachezaji hao wawili. Inawezekana United imewasiliana na Raiola pamoja na Mendes ambao wote wamemwambia Romano.

Lakini kati ya hawa hawajui hasa klabu itaamua kwenda kwa mchezaji gani baina ya hao wawili. Hapo ndipo Romano pia analazimika kuwa na watu wa ndani. Utasikia tu Romano anatuambia pale Twitter ‘Manchester United imeamua kuachana na mpango wa kumchukua Frenkie de Jong na sasa itapeleka macho yake kwa Ruben Neves wa Wolves‚‘. Hii itakuwa ni habari ambayo Romano ameipata kutoka kwa watu wa ndani.

Pia wakati mwingine timu inatoswa katika dau lake la kwanza dhidi ya mchezaji fulani. Inapofikiria kurudi tena na dau la pili ni kitu ambacho wakala wa mchezaji huenda asifahamu. Wanaojua kwamba watarudi na dau la pili au wataachana na mpango wenyewe ni viongozi.

Hapo ndipo Romano anaegesha sikio lake kwa umaridadi mkubwa. Utasikia tu, anatuambia ‘Manchester United imekataliwa katika dau lake la kumtaka De Jong na sasa inafikiria kurudi na dau la pili la pauni 67 milioni’.Habari hii inakuwa imevuja klabuni.

Lakini hapa kuna pande tatu. Kuna upande wa wakala, upande wa klabu inayonunua pia upande wa klabu ambayo inauza. Kwa habari kama hii, Romano lazima awe ameegesha sikio lake ndani ya Barcelona. Hapo ni lazima apate maoni ya Barcelona.

Yaani lazima ajue ni dau gani hasa linaweza kuwashawishi Barcelona kumuuza hata kama hawatafika katika dau la awali la pauni 75 milioni ambalo walikuwa wanalitaka. Jambo hili lazima Romano aegeshe sikio lake kutoka kwa watu wa ndani.

Anaweza kwenda mbali zaidi na kujua ni mchezaji gani ambaye Barcelona wanafikiria kumchukua kwa ajili ya kuziba dau la De Jong. Hii ndio tofauti yake na wanahabari wengine. Amewekeza zaidi katika watu wa ndani ya klabu.

Lakini achilia mbali watu wakubwa katika klabu, Romano anaweza kuwa amewekeza katika watu wa kawaida kabisa klabuni. Katibu mukhtasi, mpiga picha wa klabu, mfagizi na wengineo. Hawa ndio wanaoshughulika na shughuli za kila siku za klabu.

Kwa mfano, mpigapicha lazima ataambiwa ajiandae kwa sababu keshokutwa Gabriel Jesus atapigwa picha akiwa na jezi ya klabu baada ya kutoka katika vipimo vya afya. Unahitaji kuwa na mpigapicha kwa ukaribu zaidi.

Katibu mukhtasi ndiye ambaye anapokea faksi zote za klabu na kuwapelekea mabosi. Analazimika kuwa na jicho la mwewe katika kila karatasi kama ameonyeshwa pesa na Romano. Huu ndio ukweli unaohusu mzunguko wa maisha ya klabu.

Wakati alipofika Arsenal mwaka 1996, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger aliwaambia wachezaji wake mastaa umuhimu wa kuwaheshimu wafanyakazi wote wa klabu bila ya kujali nafasi zao kwa sababu wanashika siri nyingi za klabu. Ni katika mambo kama haya.

Kwa Romano ni lazima awe na mzunguko huu wa watu pale Arsenal, Chelsea, Liverpool, Tottenham, Wolves, Manchester City na kwingineko. Akijumlisha habari zake kutoka kwa mzazi wa mchezaji, au mchezaji mwenyewe, wakala, mfanyakazi wa ndani wa klabu, inakuwa rahisi kwake kuja na habari ya uhakika.

Romano anaweza asiwe na uhusiano na wakala wa Raphinha, lakini anaweza kuzipata habari za Raphinha kupitia kwa watu wake wa ndani wa Leeds United au Chelsea, Barcelona na Arsenal ambazo zimekuwa zikimuwania staa huyo wa kimataifa wa Brazil.

Endapo atazikosa habari hizo kwa wakala au watu wa ndani wa klabu bado Romano ana mahali pa kuzipata habari hizo. Kesho nitakwambia ni wapi kwingine ambapo Romano anaweza kuzipata habari za ndani za uhamisho wa mchezaji kiasi cha kuja kututambia kwa uhakika kabisa kuhusu uhamisho wa staa fulani akiwa na kauli yake maarufu inayotisha sasa kuhusu uhamuisho ya ‘Here we Go.”

Columnist: Mwanaspoti