Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ewura katika hatua ya ‘kishujaa’ kudhibiti bei mpya za maji

976b747c8c558d8374fb73dc467ea5b0.png Ewura katika hatua ya ‘kishujaa’ kudhibiti bei mpya za maji

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UAMUZI wa kishujaa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati za Maji (Ewura) wa kufuta bei zote ambazo zilitakiwa kuanza kutumika Januari 2021 na kuzitaka mamlaka za maji kuendelea na bei zilizotumika 2018/19 umewafuta machozi watumiaji wa maji waliokuwa wakilalamikia ankara kubwa zisizolingana na matumizi kote nchini.

Ewura imejali kilio cha watumiaji maji nchini kote ambao katika siku za hivi karibuni, wamekuwa wakilalamika kubambikiziwa ankara za maji, hiyo kutakiwa kulipa fedha nyingi wakati huduma wanayopata haipo katika ubora.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje wakati akizungumza na vyombo vya habari anasema, hatua ya mamlaka hiyo kusitisha bei mpya za watumiaji maji, inalenga kuipa nafasi kufanya uchunguzi wa kina juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kubambikizwa ankara za maji.

Chibulunje anasema, kwa kawaida, Ewura ndiyo inayoainisha bei kwa mamlaka za maji za miaka mitatu 2018/19, 2019/20 na 2020/21 ambazo ndizo zinaendelea kutumika hadi sasa na ilitakiwa zianze kutumika bei mpya tangu Januari mwaka huu.

Uamuzi wa Ewura wa kusimamisha upandishaji wa ankara za maji na zisianze kutumika Januari mwaka huu, ni uamuzi muafaka ambao umezingatia kilio cha wapokea huduma ya maji.

Chibulunje anasema Ewura hawajakurupuka kusitisha matumizi ya bei mpya, kwani imekuwa ikipokea malalamiko ya wananchi na katika malalamiko hayo yanayohusu umeme, mafuta, gesi asilia, malalamiko ya maji yameongoza kwa kuchukua asilimia 60 ya malalamiko yote.

Licha ya malalamiko kuhusu huduma ya maji kuongoza, zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanalalamikia ankara za maji kwamba ni kubwa na hawakubaliano nazo.

“Kilio kikubwa kutoka kwa wateja wa huduma za maji kipo kwenye ankara za maji ambapo asilimia 75 ya malalamiko yote kwenye maji ni kuhusu kutokubaliana na ankara za maji zinazotolewa na mamlaka za maji mbalimbali,” anasema Chibulunje.

Chibulunje anasema kutokana na watumiaji wa maji kulalamikia mamlaka za maji na katika malalamiko hayo robo tatu yake kuwa ya ankara za maji, kumesababisha Ewura kusimamisha matumizi ya ankara mpya ili kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuhusu malalamiko hayo.

Pia watumiaji wa maji takribani asilimia 13 wamekuwa wakitoa malalamiko yanayohusu migogoro ya uunganishaji huduma za maji katika maeneo yao, kwamba hawaridhiki nazo. Kwa mamlaka inayosikiliza wapokea huduma kama Ewura ni budi kujipa muda kuchunguza kilio hicho.

Mamlaka hiyo imechukua uamuzi huo kwa kuzingatia sheria ya Ewura kifungu namba 414 na sheria ya maji ya mwaka 2019, pamoja na kanuni za upangaji bei za mwaka 2020, ambazo zimeainisha utaratibu wa marekebisho ya bei husika.

Kwanini Ewura imeamua kusitisha matumizi ya bei mpya? Ewura ndiyo hupitia hatua kuu nne wakati wa kufanya mchakato wa mabadiliko ya bei yanayowasilishwa kwake na mamlaka za maji.

Inapitia katika hatua hizo ili kuhakikisha kwamba bei zinazopandishwa nayo zinakuwa halali, za kweli, zinazokubalika, zinazojali makundi yenye kipato cha chini na zitawezesha mamlaka kutoa huduma endelevu.

Ewura ndiyo hupokea maombi ya kubadilisha bei kutoka kwa mamlaka husika za maji baada ya kupitiwa na kuidhinishwa na kuchambuliwa na wajumbe wa Bodi ya Maji ya Mamlaka husika.

Kwa mujibu wa sheria ya maji ya mwaka 2019, wajumbe wa bodi wa mamlaka za maji ni wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo madiwani, mwakilishi wa watumiaji maji wakubwa, watumiaji wadogo, mkurugenzi wa mji na wanawake.

Chibulunje anasema maombi ya mabadiliko ya bei yanapowasilishwa Ewura, baada ya kuchambuliwa na bodi za mamlaka za maji, yanapaswa kuainisha bei zinazopendekezwa, sababu za msingi za kuomba mabadiliko ya bei na manufaa ambao wateja watapata kutokana na mabadiliko hayo.

Maombi yaliyokidhi vigezo hivyo, vinaipa fursa Ewura kuanzisha taftishi ambayo pamoja na mambo mengine inajumuisha utaratibu wa kukusanya maoni ya wadau wa huduma zinazotolewa na mamlaka husika.

Taftishi hiyo inahusisha pia kutangaza bei iliyopendekezwa kwenye vyombo vya habari likiwemo gazeti la serikali, tovuti ya Ewura, magazeti na kwenye mbao za matangazo katika eneo la huduma ili kupata maoni ya wadau wa huduma za maji kuhusu bei zilizopendekezwa. Pia hupokea maoni kutoka Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) na Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazothibitishwa na (Ewura CCC) na kuyaweka pamoja.

Katika mikutano hiyo ya kutafuta taftishi, wananchi wengi wamekuwa na mawazo kwamba hicho ni kikao cha uamuzi wa kuamua kama bei ipite au isipite, jambo ambalo si kweli. Lakini ukweli ni kwamba katika mikutano hiyo, Ewura huwa inakusanya maoni ili kupata sababu ya kukataa au kukubali kupandisha bei na nini kifanyike ili kuboresha huduma.

Kwa kawaida na kisheria, uamuzi wa kupandisha bei iliyoombwa hufanywa na Bodi ya Ewura kwa kuzingatia uzito wa sababu zilizotolewa na mamlaka husika iliyotoa kwa ajili ya kuomba kubadilisha bei ya huduma zake pamoja na maoni ya wadau na wateja wa mamlaka ya maji husika, ushauri wa mabaraza ya ushauri (Ewura CC na Ewura GCC).

Pamoja na kupokea maombi ya mamlaka husika kupindisha bei ya maji, Ewura hujiridhisha kwa kufanya tathmini ya mapendekezo ya bei iliyotolewa na mamlaka husika kulingana na gharama zinazotumika katika kutoa huduma za maji ambazo ni pamoja na gharama za kila siku za uendeshaji katika uzalishaji maji, usafirishaji, usambazaji, watumishi, utawala na matengenezo.

Chibulunje anasema gharama kwa ajili ya kubadilisha miundombinu iliyochakaa, kuisha kwa muda wake au kuongeza miundombinu kwa ajili ya wateja wapya, hutegemea fedha iliyotengwa ya uchakavu.

“Gharama zote hizo lazima ziwe zimeanishwa na kuchambuliwa kwa kina katika mpango wa kibiashara wa mamlaka ya maji wa kipindi cha miaka mitatu ijayo,” anasema.

Upitishaji wa gharama unazingatia uhalali kulinganisha na gharama zilizotumika katika kipindi cha nyuma za mamlaka husika pamoja na hesabu ya fedha iliyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Chibulunje anasema, gharama zote hugawanywa kwa wateja kulingana na matumizi yao ya maji na ndipo bei za maji kwa kila daraja la mteja hupatikana.

Katika kugawanya gharama hizo, Ewura huzingazia na kulinda maslahi ya wateja, huduma kwa wasio na uwezo pamoja na uendelevu wa huduma husika. Vile vile, katika kufanya tathmini ya mapendekezo ya bei, Ewura huzingatia mlinganisho wa gharama za uendeshaji za mamlaka nyingine za maji hapa nchini zinazotoa huduma ya maji safi na majitaka katika mazinigra yanayofanana.

Aidha, pamoja na maoni ya wateja na wadau kuzingatiwa katika kufikia uamuzi wa bei inayostahili, maoni yao huzingatiwa katika kupitisha bei na pia hutumika kuainisha masharti ambayo mamlaka ya maji husika itapaswa kuyatekeleza sambamba na bei zitakazoidhinishwa.

Uamuzi wa maombi ya bei hutangazwa kupitia agizo la Ewura kwenye gazeti la serikali na katika magazeti ya kawaida. Katika agizo hilo, Ewura huainisha bayana misingi na hoja zilizozingatiwa katika kufikia uamuzi ule na sheria ambayo mamlaka ya maji husika itatakiwa kuelekeza.

Agizo, hilo huweka bayana tarehe ambayo bei zinazoidhinishwa zitaanza kutumika. Kwa mujibu wa sheria ya Ewura, mtu yeyote ambaye hakuridhika na uamuzi wa Ewura anayo haki ya kukata rufaa kwenye Baraza la Ushindani wa Haki katika Biashara.

Columnist: habarileo.co.tz