Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Emanuel Saakai, kocha wa Kitanzania Ulaya mwenye leseni ya UEFA

Saakai Pic Data Emanuel Saakai

Thu, 20 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kipindi ambacho Pep Guardiola, alianza safari yake ya ukocha akisimama kama mkuu kwenye benchi la ufundi, ilikuwa 2007 ambapo Mtanzania, Emanuel Saakai alikuwa zake Arusha akijaribu kupambana pengine anaweza kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa.

Guardiola wa Manchester City ambaye anatajwa kuwa mmoja wa makocha bora kwenye soka la kisasa, miaka michache baadae baada ya kufanya makubwa akiwa na kikosi cha wakubwa Barcelona baada ya kuthibitisha ubora wake akiwa na vijana, alitazamwa na Emanuel.

Kulingana na ugumu wa wakati huo kwenye soka la Tanzania, Emanuel aliona anaweza kuuishi mpira kwa kuendeleza vipaji vya wengine.

Milango ya neema ilifunguka taratibu na hatimaye ana leseni B ya UEFA ambayo ametunukiwa Ujerumani huku akijichotea uzoefu kwa kufanya kazi kwenye akademi ya miamba ya soka nchini humo, Borussia Dortmund.

Nje ya Bongo, imefanya mahojiano ya kina na Mtanzania huyo ambaye anaishi Australia na hapa anafunguka mambo mengine kibao ikiwemo safari yake ya ukocha hadi kupata shavu la kwenda kusoma Ujeruman kwa Frank-Walter Steinmeier.

SAFARI KWENYE SOKA

Emanuel anajieleza kwa kusema, "Mimi ni mzaliwa wa Ngorongoro (Mmasai) lakini nimekulia Ngaramtoni, Arusha. Safari yangu ya kwenye Soka ilianzia kwanzia nilipokua na miaka miwili/mitatu,"

"Nilianza kwa kucheza mpira wa makaratasi na rafiki zangu mtaani kwetu alafu baadae shuleni kwenye timu za shule. Nilianza kucheza kwenye ligi za vijana mkoani Arusha alafu baadae ni kaamia Zanzibar nikipokua na miaka 15.

"Hapo ndipo nilipocheza kwa miaka mi 3/4. Nikarudi Arusha tena kuendelea na kucheza mpaka nikapata majereha makubwa na kushindwa kuendelea kucheza. Ndipo nilpoamua kufundisha timu ya New Vision FC kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 2012, nikaamua kuanzisha Academy yangu, Lengo Football Academy (Lengo)," anasema.

Hakuishia hapo anaendeleza kueleza kwa kusema, "Nia na madhumuni ya kuanzisha Lengo ilikua ni kukuza vipaji na kusaidia vijana na jamii isiojiweza nchini kupitia mchezo wa mpira.

"Hapo ndipo nikaanza kuwasiliana na vyama vya Mpira Duniani kwajili ya kujaribu kupata msaada wa kwenda kujiendeleza kielimu kusomea masuala ya Ukocha. Chama cha Mpira cha Australia FFA ndipo wakanialika kupitia ufadhili na kwenda kusoma ngazi ya kwanza (grassroots level).

" Hii ilikua ni 2012 mwishoni. Wakanialika tena mwaka 2014 kwajili ya kuchukua ngazi za Certificates ya kufundisha timu za vijana pamoja na naza wakubwa (seniors men’s) alafu baadae nikaalikwa tena kwajili ya kufanya C Licence mnamo Mwaka 2015 na kukamilisha 2016. Kwenye safari yangu ya tatu ndipo nikakutana na Mke wangu huko! Kila safari nilikua niki kaa kwa wiki tatu mpaka miezi miwili, anasema

UZOEFU WAKE

Mmiliki huyo wa leseni B ya UEFA ‘B’ ambaye alihitimu kupitia DFB nchini Ujerumani anasema, "Alifundisha na kufanya kazi na nyota wa kandanda wa kimataifa ikiwa ni pamoja na Harry Kewell, Akademi za FC Barcelona na Juventus FC kama mwakilishu wao Australia,"

"Upande wa A-League ambayo ni Ligi Kuu ya Australia nimefanya kazi na Central Coast Mariners, pamoja na wababe wa Bundesliga Borussia Dortmund FC. Nimekuwa kocha Mkuu wa timu za vijana za South Melbourne FC na Green Gully SC (Australia).

"Lakini pia nimekuwa nikiwafunza na kuwashauri vijana wanaotaka kulipwa kwa upande wa Ligi A (Ligi Kuu), Central Coast Mariners FC. Nimehudhuria au kufaulu katika kozi za mafunzo ya ukocha na semina zinazotolewa na FC Barcelona, ​​Manchester City, Cardiff City, Ajax, Juventus, FA ya Italia, FA ya Ubelgiji na FA ya Ujerumani," anasema Mtanzania huyo.

WACHEZAJI ALIOWATOA

"Dor Jok, anacheza katika timu ya Ligi Kuu ya Australia ya Central Coast Mariners FC, Muginga Mpota, chipukizi wa Kitanzania aliyesajiliwa hivi karibuni katika klabu ya Daraja la 2 akiwa na umri wa miaka 17 pekee. Atakuwa mtaji mkubwa kwa Taifa Stars siku zijazo.

"Amanhom Khamis, alisajiliwa na klabu ya Ligi Kuu ya Australia kwneye timu zao za vijana na mwingine ni Esrom Paulos, yuko katika harakati za kusaini klabu ya kulipwa ambayo siwezi kuitaja kwa sasa” anasema kocha huyo.

CHANGAMOTO ALIZOKUMBANA NAZO

Emanuel anasema miongoni mwa changamoto kubwa ambazo amekumbana nazo kwenye safari yake ya soka ni pamoja na kupata nafasi ya kujiendeleza.

"Kubwa kabisa ni kupata nafasi kwenye kukubalika kujiunga na Kozi hizi za UEFA. Pili, kupata kazi za Ukocha kwenye ngazi za juu nikiwa Muafrika nisiokua na jina kama mchezaji wa kulipwa,"

"Namshukuru Mungu sana kwani kutokana na kujituma kwangu na uwezo na kipaji cha kufundisha mpira Mungu alionibariki naweza kuendelea kujituma na kuwashawishi (kwa vitendo) hawa watu waliokua kwenye nafasi za kutoa fursa waweze kunifikiria na kunipa nafasi,"

"Ila sio rahisi kabisa, kwangu mimi kukubalika duniani, inabidi nifanye kazi mara Millioni moja zaidi ili niweze kupewa fursa. Lazima niwe bora kwa muda mrefu ili tu niweze kufikiriwa na pamoja na kuwazidi washindani wenzangu," anasema Emanuel

LESENI B YA UEFA

Leseni ya UEFA B ni kiwango kimoja chini ya Leseni ya UEFA A, na inaruhusu wamiliki kuwa makocha wakuu wa timu za vijana kwneye vilabu vya kulipwa, au wasaidizi (assistant senior team coaches) kwenye klabu za kulipwa.

MAONI YAKE KUHUSU STARS

Kwa faida ya Tanzania kuhakikisha inafanya vizuri kwenye ngazi za juu za soka, Emanuel ameyataja mambo 6, "Elimu bora kwa Makocha kuanzia kwenye ngazi ya chini na kuuwapa fursa (ajira) hawa makocha kwajili ya kuwaendeleza wachezaji wetu Tanzania.

"Ligi za vijana zitakazo chezwa nchi nzima kuwapa wachezaji angalau wawe na uwezo wa kucheza mechi 30 za kiushindanj hii ni ngazi zote chini ya miaka 12 hadi 23. Miundombinu (infrastructure), yaani viwanja vizuri na salama vya kuchezea.

"Vituo vya kukuza na kulea vipaji kwenye kila Wilaya na Mikoa kwajili ya kuendeleza vipija nchi nzima. Elimu na huduma ya Sayansi michezoni kwajili ya kujikinga na majeraha kwa wachezaji kupitia mazoezi maalumu,"

"Uundaji wa njia ambazo vijana watapita hadi kuwa wachezaji wkimataifa ndani na hata kimataifa. Hapa TFF inatakiwa kuwa na ushiriano mkubwa na klabu hili kufanikisha," anasema.

WASIKIE HAWA

Magwiji wa soka ambao wamefanya kazi na Emanuel haya waliwahi kusema kumhusu.

Harry Kewell, nguli wa zamani wa Liverpool FC na Australia na Harry Kewell Academy "Ninapenda mapenzi ya Emanuel kwa mchezo. Analeta kitu tofauti kwa timu yangu ya kufundisha."

Eric Abrams, mbunifu wa Kizazi cha Dhahabu cha Ubelgiji, na Mkurugenzi wa zamani wa Ufundi “Inafurahisha kuona Emanuel, kama Mwafrika, akiingia kwenye soka licha ya vizuizi vyote kwenye safari yake. Wale kama yeye waliojitolea na wanaovumilia wataendelea.”

Takis Fyssas, gwiji wa soka wa Ugiriki na mshindi wa Ubingwa wa Ulaya “Emanuel amejaa shauku, nguvu na kujitolea kwa kazi yake katika soka.”

Ian Greener, mwanasoka wa zamani wa Ligi Kuu England na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya vijana “Mtu huyu anajua kila kitu kuhusu soka.”

Columnist: Mwanaspoti