Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Elimu ya juu inavyoimarishwa kupitia TCU

Cf7eafba6e9d2e34b6dc094b9248a73c Elimu ya juu inavyoimarishwa kupitia TCU

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“ NAOMBA niahidi kwamba Tume itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania katika Sekta hii ya elimu ya juu ili kuhakikisha Watanzania katika ngazi zote wanapata elimu bora yenye kukidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda na kimataifa.”

“Tume ina jukumu la kuhakikisha kuwa rasilimali watu inayozalishwa na vyuo vikuu nchini inakuwa na watu wenye weledi na ujuzi stahiki kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda nchini na kuhakikisha kuwa nchi yetu inasonga mbele kiuchumi na kimaendeleo kwa jumla, ambalo ndiyo dhamira kuu ya serikali na lengo la msingi la maendeleo ya nchi yetu.”

Ndivyo anavyosema Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Mayunga Nkunya katika ufunguzi wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika Agosti 31, 2020 hadi Septemba 5, 2020 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam yakiwa na kaulimbiu:

‘Nafasi ya Elimu ya Juu katika Kuleta Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo Endelevu.’ Maonesho ya mwaka huu yamezishirikisha taasisi 67.

Katika maonesho haya, wananchi na wadau mbalimbali wa elimu ya juu hupata fursa ya kuonana moja kwa moja na kubadilishana mawazo na taasisi husika, kuomba udahili na huduma nyingine moja kwa moja katika vyuo, pamoja na taasisi na vyuo kujitangaza na kueleza namna zinavyotoa huduma na kadhalika.

Vijana mbalimbali waliotuma maombi ya udahili katika maonesho hayo, wanaomba yazidi kuboreshwa ili waombaji katika maonesho wawe wanapata papohapo uhakika wa maombi yao kukubaliwa au kukataliwa katika programu na vyuo husika.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, hadi asubuhi siku ya kufunga, zaidi ya vijana 33,969 waliohudhuria maonesho, walikuwa wameomba moja kwa moja viwanjani hapo, kudahiliwa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwa masomo ya shahada ya kwanza katika mwaka wa masomo 2020/2021.

Kihampa anasema: “Idadi ya wananchi wanaotembelea maonesho haya imeendelea kuongezeka hasa kutokana na baadhi ya vyuo vya elimu ya juu kuanza kutoa huduma mbalimbali za ushauri wakati wa maonesho, ikiwemo kufanya udahili wa wanafunzi.”

Katika maonesho hayo, Mwenyekiti wa TCU, Profesa Nkunya, anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa mafanikio makubwa ya TCU yaliyopatikana kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi hiki cha miaka mitano inayomalizika sasa.

Anasema miongoni mwa mafanikio hayo ni kuimarika kwa usimamizi wa mifumo ya uthibiti ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini ili kukidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa, vyuo vikuu nchini vinakidhi idadi ya kutosha ya wahadhiri na viongozi waandamizi wenye sifa stahiki; programu za masomo zinazofundishwa vyuoni zimeidhinishwa na mamlaka husika vyuoni na TCU na pia, kuhakikisha kunakuwa na uwiano unaokubalika baina ya wahadhiri na idadi ya wanafunzi waliopo vyuoni katika kila programu,” anasema.

TCU inasema imeshatoa mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa makamu wakuu wa vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 44 kati ya 47 vya umma na binafsi mintarafu usimamizi wa mafunzo, uanzishaji mitaala inayoendana na mahitaji na jinsi ya kuanzisha ushirikiano na waajiri mbalimbali zikiwamo asasi za umma na binafsi vikiwemo viwanda.

Imebainika kuwa, TCU imetengeneza mfumo wa kuratibu udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu uliounganishwa moja kwa moja na mifumo ya udahili ya vyuo vya elimu ya juu nchini. Taarifa ya Tume hiyo inasema: “Mfumo huu pia umeunganishwa na kanzidata za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar (ZHELB).” Inaongeza:

“Mfumo umerahisisha upatikanaji wa taarifa za udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu na kuiwezesha TCU kuhakiki sifa za wanafunzi wanaodahiliwa na vyuo vya elimu ya juu nchi nzima kwa uhakika na ufanisi zaidi.” Profesa Nkunya anasema:

“Mfumo huu umeongeza uhuru kwa waombaji kuchagua vyuo na programu wanazozipenda, na kutoa mamlaka kamili kwa vyuo vikuu kushiriki moja kwa moja katika udahili wa wanafunzi kupitia mabaraza ya seneti yao kama yalivyo matakwa ya sheria.” Anaongeza:

“Pia imetengeneza mfumo wa kielektroniki wa kuhifadhi takwimu na taarifa za vyuo vikuu kuhusu, usajili wa vyuo, idadi na sifa za kitaaluma za wahadhiri, wanafunzi, na rasilimaliwatu kwa jumla.

Ili kuimarisha mfumo wa utoaji wa ithibati ya mitaala, TCU imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali yanayolenga kuboresha elimu ya vyuo vikuu nchini.

Anasema Tume imeendelea kuvishauri vyuo vikuu kuandaa mitaala inayoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, mahitaji ya wataalam katika soko la kitaifa, kikanda na kimataifa pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwamo mapinduzi ya nne ya viwanda.

Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, baadhi ya vyuo vikuu vimeshatengeneza na kuanza kufundisha mitaala ya aina hiyo ambavyo ni pamoja na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi (CUHAS).

Imebainika kuwa, njia nyingine inayotumiwa na TCU kufikisha elimu kwa walengwa ni pamoja na kutembelea wahitimu wa kidato cha sita waliopo kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kufanya mikutano na wahitimu wa kidato cha sita nchi nzima.

“Hadi sasa (mwaka 2020), wafanyakazi wa Tume wamekwishatembelea kambi 17 za JKT na kuwafikia wahitimu wote wa kidato cha sita waliopo katika kambi hizo kwa mujibu wa sheria,” anasema Profesa Nkunya. Anaongeza:

“Takribani wanafunzi 1,800 kutoka Zanzibar wamenufaika na programu ya elimu kwa umma iliyofanyika katika Wiki ya Maonesho ya Elimu ya Juu Zanzibar yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka Julai 27 hadi 30, 2020 katika viwanja vya Mapinduzi Kisonge, Zanzibar.”

Katika maonesho hayo, Profesa Kihampa, anazungumzia usajili wa kampuni za wakala wa vyuo vikuu vya nchi za nje akisema: “Kwa mara ya kwanza Tume imesajili kampuni 14 zinazohusika na udahili wa wanafunzi kwa vyuo vikuu vya nje ya nchi walikidhi vigezo vya usajili kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.” Anasisitiza:

“Lengo la usajili ni kuwalinda Watanzania wanaokwenda kusoma nje ya nchi dhidi ya mawakala wasio waadilifu na kupelekwa kusoma katika vyuo na programu za masomo zisizotambuliwa na mamlaka halali za nchi husika.”

Akizungumza katika siku ya ufungaji wa maonesho kwa niaba ya vyuo vikuu na taasisi zilizoshiriki maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel, anahimiza waombaji wa masomo katika vyuo vikuu vya nje ya nchi kuzingatiana kutumia kampuni wakala zilizosajiliwa na TCU ili wasiangukie katika mikono ya matapeli.

Anaishauri serikali kupitia TCU na mamlaka nyingine, kuzingatia weledi, ujuzi na uzoefu katika kuajiri wahadhiri wa vyuo na taasisi za elimu ya juu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo kipaumbele kinatolewa zaidi kwa kuzingatia alama za ufaulu katika vyeti.

“Mtu anaweza kuwa na GPA ya 4.5, lakini utoaji wake wa ‘material’ (ufundishaji) ukawa wa kiwango cha chini kabisa… Huko hospitali kuna madaktari wengi wenye ‘competence’ (weledi), lakini kwa kuwa hawakufikia GPA fulani, hawapati nafasi ya kuwafundisha vijana huko katika vyuo vya elimu ya juu,” anasema Mollel.

Akifungua maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo anaipongeza TCU kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya kuboresha elimu ya juu nchini.

Anasema: “Endeleeni kusimamia kwa dhati ubora wa elimu ya juu nchini ili kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa ya kikanda na kimataifa ili kuleta maendeleo ya wahitimu binafsi, pamoja na nchi yetu kwa jumla.”

Anasema serikali imeimarisha ufundishaji katika vyuo vikuu na kufadhili masomo ya wahadhiri 714. Kati ya hao, 191 ni wa shahada ya umahiri na 523 ni wa shahada ya uzamivu.

“Maboresho yaliyofanywa na Serikali katika elimu ya juu, yamewezesha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kutoka 65,064 mwaka 2015 hadi 87,813 mwaka 2020,” anasema.

Anaongeza: “Ongezeko hili limechangiwa na Serikali kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 125,126 mwaka 2015 hadi kufikia wanafunzi 132,119 mwaka 2020… Fedha za mikopo zimeongezeka kutoka Sh bilioni 341 mwaka 2014/15 hadi kufikia Sh bilioni 450 mwaka 2019/20.”

Anasema kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kutegemeza maendeleo ya nchi kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuwa na maendeleo endelevu yaliyojikita katika uzalishaji wenye tija, mwaka 2015/16 hadi Juni, 2020, imesimamia azma hiyo na kutoa mafunzo na kuanzisha vituo vya ubunifu katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

Hii ni pamoja na kuanzishwa kwa kumbi za ubunifu (Innovation Hubs) na vituo atamizi (incubators) katika vyuo vikuu; ikiwa ni pamoja na: UDSM Innovation Hub; SUA Innovation Hub; Bio-Innovation Hub (Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela); UDOM - Innovation Space; MUST Innovation Hub; na Zanzibar Technology and Business Incubator (Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia).

Anasema Serikali imeanzisha vituo atamizi 17 ili kukuza na kuendeleza ubunifu ambavyo vimewezesha kuanzishwa kwa kampuni 94 zinazotokana na bunifu hizo na kuwezesha kuibuliwa na kutambuliwa kwa wabunifu wachanga 415 kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu).

Kati yao, wabunifu 60 mahiri wanaendelezwa ili kufanya bunifu zao kufikia hatua ya kubiasharishwa ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Haya ni baadhi ya mafanikio tuliyoyapata katika sekta ya elimu. Haya ni mafaniko yetu sote ambapo nalazimika kuyasema ili wananchi wayasikie na kujivunia; na pia watambue namna Serikali yao ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Magufuli ilivyopania kuboresha elimu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu,” anasema Dk Akwilapo.

Columnist: habarileo.co.tz