Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

EMILIANO: Mtoto wa maskini aliyeibuka shujaa wa Argentina Qatar

Emili Pic EMILIANO: Mtoto wa maskini aliyeibuka shujaa wa Argentina Qatar

Sat, 17 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mchezo kati ya timu ya taifa ya Argentina na Uholanzi unamalizika, kulikuwa na kundi kubwa la wachezaji waliokuwa wameenda kumfuata Lautaro Martinez baada ya kufunga penalti ya mwisho.

Wakati mastaa hao wanaenda kumpongeza mfungaji wa penalti ya mwisho, kapteni Lionel Messi yeye alienda upande tofauti na wachezaji wengine wote, alienda upande ambao alikuwapo kipa wao, Emiliano Martinez. Alipofika akamkumbatia pale chini alipokuwapo na kumpongeza akiamini yeye ndiye aliyesababisha Argentina kuvuka katika hatua hiyo.

Video iliyonasa tukio hilo, imekuwa ni moja kati ya vipande vya video vilivyopendwa zaidi na mashabiki wa soka duniani kwa sababu ya heshima ambayo Messi alionyesha kwa kipa huyo.

Kama ulimsoma ama kumsikia alichokisema kiungo wa Real Madrid, Toni Kroos hivi karibuni akizungumzia mitazamo wa wengi katika soka, alikosoa suala la watu na hata watoa tuzo kuwaangalia zaidi wafungaji tu wakati kuna wachezaji wengi sana wanahusika kabla ya mpira kumfikia mfungaji, akisema hata aliyeanzisha tuzo za mchezaji mmoja mmoja katika soka ambalo ni mchezo wa timu, alifanya makosa makubwa.

Na hakika walichofanya wachezaji wa Argentina kwenda kumpongeza mfungaji wa penalti ya mwisho, Lautaro Martinez, ni katika mwendelezo wa mitazamo ile ile ya wadau wa soka aliyoikosoa Kroos. Na ndio sababu video ile ya Messi kwenda kumpongeza kipa Emiliano Martinez iligusa hisia za wengi walioingalia.

Katika moja ya kauli zake, Martinez aliwahi kusema atapambana kwa jasho lake lote kuhakikisha Lionel Messi anatwaa mataji ya kimataifa na alifanya hivyo alipoibuka shujaa akiiwezesha nchi hiyo kushinda Kombe la Copa Amerika 2021 na katika fainali za sasa za Kombe la Dunia huko Qatar ameokoa penalti kadhaa na hatari nyingi na kuliwezesha taifa lake kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Dunia ambayo watakutana na Ufaransa keshokutwa Jumapili.

EMILIANO NI NANI

Pengine watu wengi hawamfahamu vyema ni nani huyu Emiliano Martinez ambaye enzi za utoto wake alipewa jina la utani la Martinho na ndio jina lililodumu hadi leo.

Martinez alizaliwa Septemba 2, 1992 huko Mar del Plata nchini Argentina, jina lake kamili ni Damian Emiliano Martinez Romero, lakini kwa kifupi ndio wanamwita Emiliano Martinez.

Baba yake anaitwa Alberto na mama yake anaitwa Susana, alilelewa na kukulia katika kitongoji hicho akiwa na kaka yake Alejandro.

Moja kati ya kumbukumbu mbaya ambayo staa huyu anayo kwenye maisha yake ya utotoni ni kushuhudia baba yake akilia mara kwa mara usiku wa manane kwa sababu hakuwa na pesa ya kulipia kodi ya nyumba na mahitaji mengine.

Kwa mujibu wa tovuti ya Lifebogger ni kwamba hadi chakula ndani ya familia ya staa huyu kilikuwa kinapatikana kwa manati, hiyo ilitokana hali ya umaskini iliyokuwa inawakabili kwa wakati huo.

KUJIKWAMUA KIMAISHA

Kutokana na maisha magumu, Martinez aliamini njia pekee ya kujikwamua ni yeye kucheza soka, alipambana na akafanikiwa kufanya majaribio kwenye timu ya CA Independiente ya huko Argentina na akachaguliwa kujiunga na akademi ya timu hiyo.

Alicheza kwenye timu hiyo hadi akatimiza umri wa miaka 16, wakati huo akabahatika kuitwa kwenye timu ya taifa ya Argentina kwa vijana umri chini ya miaka 17.

Hiyo ikawa ndio njia yake ya kutoka kwani maskauti wa Arsenal ya Ligi Kuu ya England walimuona kwenye moja ya mechi akiwa na taifa hilo na ikapelekwa ripoti kwa mabosi wa timu hiyo.

Kidogo ilikuwa ngumu kuondoka Independiete, kwa sababu timu hiyo ilihitaji kiasi kikubwa cha pesa, ikabidi mazungumzo yachukue muda mrefu hadi kufikia Julai 10, 2010 ambapo Arsenal ilikubali kutoa Pauni 1.1 milioni kumnunua staa huyo.

Rasmi akahama kutoka Argentina na kuanza kuishi London, England huku wakati huo hakukuwa hata na mtu aliyemfahamu kwani familia yake yote ilibakia nchini Argentina.

“Ilikuwa ngumu sana, lugha, utamaduni na vyakula vilikuwa tofauti, kuna muda mtu anakuongelesha kana kwamba umeishi England kwa miaka 10, kumbe ndio kwanza umefika, sikuwa nafahamu Kiingereza, hiyo ilikuwa changamoto kubwa na ilinichukua muda mrefu hadi kufikia hatua ya kuzoea mazingira,” alisema Martinez kwenye moja ya mahojiano yake akielezea nyakati zake za kwanza nchini England.

Akiwa hapo alicheza timu za vijana na hakuchukua muda mrefu alitolewa kwa mkopo kwenda Oxford United ambako alipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza na baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika alirudi Arsenal na akacheza mechi yake ya kwanza akiwa na kikosi cha kwanza dhidi ya Coventry City kwenye Kombe la Carabao.

Baada ya hapo akawa anahudumu kama golikipa wa akiba na mwishowe akaanza kutolewa kwa mkopo kwenye timu mbalimbali ikiwa pamoja na Wolves, Getafe, Sheffield Wendseday, Reading, Rotherham na mwisho akauzwa kwa Euro 17 milioni kwenda Aston Villa mwaka 2020 ambapo anacheza hadi sasa.

Mambo makubwa aliyoyafanya katika siku za mwisho Arsenal yalimpa nafasi ya kuitwa timu ya taifa ya Argentina na amekuwa kipenzi cha benchi la ufundi kutokana na ubora wake.

Baada ya aliyekuwa kipa Na.1 wa Arsenal, Bernd Leno, kuumia kuelekea mwishoni wa msimu wa 2019-20, Martinez akawa kipa Na.1 pale Emirates Stadium na akacheza kwa kiwango cha juu sana akiisaidia Gunners kushinda Kombe la FA Agosti 2020. Katika nusu fainali, Arsenal iliifunga Manchester City ya Pep Guardiola mabao 2-0 na katika fainali ikaifunga Chelsea 2-1, mabao yote manne ya hatua hizo mbili yakifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang na golini alisimama mwamba huyu, Martinez.

Martinez akacheza pia dhidi ya Liverpool katika mechi ya Ngao ya Jamii Agosti na kuisaidia Arsenal kutwaa taji hilo, likiwa ni taji lao la pili kubeba kwenye Uwanja wa Wembley ndani ya muda wa mwezi mmoja.

Baadaye, Septemba 16, 2020 Martinez akajiunga na Aston Villa ambako anakiwasha hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya England.

Baada ya msoto wa muda mrefu kwa sasa ameikomboa familia yake kutoka kwenye janga la umaskini na kwa wiki anakunja jumla ya Pauni 44,000 akiwa na Villa ambazo ni zaidi ya Sh125 milioni za Kitanzania.

TAKWIMU KWENYE KOMBE LA DUNIA 2022

Ameokoa jumla ya michomo mitano, amecheza mechi tatu bila ya kuruhusu bao ambazo ni dhidi ya Mexico na Poland kwenye hatua ya makundi, kisha dhidi Croatia kwenye nusu fainali. Pia ameokoa penalti mbili kwenye michuano hii. Amecheza mechi sita za michuano hii na amecheza dakika zote.   NJE YA SOKA

Jamaa amemuoa mrembo Mandinha Martinez mwaka 2016 na hadi sasa amebahatika kupata watoto wawili Santi Emiliano Martinez aliyezliwa mwaka 2018 na mwingine amezaliwa mwaka 2020.

Columnist: Mwanaspoti