Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dwamena amenikumbusha marehemu Ibrahim Jeba

Raphael Dwamena Mchezaji wa kimataifa kutoka Ghana Raphael Dwamena (28) amefariki Uwanjani

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Stori mbili za kweli za kusikitisha sana. Majuzi amefariki nyota wa Ghana, Raphael Dwamena. Ameanguka uwanjani na kufa papo hapo wakati akiichezea klabu yake ya Egnatia dhidi ya Partizani katika pambano la Ligi Kuu ya Albania.

Kabla ya kifo chake Dwamena alikuwa amekatazwa na madaktari asicheze soka kutokana na kugundulika alikuwa na tatizo la moyo. Hata hivyo, aliamua kubisha. Alishaanguka uwanjani wakati anachezea Levante ya Hispania. Klabu hiyo baadaye iliamua kuachana naye licha ya kwamba alikuwa mtambo wa mabao.

Kuna wakati aliwahi kutakiwa na Brighton and Hove Albion ya England lakini dili hilo lilikwama kwa sababu alifeli vipimo vya afya kwa sababu hii hii ya kuumwa moyo. Hakukata tamaa akaamua kuendelea na safari yake ya soka.

Aliwahi kwenda Austria kuendelea kucheza soka lakini akaanguka uwanjani katika pambano la Kombe la Austria kati ya timu yake ya Blau-Weiss Leinz dhidi ya Hartberg. Hata hivyo, madaktari walifanikiwa kumnusuru na akasimama.

Imenikumbusha kifo cha rafiki yangu, Ibrahim Rajab ‘Jeba’. Staa wetu wa zamani ambaye kifo kilimkuta akiwa na hadhi ya mwanasoka ambaye alikuwa akipigania maisha yake kupitia mchezo huu. Alikuwa amerudi kwao Zanzibar baada ya kucheza bara.

Huku Bara Jeba alicheza Simba B, akaenda zake Azam ambapo aligundulika kuwa na tatizo la moyo. Azam walimpeleka India kutibiwa lakini madaktari wakaamuru kwamba Jeba asiendelee kucheza soka. Akabisha.

Aliporudi alienda zake Mtibwa akaendelea kucheza soka huku Azam na Simba wakishangaa. Nawaelewa Mtibwa ingawa walikuwa wanahatarisha maisha ya Jeba. Ni kama ninavyojaribu kuielewa hii timu ya Albania.

Kuna wakati unamuona mchezaji na unakiona kitu tofauti katika miguu yake. Kitu ambacho haukioni kwa wachezaji wengi. Ndivyo Jeba alivyokuwa. Kama asingekuwa na tatizo lolote basi Jeba alikuwa mmoja kati ya viungo bora ambao Tanzania imewahi kuwatoa.

Hivi hivi akiwa mgonjwa na Mtibwa yake alikuwa msumbufu katika eneo la kiungo. Uwezo wake wa kumiliki mpira. Uwezo wake wa kupiga pasi kwa ufasaha. Uwezo wake wa kutazama mbali zaidi kuliko wachezaji wenzake. Jeba alikuwa ananivutia.

Alikuwa pia anazivutia timu kubwa lakini zote zilifahamu tatizo lake na zilijua kwamba Mtibwa walikuwa wanatembelea mstari mwembamba wa mauti yake. Hatimaye alifariki akiwa kwao Zanzibar baada ya tatizo kuwa kubwa.

Kesi ya Jeba na Dwamena zinatofautiana kidogo tu. Kuna nyakati ambazo naambiwa Jeba alikuwa anabisha haumwi. Aliamini kwamba alikuwa amerogwa. Zipo nyakati ambazo alikwenda katika kisomo au katika mambo mengine ya kidunia kujaribu kubishana na madaktari wa India. Hata hivyo, mwishowe ukweli ulithibitika.

Kwa upande wa Dwamena nadhani alielewa ukubwa wa tatizo lake. Aliamua tu kufanya makusudi huku klabu yake ya Albania nayo ikijigeuza kuwa Mtibwa Sugar. Ilitaka kutumia kipaji chake mpaka pale ambapo atakomea. Na kweli walitumia kipaji chake cha ufungaji mabao mpaka pale alipofia uwanjani mapema wiki hii.

Hapa kuna mambo mawili yenye mfanano. Unajua utamu wa kucheza soka? Unajua namna ambavyo unajua kuweza kutengeneza pesa kwa kutumia kipaji chako halafu anatokea mtu anakwambia hauwezi kucheza tena na inabidi usimame kucheza soka?

Hili jambo ndilo ambalo inawezekana liliwatokea Dwamena na Jeba. Walikuwa wanafanya kazi wanayoipenda kwa ufasaha. Zaidi ni kwamba walikuwa wanalipwa vizuri au wanategemea walipwe vizuri zaidi siku za usoni. Na unaweza kukuta hakuna kitu kingine unachoweza kufanya zaidi ya hii kazi unayoifanya. Hapa ndipo tamaa inapokwenda mbele ya umauti.

Labda wangesikiliza tungeweza kuwa nao mpaka leo lakini ukweli inaikuwa ngumu kwa wakati huo kumuelewesha mtu avue viatu vyake na aache kucheza soka. Wakati huo huo kila akitazama mechi za soka anawaona wachezaji wengi wa kawaida ambao wanalipwa vizuri angali yeye amekaa katika kochi. Inaudhi.

Rafiki yetu kutoka Zambia, Enock Mwepu naye alikatishiwa utamu wake wa kucheza soka akiwa na Brighton baada ya madaktari kugundua kwamba ana tatizo la moyo. Uzuri ni kwamba yeye aliamua kustaafu na sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Brighton.

Hakuna kitu kinachouma kama kuitwa ‘mchezaji wa zamani’ wakati una umri wa miaka 25 tu. Afadhali ya Kun Aguero ambaye alikuja kugundulika ana tatizo la moyo wakati ameshavuna utajiri mkubwa huku akiwa ameshatuonyesha ubora wake ujanani.

Safari fupi za maisha ya Dwamena na Jeba zinatuonyesha namna ambavyo wachezaji wetu kutoka Afrika huwa wanashindwa kukubaliana na madaktari kwa sababu tofauti. Kubwa zaidi inakuwa njaa.

Achilia mbali moyo tuna wachezaji wengi ambao wanaficha majeraha kwa sababu ya kuhakikisha wanapata mkataba na klabu Fulani. Kuna wachezaji wengi ambao wanacheza wakiwa na majeraha kwa ajili ya kuonyesha uhodari wao kwa dakika kadhaa ili wapate nafasi ya kusaini mikataba mipya.

Nawashauri wachezaji wengi wa Afrika, hasa hawa Watanzania wazingatie afya zao. Ukweli unabakia wazi kwamba afya zao ni muhimu kuliko mchezo wa soka. Maisha ni muhimu kuliko mchezo wa soka. Na kwa upande wa klabu ni hivi hivi.

Kwa klabu nazo zijali afya za wachezaji. Wakati mwingine klabu zinakuwa na haraka ya kusaini mchezaji bila ya kujali afya yake. Wachezaji wengi wa hizi klabu zetu kubwa huwa wanasajiliwa kwanza kisha ndio tunaambiwa wanapimwa afya zao. Nina uhakika Aziz Ki alisainiwa nje ya nchi kabla ya kupimwa afya yake.

Lakini hapo hapo tuliwahi kunong’onezwa mahali kwamba Gael Bigirimana pia aliwahi kukumbwa na tatizo la moyo. Lakini tuna uhakika kwamba wachezaji wote wa Ligi Kuu wakipimwa kwa uhakika hakuna ambaye atakuwa na tatizo kubwa la moyo? Sidhani. Kwanza wenye ubavu wa kupima afya za wachezaji ni klabu chache tu.

Columnist: Mwanaspoti