Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dube! Mbabe wa Simba, Yanga afichua siri ya kofia yake

Dube Kofia.jpeg Prince Dube

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sekunde ya 13 tu tangu refa apulize filimbi ya kuanzisha mechi, mpira umekaa kwenye kamba. Ni moja ya mabao ya mapema zaidi katika Ligi Kuu Bara msimu huu na lililochangia kuongeza presha kwa timu ya Simba ambayo inaifukuzia Yanga katika mbio za ubingwa. Ni bao jingine kali kutoka kwa muuji mwenye tabasamu Prince Dube wakati Azam ilipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Wekundu wa Msimbazi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi.

Dube huyu ndiye yule yule aliyeifunga Simba bao kali la shuti la mbali kutokea pembeni kushoto mwa uwanja na kuwazamisha Wekundu wa Msimbazi kwa bao 1-0 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza msimu huu kwenye uwanja huo huo Oktoba 27 mwaka jana.

Na ndiye Dube yule yule aliyewalaza mapema Yanga msimu uliopita kwa bao 1-0 akipiga shuti la mbali na kumtungua kipa Faruk Shikhalo katika mechi iliyokuwa ya mwisho Yanga kupoteza kabla ya Wanajangwani kucheza mechi 49 mfululizo za Ligi Kuu bila ya kichapo hadi rekodi yao ilipoharibiwa na Ihefu walipopigwa 2-1 kule Ubaruku Januari 16, 2023.

SIRI YA KOFIA

Uwanjani anatisha, lakini nje ya uwanja sio muongeaji sana. Sura yake muda mwingi imejaa tabasamu, ni mwenye aibu kiasi kwamba huwezi kumkuta nje ya uwanja bila kofia inayomsaidia kujisitiri na macho ya watu wanaomzunguka kwa wakati huo. Huyu ndiye straika fundi wa mpira wa Azam FC, Prince Dube aliyeishangaza Mwanaspoti wakati wa mahojiano alipoombwa aitoe kofia yake aliyoivaa alikataa na kutoa sababu zake.

Dube alianza kwa kusema: “Naomba mnisamehe siwezi kuitoa kofia hii, nisitafsiriwe kama mtu mwenye kiburi, nina aibu sana kofia ni kama sapoti yangu huwa naivua wakati wa kuingia uwanjani na kulala tu.” Anaongeza: “Ndio maana muda mwingi nikikaa jukwaani huwezi kunikuta kichwa wazi, kingine kinachonipa ujasiri nakuwa bize na simu, nakuwa nacheza gemu ili mradi tu nisipate muda mwingi wa kujieleza mbele ya watu.”

Anaulizwa unafanya kazi inayotazamwa na watu wengi unawakwepaje? Anajibu: “Ndio maana nikitoka uwanjani jambo la kwanza napanda basi la timu moja kwa moja na sipendelei sana mitandao zaidi ya kufanya sana mazoezi binafsi na kucheza gemu, naona ndivyo vinavyonipa faraja kubwa. Katika mahojiano hayo, Dube amefunguka mambo mengi ikiwemo namna alivyotaka kuvunja rekodi ya Kipre Tcheche ambaye aliacha rekodi ya mabao 17 msimu wa 2012/13 ambayo hakuna mshambuliaji wa kigeni aliyefikia idadi hiyo.

AZITULIZA SIMBA, YANGA

“Simba na Yanga ni timu kubwa kwa Tanzania hili limethibitishwa hadi kwa vingozi wa timu yetu. Kunakuwa na utofauti mkubwa tukiwa tunafanya maandalizi ya kuzikabili timu hizo tofauti na tukiwa tunatarajia kucheza dhidi ya timu nyingine hivyo mimi kupata nafasi ya kuzifunga nimeweka rekodi; “Kuifunga Simba na Yanga kwangu ni rekodi nzuri, nimeingia kwenye kitabu cha washambuliaji waliowahi kuzifunga. Pia kwa upande wangu kama mchezaji nimeweka historia kwenye maisha yangu ya soka kuwahi kufanya kitu hicho.”

Anasema presha ya kucheza dhidi ya timu hizo zenye mashabiki wengi zaidi nchini ni moja ya changamoto ya wachezaji wengi kushindwa kufunga hivyo yeye kupata nafasi na kukwamisha mpira nyavuni ni rekodi nzuri.

UMAARUFU KAPATIA HAPA

Anasema ameanza kucheza soka akiwa na umri mdogo kutokana na kuamini katika kutumikia kipaji chake na alikuwa akilipa soka kipaumbele zaidi ya shule huku akithibitisha kuwa hakuwahi kuwa na ndoto kubwa zaidi ya kucheza soka.

“Nakumbuka mchezo wangu wa kwanza wa mechi za mashindano nilicheza dabi ya Zambia kati ya timu yangu ya Highlanders dhidi ya Power Dynamos, mechi hiyo ni sawa na Simbva na Yanga kwa hapa Tanzania;

“Ulikuwa ni mchezo wa presha kwangu kwani nilikuwa na umri mdogo, wachezaji wa timu pinzani walikuwa wananitania kuwa sistahili kucheza mechi hiyo huku wakinitaka niende shule kusoma niachane na soka,” anasema.

Anasema dakika 90 za mchezo wapinzani ambao walikuwa wanamtania walimtafuta na kumwambia ana kipaji na anatakiwa kukiendeleza ni baada ya kufunga bao na kutoa pasi ya bao timu take ikiibuka na ushindi.

“Hakika ni historia nzuri kwangu kwenye maisha ya soka kwani mechi hiyo ilinipa umaarufu mkubwa kutokana na umbile langu la utoto na kuibuka shujaa kwenye mechi kubwa kama hile ni moja ya tukio langu bora kwenye maisha yangu ya soka.”

UKAME WA MABAO

Dube ambaye kwasasa ametuopia mabao matano kwenye ligi timu yake ikiwa imecheza mechi 22 za msimu anathibitisha kuwa amekuwa akikamiwa na mabeki, changamoto ambayo inamfanya ashindwe kufunga mara kwa mara huku akibainisha kuwa amekuwa akipata nafasi chache za kufunga.

“Msimu wangu wa kwanza nilifanikiwa kufunga mabao mengi zaidi (14) ni kwasababu mabeki wengi walikuwa hawajafahamu mikimbio yangu na aina ya uchezaji wangu kwasasa nakiri kuwa wamekuwa wakikaba kila njia hii ni kutokana na kunisoma;

“Nina kila sababu ya kupambana kwenye uwanja wa mazoezi kusaka mbinu mpya ambazo zitanifanya niweze kuwa bora na kuithibitishia timu kuwa haijakosea kuendelea kuniamini na kunipa nafasi ya kuendelea kuitumikia.”

KINACHOMKWAMISHA

Dube ambaye amesajiliwa na Azam FC msimu wa 2020/21 na kufanikiwa kucheza msimu huo kwa mafanikio akitupia mabao 14 msimu uliofuata ulikuwa wa majanga kwake kwani alipaja jeraha la goti lililomuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita akifunga mabao matatu tu msimu mzima.

“Hakuna kitu kinarudisha nyuma mchezaji kama kuumia akiwa katika ubora,” anasema. Inaendelea kesho “Ni wachezaji wachache sana ambao wanaweza kurudi na kuendelea walipoishia kwa upande wangu naomba kuthibitisha kuwa nimerudishwa nyuma;

“Nimeanza upya kuipambania kile ninachoamini kwani nilishindwa kusoma nikiamini soka ndio mkombozi wangu sijawa fiti kama nilivyotua msimu wangu wa kwanza bado najikongoja kuhakikisha narudisha ubora nashuikuru uongozi kwa kuniamini na kuendelea kunipa muda zaidi sasa nimeanza kurudi baada ya mguu wangu wa kulia kukaa sawa japo natumia miguu yote.”

Dube anasema mabao matano aliyoyafunga msimu huu ni chachu ya kuendelea kumrudisha mchezoni anatamani kufunga mengi zaidi ili kurudi kwenye ushindani kama aliouonyesha msimu wake wa kwanza kutua Tanzania.

ANAMKUBALI SOPU

Anasema ni moja ya wachezaji bora walio ndani ya timu ya Azam FC ambaye amekamilika kwa kila kitu anajua kufunga na kutoa asisti ni mpambanaji na sio mtu wa kukata tamaa.

“Namuheshimu na alipofika nilimuita na kumwambia wewe ni mchezaji mzuri na bora tunatarajia mambo mazuri kutoka kwako amini kile unachokifanya ni bora;

“Alipofunga sikuacha kumsisitiza kuwa yeye ni bora na ni mchezaji muhimu ndani ya timu tunamtegemea kwa mengi ili aweze kutusaidia kwa pamoja tuweze kufikia malengo,” anasema.

SABABU AZAM KUYUMBA

Anasema wapo pia hawafurahishi na kile kinachoendelea ndani ya timu kushindwa kupaa matokeo huku akikiri kuwa kinachochangia wao kushindwa kuendeleza ubora kuwa ni mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi.

“Timu yoyote ambayo inafanya mabadiliko ya benchi la ufundi mara kwa mara haijawahi kuwa na matokeo mazuri na mafanikio kwenye ligi wanayioishiriki hii ni kutokana na timu kukosa muendelezo mzuri wa mfumo;

“Kila kocha anamfumo wake anaweza akaja kabla hata timu aijaweza kuuelewa analetwa kocha mwingine ambaye pia anamfumo wake akili zetu kama wachezaji tunarudi kuanza upa hii ni moja ya sababu ya timu yetu kupoteana na kushindwa kuwa bora.”

Anasema “suala la kusajili wachezaji tunacheza mpira wa aina tofauti kila mchezaji anaubora wake na mapungufu ni rahisi kuelewana tofauti na mfumo wa kocha ambaye kuna ambaye anapenda kukimbia sana mwingine kumiliki mpira na mwingine kujilinda.”

HAWAWAZI TENA SURE, MUDA

Anasema alipotua Azam FC alikutana na viungo Mudathir Yahya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao wote wamejiunga na Yanga kuwa ndio wachezaji ambao walikuwa wamemuwezea mikimbio yake na kumlisha mipira mingi iliyozaa mabao.

“Sure na Mudathir ni wachezaji ambao nawakumbuka sana kwasababu tayari tulikuwa tumetengeneza bondi zuri ya kuelewana kiwanjani kwa sasa nafurahi zaidi nikicheza pamoja na Yahya Zayd na Ayoub Lyanga ambao pia naona tunatengeneza maelewano mazuri;

“Kila mchezaji aliyepo ndani ya timu ni mzuri na anafanya kazi nzuri utofauti ni aina ya uchezaji pia ujio wa mastyaa wapya wameongeza kitu ndani ya timu japo tunahitaji muda zaidi ili kuweza kutengeneza maelewano mazuri ambayo yataipa timu mafanikio.”

AZAM INAMPA PRESHA

Baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu na kuendelea kuaminiwa na benchi la ufundi sambamba na viongozi kumpa mkataba wa kuendelea kubaki ndani ya timu hiyo mshambuliaji huyo anakiri kuwa wanampa presha ya kumtaka ajitume zaidi ili kuwathibitishia kuwa hawajakosea kumbakisha ndani ya timu hiyo.

“Unajua uongozi ukikuamini unatarajia makubwa kutoka kwako na mimi nimetoka majeruhi napambana kuji[pambania ili niwe bora hivyo nakumbana na changamoto kubwa ya kuhakikisha nakuwa miongoni mwa mastaa ambao wanaipa timu matokeo mazuri;

“Hii itaendelea kunijengea uaminifu na kunipa nafas ya kuaminiwa zaidi kwa kuisaidia timu naomba kuwaambia viongozi kuwa natambua thamani kubwa wanayonipa sina kitu kingine cha kuwalipa zaidi ya matokeo mazuri ikiwa ni pamoja na mimi mwenyewe kufunga.”

HADI ANAITWA MACHAPATI

Anasema tangu ametua Tanzania na kujiunga na Azam FC amekuwa muumini mkubwa wa chapati na hicho ndio chakula chake pendwa ambacho hadi wachezaji wenzake wameamua kumbadili jina kwa kumuita mzee wa Chapati.

“Napenda sana chapati ndio chakula changu pendwa wachezaji wamekuwa wakinitania muda wa kula unapofika mzee wa chapati na huwa wananiachia ata nikiwa sipo wanauliza idadi ya zilizopo ili nisije nikakosa kitu ninachokipenda;

“Imetokea tu napenda hicho chakula kila kitu kinapatikana hapa lakini mimi huniambii kitu kuihusu chapati na ndio chakula kinachopatikana kwa wingi hapa kwasabbu sio mimi tu napendelea ni wachezaji wengi ila mimi ni zaidi.”

ANAONA KITU KWA CHIRWA

Ni washambuliaji wengi wamepita Azam FC tangu msimu wa 2020/21 ambao Dube alitua ndani ya timu hiyo kwa upande wake amethibitisha kuwa Obrey Chirwa ambaye anakipiga Ihefu FC kwa sasa ndiye mshambuliaji wake bora kuwahi kumshuhudia na alitamani angekuwa naye pamoja hadi sasa.

“Chirwa ni mshambuliaji mzuri mpambanaji na mwalimu uwanjani lakini soka ni kazi ambayo inamfanya mchezaji akaonekana bora leo na kesho akawa mchezaji wa kawaida kuondoka kwake ni mipango ya uongozi siwezi kuzungumzia zaidi lakini kwangu bado ni bora;

“Nimepata nafasi ya kufanya kazi na washambuliaji wengi siwezi kusema ni wabaya hapani ni wachezaji wazuri lakini chaguo langu kwa nyakati nilizocheza na Chirwa nilitamani kuendelea kuwa pamoja naye.”

HANA MZAHA NA KAZI

Ni nadadra sana kwa mastaa hasa wa ligi kuu kurudia kutazama mechi walizo cheza ili kuweza kusawazisha makosa waliyoyafanya kwenye mchezo husika kwa upande wa Dube amefunguka kuwa ubora wake unatokana na kurudia kujitazama na kufanyia makosa mapungufu yake kabla ya kocha kumuelekeza.

“Napenda kujitazama ni nini nimekifanya kwenye kila mechi ninazocheza huwa najitengea muda nakaa chumbani na kuangalia marudio ya mchezo nikiona mapungufu nayafanyia marekebisho mwenyewe kwenye uwanja wa mazoezi kabra ya kocha;

“Hili limekuwa likinifanya kuwa bora kwenye mchezo unaofuata kwasababu najua nini natakiwa kukifanya ili nisirudie makosa yangu japo kunakuwa na mbinu tofauti lakini najitahidi sana kuto kurudia kile nilichokifanya kwa makosa mechi iliyopita.”

KIKOSI CHAKE HATARI

Zikiwa zimebaki mechi nane kwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara mshambuliaji wa Azam FC, Dube amefunguka kuwa ligi ya msimu huu inaushindani mkubwa na imekuwa bora kutokana na timu nyingi kujiandaa vyema ikiwa ni sambamba na usajili mzuri uliofanyika.

Anasema kwa upande wake ameshuhudia timu nyingi zikiwa na mastaa wakubwa na bora ambao wamekuwa wakizipambania timu zao kupata matokeo na kutaja kikosi chake bora ambacho amekiri kuwa ni cha mauaji hasa safu ya ushambuliaji kinaweza kutumia mabao mengi sana.

Anasema langoni anampanga Aishi Manula (Simba), Lusajo Mwaikenda, Bruce Kangwa, Danny Amoah wote (Azam FC), Henock Inonga (Simba), Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Yanga), Ayoub Lyanga (Azam FC), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Yanga), Fiston Mayele ‘Yanga’, Clatous Chama (Simba), Never Tiger (Azam FC).

HANA HAMU NA NYOSSO

Tanzania imebarikiwa vipaji vya wachezaji wengi katika nafasi tofauti nimecheza kwa muda wa misimu mitatu sasa nimeshuhudia vipaji vingi lakini kwa upande wa wachezaji wanaonipa changamoto kutokana na nafasi ninayocheza ni mabeki.

“Nakutana na changamoto nikicheza na beki wa Yanga Dickson Job na Henock Inonga ni m,iongoni mwa mabeki bora na wasumbufu kuwapita kirahisi kutokana na kucheza kwa kutumia akili zaidi na sio nguvu; “Nyosso ndiye beki mgumu sana kwangu nikiwa na mechi na timu yake huwa najianoa zaidi tofauti na mechi nyingine zote ni beki ambaye yupo fiti anaingia sana mwilini anahitaji kucheza naye kwa akili.”

Anasema Nyosso ni beki wake bora wa muda wote amekuwa akimpa mtihani mgumu kina wanapokutana kutokana na kutumia nguvu zaidi hivyo anamfanya awe na mazoezi ya ziada kumkabili.

AKAMINKO BONGE LA KIUNGO

Ni kiungo ambaye amekuwa akizungumzwa sana tangu amesajiliwa ndani ya timu hiyo kutokana na ubora alionao ambao Dube amethibitisha pia kuwa ni mchezaji mpambanaji ambaye anaipambania timu.

“Kiungo ni lazima azungumzwe sana midomoni mwa mashabiki kwasababu ni mchezaji ambaye anategemewa kwenye kupandisha mashambulizi nisawa na mshambuliaji ili kutajwa sana ni lazima awe anafunga kama ilivyo kwa Fiston Mayele;

“Akaminko ni kiungo mzuri kwasababu anajua kukaa na mpira mguuni pia ni mwepesi wa kutoa pasi pale anapotakiwa kufanya hivyo na zimekuwa zikifika kwa usahihi pia anajua kupandisha mashambulizi na kusaidiana na mabeki kuhakikisha timu inapunguza makosa safu ya ulinzi.”

Columnist: Mwanaspoti