Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Droo ya kibabe CAF...Simba, Yanga uso kwa uso na Waarabu

Yanga Na Simba Droo ya kibabe CAF...Simba, Yanga uso kwa uso na Waarabu

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ile droo ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa kalenda Novemba 16, inafanyika leo pale Cairo, Misri huku vigogo na wawakilishi wa nchi, Simba na Yanga zikiwa kwenye mtego wa kuangukia mikononi mwa timu za Kiarabu, lakini makocha wa timu hizo wametamba wako tayari kukabiliana nao ikiwa watapangwa pamoja.

Simba wametinga hatua hiyo ya makundi kupitia Ligi ya Mabingwa, wakati watani wao, Yanga yenyewe ipo Kombe la Shirikisho baada ya kuiduwaza Club Africain ya Tunisia kwa kuichapa kwao bao 1-0 katika mechi ya marudiano ya play-off kwani mchezo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu jijini Dar.

Yanga ilianguka kutoka Ligi ya Mabingwa kwa kupigwa jumla ya mabao 2-1 na Al Hilal ya Sudan.

Awali droo hiyo ilipangwa kufanyika Jumatano ya Novemba 16 na sasa kufanyika leo kuanzia saa 8 mchana ikitanguliwa na ile ya Ligi ya Mabingwa yenye vigogo vitupu kabla ya mechi za hatua hiyo kuanza kupigwa Februari mwakani.

MAMBO YATAKAVYOKUWA

Kama hujui kutakuwa na vyungu vinne na kila kimoja kitakuwa na majina ya timu nne na kila kundi litajumuisha timu kutoka chungu cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne.

Simba wao wamepangwa katika chungu cha tatu pamoja na CR Belouizdad na JS Kabylie za Algeria na Al Hilal ya Sudan ambazo hawezi kupangwa nazo katika kundi moja.

Chungu cha kwanza kina Mabingwa wa kihistoria waliobeba Ligi ya Mabingwa mara 10, Al Ahly ya Misri, mabingwa mara tatu wa ligi hiyo, Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia iliyotwaa taji hilo mara nne na Raja Casablanca iliyoibeba taji hilo mara tatu.

Chungu cha pili, kuna Zamalek ya Misri iliyobeba taji mara tano, kisha Mamelodi Sundowns ya sauzi iliyobeba mara moja pamoja na Petro Luanda ya Angola na AC Horoya ya Guinea, ilihali kundi la mwisho lina timu za Al Merrikh ya Sudan, AS Vita ya DR Congo, Coton Sport ya Cameroon na Vipers ya Uganda.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga imepangwa chungu cha pili na DC Motema Pembe ya DR Congo, AS FAR ya Morocco na US Monastir ya Tunisia ambazo kwa vyovyote haiwezi kukutana nazo katika kundi moja.

Chungu cha kwanza kina bingwa mara mbili wa Shirikisho, TP Mazembe ya DR Congo, Pyramids ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na USM Alger ya Algeria, huku chungu cha tatu kikiwa na FC Saint-Éloi Lupopo ya DR Congo, Al Akhdar ya Libya iliyoing’oa Azam, Real Bamako ya Mali na Rivers United ya Nigeria iliyoitoa Yanga Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Katika chungu cha nne chenyewe kitakuwa na Diables Noir ya Congo Brazzaville, Future ya Misri, Marumo Gallants ya Afrika Kusini na ASKO Kara ya Togo.

Columnist: Mwanaspoti