Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dokta Shein, mwenza aliyeaminiwa na Mkapa

Mkapa Shein Rais Dr. Shein akiwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MIAKA 10 ya utawala wa Rais Ali Mohamed Shein, kuiongoza Zanzibar, inafikia ukingoni mara baada uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Maandiko mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, vinamtaja Dk Shein kama mwanasiasa aliyeonyesha kipaji cha uongozi tangu akiwa kijana.

Anatajwa kupitia nafasi mbalimbali za uongozi, lakini kwa sehemu kubwa, ni kuibuliwa kwake na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kuwa Makamu wa Rais Julai 12, mwaka 2001, kulikomfanya Shein kujulikana zaidi kwa walio wengi.

Juni 12, 2001, Mkapa alimteua Dk Shein kushika wadhifa huo na siku iliyofuata, yaani Juni 13, 2001, akaliwasilisha jina lake bungeni ambako wabunge walilipitisha kwa kuliidhinisha kwa kura nyingi.

KUONDOKA DK OMAR

Uteuzi huo ulitokana na kifo cha aliyekuwa mtangulizi wake, Dk Omar Ali Juma , aliyefariki Julai 4, 2001 na kuibua mshtuko nchini na kwingineko Afrika.

Rais wa wakati huo , Mkapa, aliutangazia umma na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo vyombo vya kimataifa, Julai 5, mwaka 2001 kuwa Dk. Omar wakati huo akiwa na miaka 60 amefariki duniani kutokana na ugonjwa wa moyo.

Rais Mkapa alinukuliwa akitangaza kifo cha makamu wake wakati huo aliyefariki saa 5:45 usiku na alitangaza siku saba za maombolezo ya kifo hicho.

Dk. Omar aliaminika kuwa kiongozi aliyekubalika kwa karibu na Mkapa. Alishika wadhifa huo tangu walipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 1995.

Mkapa alimtaja Dk Omar kama msaidizi wake wa karibu, mtu mwenye thamani, mchapakazi na asiyekuwa na makuu aliyeacha pengo kubwa kwa taifa

UTEUZI WA SHEIN

Ni jambo lililotarajiwa kutokana na mtizamo huo wa kiwasifu, uteuzi wa mrithi wa Dk. Omar, angepatikana kiongozi mwenye kaliba hiyo, hapo ndipo alipoibuliwa Dk. Shein, akitokea kwenye safu ya Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Dk. Shein , ambaye kitaaluma anaangukia fani ya utabibu wa binadamu, mwishoni mwa wiki iliyopita katika vikao vya CCM vya kumpitisha mrithi wake jijini Dodoma, alijitambulisha kuwa na miaka 72 na kuitumikia SMZ tangu mwaka 1969.

Hakuonekana sana katika ngazi za juu kiutendaji serikalini, hadi pale alipoibuliwa kutumika kama naibu waziri ndani ya SMZ. Kitaaluma, elimu yake ya juu aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Odessa nchini Urusi na pia kupata elimu zaidi Uingereza.

Anatajwa kuonyesha umahiri wa uongozi tangu alipokuwa kijana hasa baada ya kujiunga na Umoja wa Vijana wa Afro-Shirazi (ASP) wakati akiwa mwanafunzi .

Mmoja wa watu waliowahi kusoma na Dk Shein katika Shule ya Lumumba huko Zanzibar, Dk Mohammed Saleh Jidawy, alikaririwa na vyombo vya habari akitaja wasifu wake mwingine kuwa mwanariadha hodari, katika ujana wake.

Pia, katika zama hizo za ujana anatajwa kujitolea katika shughuli za kijamii za kuwaelimisha vijana wenzake kujitambua na ndani ya siasa za ASP, anatajwa kuwanoa wenzake kwenye ulingo wa siasa za mwelekeo wa chama chao.

Mwaka 1997, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM – NEC na kutokana na nafasi hiyo, aliteuliwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwaka 2005.

KUINGIA IKULU

Dk. Shein alishinda uwakilishi katika jimbo la Mkanyageni katika uchaguzi mkuu wa Novemba 2000 na kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Baada ya ushindi huo, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, Novemba 2000.

Wakati wa kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa 2005, Dk Shein aliteuliwa kuwa mgombea mwenza kupitia CCM. Wakati huo, mgombea urais kupitia chama hicho alikuwa Jakaya Kikwete.

Annet Ngahyoma, mmoja wa watu waliofanya kazi na Dk Shein baada ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, ananukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kiongozi huyo ni mtu mpole na mwenye kupenda dini.

URAIS WA Z’BAR

Dk Shein aliongoza baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2010 na kuchukua hatamu za uongozi. Ilikuwa ni baada ya Rais Amani Karume, aliyekuwepo madaraka, kumaliza kipindi chake cha uongozi.

Shein aliapishwa Novemba 3 mwaka 2010 na kuanza kazi na hata leo anajulikana pia kuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumbishwa katika kile anachokiamini.

Mwaka 2015, Dk Shein aliwania urais kwa mara ya pili kukamilisha kipindi cha miaka 10 ya urais wa Zanzibar, lakini akiwa ametumikia takribani miaka tisa ya jukumu la Makamu wa Rais wa Muungano.

Baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Dk Shein atastaafu kwa mujibu wa katiba , akiwa ni kiongozi aliyedumu madarakani kwa muda mrefu akizitumikia Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Columnist: www.tanzaniaweb.live