Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dk. Mengi- Tamwa yamuenzi kwa kuacha alama ya haki za binadamu, usawa

MENGI Dk. Mengi- Tamwa yamuenzi kwa kuacha alama ya haki za binadamu, usawa

Wed, 29 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk. Rose Reuben, anamzungumzia Dk. Reginald Mengi kwa jitihada zake za kupigania haki za wanawake na watoto kupitia vyombo vyake vya habari kwa kushirikiana na chama hicho.

“Magazeti yake, televisheni pamoja na redio zake vilifanya kazi kubwa kupigania haki za wanawake na watoto, tuliweza kufanya kazi na vyombo hivyo kwa kurusha taarifa zinazotetea haki za wanawake na watoto pamoja na matangazo ya kuhamasisha kutokomeza ukatili dhidi yao,” anasema Dk. Rose.

Anasema alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha waandishi wa habari na tasnia nzima inapata ajira kwa wingi kupitia vyombo vyake vya habari.

Mchango wake mkubwa katika sekta ya habari ulikuza vyombo vya habari nchini na kujipatia sifa nyingi.

Katika jitihada zake hizo, Rose anasema Dk. Mengi alikuwa anapenda kuona tasnia ya habari inasonga mbele kila siku, hakupenda kuiona inarudi nyuma.

“Sisi Tamwa tunamkumbuka Dk. Mengi kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika sekta ya habari kwa kukuza vyombo vya habari. Waandishi wa habari na tasnia nzima ilipata ajira kwa wingi kupitia vyombo vyake vya habari.”

“Nakumbuka tangazo la ‘Sidanganyiki’ lililokuwa linarushwa na kituo cha ITV ambalo lilikuwa linawaasa watoto wa kike wasidanganyike na mafataki kwa kupata ujauzito. Ni tangazo ambalo lilisaidia sana kupunguza mimba za utotoni, lakini pia matangazo ya kupunguza mimba za utotoni nayo tuliyatangaza sana katika vyombo vyake vya habari.”

Kupitia vyombo hivyo, Rose anasema habari nyingi za ukatili wa kijinsia zilipewa nafasi kubwa kwa kuripotiwa na kuelimisha jamii kwa sababu alipenda kupigania haki ya wanawake na watoto.

Anasema ameacha alama ya haki za binadamu na usawa wa jinsia kwa Watanzania ikiwa imeeleweka kwa kiasi kikubwa. “Kwa sababu awali suala hilo lilikuwa halizungumzwi sana, lakini kupitia vyombo vyake vya habari vilisaidia sana angalau suala la jinsia linaeleweka kwa wanawake na wanaume.”

Kurushwa kwa taarifa kwenye vyombo hivyo, Rose anasema kumesaidia Watanzania sasa kufahamu kuwa usawa wa kijinsia ni usawa wa kijamii na siyo usawa wa kibailojia ambao watu wamekuwa wakishindana kimabavu.

Amewakumbusha wamiliki wengine wa vyombo vya habari kuendelea kuwathamini waandishi wa habari, kama ilivyokuwa kwa Dk. Mengi.

“Uandishi wa habari ni kazi, ni taaluma na siyo taaluma ambayo kila mtu anaweza kuifanya. Wamiliki wa vyombo vya habari waendelee kuwathamini waandishi wa habari wanawake na wanaume, waendele kuthamini kazi wanazozifanya, na waithamini habari.”

“Kama Tamwa tunasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari waendelee kuthamini, kutoa taarifa za kijinsia, kuzuia ukatili wa wanawake na watoto, wapaze sauti za wanawake ili tufikie maendeleo endelevu.” Anasisitiza Rose.

Anasema Tamwa inamuenzi Dk. Mengi kwa kuwatetea watu wasiojiweza wakiwamo watoto na wanawake wenye ulemavu.

Tamwa pia inawajengea uwezo wanawake wanahabari kitaaluma kwa kuwawezesha mikopo isiyo na riba ili wajiendeleza kielimu na kuendelea kutetea wanyonge ambao sauti zao hazisikiki.

Dk. Rose anasema Dk. Mengi alikuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya mambo makubwa kwenye tasnia ya habari kwa sababu hakuwa mbaguzi katika kuwapatia uwezo waandishi wa habari hata wale ambao hawakuwa katika vyombo vyake.

“Dk. Mengi alikuwa amewajengea uwezo waandishi wote bila ya kuwabagua pamoja na kuwaendeleza kimasomo,” anasisitiza Dk. Rose.

Columnist: www.tanzaniaweb.live