Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Desemba kipindi kigumu Ligi za Ulaya

Man United Happy Desemba kipindi kigumu Ligi za Ulaya

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kile kipindi cha majira ya baridi kali barani Ulaya ndio kimeanza kunoga ambapo theluji inadondoka na kufanya mazingira yake kuwa ya baridi kali inayoshuka mpaka chini ya nyuzijoto sifuri.

Hivi sasa utabiri wa hali ya hewa unaonyesha halijoto ya Uingereza ni sentigredi 5, Ufaransa na Hispania 7 na Italia 11. Chini ya nyuzijoto sifuri ni Ujerumani nyuzijoto -4 na Urusi ni -7.

Kipindi hiki kigumu kwa miili ya wachezaji ndio ambacho makocha wenye mbinu za kiufundi kabambe ndio wanafanikiwa kubeba ubingwa au kuwepo katika timu nne bora za juu katika ligi.

Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson kipindi kama hiki endapo akiongoza ligi hadi Krisimasi na Boxing Day alikuwa akifanikiwa kubeba ubingwa EPL.

Hii ilichangia kutengenezwa nadharia ambayo ilihusisha kuongoza ligi mpaka kufikia Krisimasi ndio anayekuwa bingwa wa EPL.

Sababu ni kuwa mpaka kufikia hatua hiyo tayari wako mzunguko wa pili wa ligi ambapo wachezaji wanakuwa wamechoka, au kuwa majeruhi na huku wapo kipindi cha baridi kali.

Hivyo ili kufanikiwa ni lazima uwe na kikosi bora na stahimilivu kufikia hatua hiyo.

Bahati mbaya nadharia hiyo iliyeyuka kwani kuna timu kama Chelsea, Liverpool, Arsenal zilipoongoza ligi kipindi cha Krimasi hazikufanikiwa kutwaa ubingwa.

Kipindi cha baridi kali kinachoenda hadi mwezi wa 3-4 barani Ulaya huwa ni kipindi kigumu kwa mchezaji yoyote aliyepo katika mazingira hayo.

Lakini kwa EPL huwa ni kigumu zaidi kwani wao hawana mapumziko ya kipindi cha baridi kali kama ilivyo katika la Liga na Bundesliga.

Mapumziko ya ligi hizi huwapa wachezaji faida kubwa ya kimwili na kiakili kwani hupata muda wa kuungana na familia zao kipindi cha Krisimasi na Mwaka mpya.

Wapo wanasaikolojia waliwahi kueleza kuwa kitendo cha ligi ya EPL kuendelea kuchezwa kipindi hiki kinawaathiri kiakili baadhi ya wanasoka kwani wanakosa muda wa kuungana na familia zao.

Mtakumbuka ligi nyingi za Ulaya huwa na wachezaji mchanganyiko kutoka mataifa mbalimbali wakiwamo wachezaji kutoka Afrika na Amerika ya Kusini ambao hawajazoea majira ya baridi kali.

Ingawa kisayansi kadiri mwili unavyopata ugumu katika mazingira ndivyo pia mwili hunyumbulika kwa kujibadili ili kuweza kukabiliana na hali kama hizo ndio maana baadaye wachezaji huzoea hali hiyo.

BARIDI INAATHIRI MWILI HIVI

Udhibiti wa joto la mwili katika mazingira ya baridi kali ni jambo ambalo linaweza kuleta athari katika kiwango cha mchezaji anayecheza katika mazingira hayo.

Katika mazingira ya joto au baridi mwili hujaribu kulinda mazingira ya ndani ya mwili yawe sawa katika kiwango chake inachohitajika kwa ajili ya shughuli zake.

Joto la kawaida la mwili wa mwanadamu huwa ni nyuzi joto 36.9 ambazo ni sawa na 98.6 F. Joto hili la mwili halitakiwi kushuka sana wala kupanda sana hivyo mwili hudhibiti hali hii isitokee.

Kipindi cha baridi mwili hulazimika kujibadili na kufanya mbinu ikiwamo kutetemeka ili kuupasha mwili moto.

Kwa kawaida misuli huwa na uhitaji wa damu kwa wingi ili kuweza kufanya kazi ya kujikunja na kukunjuka hatimaye kucheza kwa kiwango. Katika baridi utiririkaji huu hupungua na kuathiri misuli.

Damu hupungua kutiririka juu ya ngozi kwa sababu mishipa ya damu iliyopo juu ya ngozi husinyaa na kujificha ndani ya ngozi lengo ni kulinda joto la ndani ya mwili lisishuke.

Damu kupungua kutirika katoka katika ngozi na kuelekea kwa wingi ndani ya mwili ni muhimu hasa pale inapokuwa na ongezeko la uhitaji wa nguvu mwilini.

Mwili hufanya hivi ili kujaribu kuendelea kulinda joto la mwili na wakati huo huo kutengeneza nguvu zaidi itakayotumika na misuli kwa ajili ya mazoezi au kucheza.

Shuguli nyingine za mwilini kama za kuufanya mwili kuwa na maji mengi nazo huathirika wakati wa baridi ikiwamo upoteaji wa maji kwa jasho hupungua wakati upoteaji wa maji kwa kupumua huongezeka.

Wanasoka wanakuwa katika hatari ya upungufu wa maji mwilini kwa sababu hisia ya kupata kiu huwa inapotea katika mazingira ya baridi ukilinganisha na majira ya joto.

Hali hiyo huwafanya wachezaji kutokunywa maji ya kutosha na huku wakiwa wanapoteza maji mwilini kwa njia ya kupumua kuliko kutoka jasho.

Maji ni kitu muhimu kwa mwili katika kudhibiti mazingira ya ndani ya mwili, upungufu wa maji mwilini ni kihatarishi cha kupoteza joto la ndani ya mwili katika mazingira ya baridi.

Mwili unapokuwa na maji ya kutosha husaidia ujazo wa damu mzungukoni kuwa mzuri, hata wakitoka jasho na kupoteza joto bado mwili huweza kulinda kiwango cha utendaji wa misuli ya mwili.

Lakini hali hii inakuwa tofauti katika kufanya mazoezi au kucheza katika baridi kali kwani mwili unakuwa katika mazingira ambayo mwili hupata shinikizo kubwa na kuathirika katika njia nyingi.

Kiujumla misuli iliyopata baridi huwa ni dhaifu kiutendaji, ujibuji wa mapigo katika miitikio mbalimbali ya kimwili huwa ni ya taratibu na dhaifu.

Misisimko ya mfumo wa fahamu inayotumwa na mishipa ya fahamu kwenda katika ubongo kupata tafsiri na kutolewa uamuzi na kurudishwa na maelekezo katika maeneo ya mwili huwa ni taratibu.

Hali hii inapokuwapo ina maana uamuzi wa kimwili unakuwa wa taratibu katika baridi.

Katika baridi misuli ya mwili inakuwa mizito na wakati huo huo inashindwa kunyumbulika na wepesi wa kufanya vitendo kwa haraka na kwa wakati.

Inapotokea misuli ya mwili haipati damu na virutubisho kwa wingi na kwa haraka na kwa wakati husababisha misuli kutokuwa na nguvu za kutosha kuweza kutenda mambo mbalimbali kwa kiwango.

Pia misuli iliyo baridi na migumu au kupata mkazo huwa haifanyi kazi kwa kiwango, hali hii ndio inayochangia kupata majeraha kirahisi ukilinganisha na misuli iliyopo katika mazingira ya joto.

Kiwango cha mchezaji huathirika hii ni kutokana na mwili kufanya kazi kubwa kwa nguvu nyingi katika shughuli za ndani. Vile vile moyo hufanya kazi ya ziada katika mazingira ya baridi.

Mwili huweza kujibadili haraka na kukabiliana na mazingira magumu ya joto kali, lakini kujibadili katika mazingira magumu ya baridi kali huwa ni taratibu sana.

CHUKUA HII

Katika mechi za UEFA na za ligi Ulaya za wiki hii wachezaji walioko nje wanavaa makoti mazito na huku wakijifunika na mablanketi ili wanapoingia uwanjani misuli imepata moto hatimaye kuwa na ufanisi.

Mazoezi, mikakati na mbinu za kiufundi kabla ya majira hayo na ustahimilivu wa asili wa mwili wa mchezaji vinaweza kuchangia kucheza kwa kiwango katika mazingira magumu ya baridi kali.

Columnist: Mwanaspoti