Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dawa ya rushwa ya ngono ni uthubutu

Sex South Africaa Dawa ya rushwa ya ngono ni uthubutu

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JIJINI Dar es Salaam Ijumaa iliyopita kulifanyika Kongamano la Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili Duniani lililoandaliwa na Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania.

Katika kongamano hilo, Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lekayo aliwasilisha ripoti ya utafiti wa rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu, uchunguzi kifani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa, bila umma kuthubutu na kujitoa dhahiri, tatizo la rushwa ya ngono litazidi kukwamisha maendeleo ya kielimu na kiuchumi nchini kwani taifa haliwezi kuendelea kwa kuwa na watu wenye vyeti vyenye alama za ubora katika masomo lakini zilizopatikana kama zawadi baada kubadilishana kwa ngono.

Kadhalika, hakuna uchumi wa nchi unaoweza kuimarika na kuifanya nchi hata kuwa na ulinzi na usalama imara kama watu wake wanaajiriwa au kupandishwa vyeo kwa kuwa tu wametoa rushwa ya ngono.

Hali hiyo hiyo pia ni hatari kiafya hasa katika kipindi hiki ambacho kuna magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi.

Kwa msingi huo, zipo mbinu zinazohitaji uthubutu wa kila mdau ili kushinda katika vita hii ikiwa ni pamoja na wahusika wakiwamo waathirika na mashuhuda kuwa tayari kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria.

Hata hivyo, ushahidi huu lazima utafutwe, uchukuliwe na kutolewa kwa umakini ili usipingane na sheria.

Mbinu nyingine ni kuwapo kwa mfumo unaowalinda wafanyakazi au wanafunzi wanajikuta katika mazingira magumu kwa kutoa taarifa dhidi ya rushwa ya ngono.

Aidha, uongozi wa vyuo uimarishe taasisi na kamati zinazoshughulikia masuala ya maadili ya watumishi ikiwa ni pamoja na kamati za maadili, vitengo vya jinsia na ofisi ya mshauri wa wanafunzi.

Hili lifanyike kwa kuwapatia nyenzo, vitendea kazi na mafunzo ya kuwezesha kushughulikia masuala ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinisia katika vyuo.

Kadhalika, wanafunzi wa vyuo waongeze jitihada katika masomo, wazingatie maadili, wasikubali kurubuniwa, wavunje ukimya kwa kupaza sauti kunapotokea viashiria vya kuwanyima haki zao na wachukue hatua stahiki wanapopokonywa haki hizo na kufikisha malalamiko yao Takukuru kupitia kamati zao, taasisi za kiraia na wao wenyewe.

Wanafunzi katika taasisi za elimu waungane na kushiriki zaidi katika kampeni za kupambana na rushwa ya ngono huku taasisi za kiraia nazo zikiendelea kutumia ripoti hiyo kuimarisha ubia na Takukuru katika vita hiyo hasa katika utaifiti na elimu ya juu ili umma ujue wazi kuwa ukatili huu wa kijinsia ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Taasisi za jinsia zijijengee uwezo wa uelewa wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 kuhusu rushwa ya ngono ili waweze kusimamia utekelezaji wake vyuoni sambamba na kuwajengea uwezo wanafunzi na jamii yote ya chuo kulielewa vyema suala hili ili waweze kujitetea na kupambana nalo.

Hizo ni njia chache miongoni mwa nyingi katika kupambana na tatizo hili na ndiyo maana ninasema: “Dawa ya rushwa ya ngono ni uthubutu.”

Columnist: habarileo.co.tz