Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dakika kadhaa na Andrey Arshavin jijini Kazan`

Arshavin Andrey Aaa Dakika kadhaa na Andrey Arshavin jijini Kazan`

Sun, 25 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kazan mji ulio ulio kando ya maziwa makubwa ya Volga na Kazanka, kusini Magharibi mwa Russia. Hapa ndipo nilipokutana na Andrey Arshavin. Ilikuwa kwa mara ya kwanza. Alikuwa katika suti yake nyeusi, shati jeupe na miwani ambayo ilimfanya awe kijana wa shule tofauti na Arshavin ambaye tulimfahamu zamani.

Ilikuwa katika mechi za vijana za michuano ya Games of the Future inayoendelea jijini Kazan. Arshavin ndiye alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo. Tabasamu usoni, umaarufu uliopitiliza ulifanya watu wengi wawe karibu yake zaidi. Alama ya soka la Russia. Atababaki hivyo kwa muda mrefu ujao.

Maisha yanataka nini zaidi nikiwa kama shabiki wa Arsenal niliyepitiliza. Sikuwa nataka kufanya naye mahojiano. Wala sikuwa na ahadi ya mahojiano naye. Niliongea naye mambo mawili matatu yanayohusu Arsenal. Basi tu. Maisha yalinirudisha nyuma Arshavin akiwa katika ubora wake Arsenal.

Yakanirudisha usiku ule wa Aprili, 2009 ambao aliwafunga Liverpool mabao manne mguuni mwake, Anfield. Uwanja ulikuwa umejaa. Bahati mbaya tu wakati huo Arsene Wenger alikuwa amepoteza ubora wake pambano likaisha kwa sare. Inakuwaje unamnyima ufalme mchezaji aliyefunga mabao manne mechi moja halafu pambano likaisha kwa sare? Sijawahi kuelewa mpaka leo.

Lakini sio mbaya nikikiri namna ambavyo Arshavin alicheza Arsenal katika nyakati mbaya. Katika zile nyakati ambazo Wenger alikuwa amepoteza maarifa. Kina Pep Guardiola walikuwa wameingiza mpira mpya na bado alikuwa katika dunia ya kiza.

Labda mchezaji mzuri kama yeye angecheza leo chini ya Mikel Arteta huenda mabao yake manne pale Anfield yasingeishia kuipamba sare ya kijinga.

Wakati kina Guardiola wakituingiza katika mpira mpya, Wenger alikuwa hajui kufundisha ‘pressing’ kuanzia eneo lolote lile la uwanja. Maisha yalikuwa magumu kwa mashabiki wa Arsenal nyakati hizo. Kufungwa mabao 6-1 yalikuwa maisha ya kawaida.

Kusimama kando ya Arshavin hapa Kazan kulikumbusha mambo mengi. Huwa tunaambiana kwamba wachezaji wafupi hawana nafasi ya kutamba Ulaya. Sio kweli. Wanayo. Arshavin ananifikia mabegani. Kuipata ‘selfie’ na yeye nililazimika kukunja mgongo. Ni mfupi kama alivyo. Sijawahi tu kukutana na Sergio Aguero.

Kumbe kinachotakiwa ni mchezaji kuwa na uimara mkubwa miguuni. Kinachotakiwa ni mchezaji kuwa na kasi vilevile. Ndani ya suti ungeweza kumuona Arshavin ambaye mapaja yake yalikaribia kuchana suti.

Hata hivyo, kwa nyakati zile asingeweza kupambana hewani na Martin Skirtel. Ndio ukweli. Inabidi uwe bora miguuni, lakini kila mtu ana nafasi ya kucheza Ulaya. Hata wachezaji wafupi wapo wengi tu Ulaya.

Lakini hapohapo Arshavin alinikumbusha namna ambavyo wachezaji wa Afrika wanalazimika kupambana haswa kucheza Ulaya. Kwa baridi niliyokutana nayo Russia unalazimika kufanya kazi kubwa kuizoea hali hii kisha uende mguu sawa na wenyeji kama Arshavin.

Hapa Kazan baridi inafikia ‘negative 16’. Kwa sasa kila mahala unakanyaga barafu. Kina Arshavin wamezaliwa hapa, wamekulia hapa, wameanzia kucheza soka hapa. Ukitaka kwenda nao sambamba inabidi uwe na roho ngumu ya mapambano.

Wakati mwingine sio kwamba wachezaji wa Afrika wanashindwa kwa sababu ya kutokuwa na uwezo uwanjani. Hapana. Wakati mwingine wanakabiliwa na mambo mengi nje ya uwanja ikiwemo hali ya hewa.

Hata hivyo, Kazan ilinikumbusha pia kwamba kuna wanaume wanatoka makwao kuja kupambana na baridi hii. Wapo. Kuna wanaume walitoka Afrika Magharibi kuja kucheza Kazan kusaka maisha. Kina Alexander Song walipita hapa Kazan kukanyaga barafu. Kina Obafemi Martins walipita hapa pia wakisaka maisha.

Nilipomuona Arshavin pia kuna jambo nilikumbuka. Wako wapi wachezaji kutoka Russia wanaotamba katika Ligi Kuu England? Hawapo tena. Achilia mbali Arshavin, lakini tulishawahi kuwa na kina Andrei Kanchelskis, Roman Pavluchenko, Yuri Zhirkov na wengineo. Russia haipeleki tena wachezaji mahiri England.

Si ajabu katika televisheni za Russia hauwezi kuona Ligi Kuu England. Katika hoteli ya nyota tano niliyofikia mpira wa Ligi Kuu England hauonekani. Mara nyingi nchi nyingi ambazo zimetoa wachezaji wengi katika Ligi Kuu England huwa zinahakikisha ligi ya England inaonekana. Russia Ligi Kuu England haionekani.

Wakati fulani nilidhani kwamba labda imetokana na uhusiano mbovu kati ya Rais wa Russia, Vladimir Putin dhidi ya mahasimu wake wakubwa kama Wamarekani na Waingereza. Lakini mbona Waingereza na Wamarekani wapo katika michuano hii ya Games of the Future? Kwanini wasikatae kuwepo hapa?

Nadhani ni kwa sababu ya kukosekana kwa vipaji vingi vya Kirusi katika soka la Kiingereza pamoja na ligi nyingine kubwa za Ulaya kama vile Hispania, Ujerumani, Italia, Ufaransa na kwingineko. Kama labda wangekuwa wamejaa huko huenda hali ingekuwa tofauti na wangepambana na watu wa haki za mauzo ya televisheni.

Sijui kama enzi za kina Arshavin walikuwa wanaonyesha, lakini kwa sasa hapana. Mitaani vipaji vipo vingi labda tusubiri huenda vipaji hivyo vikarudi, lakini kwa sasa inaonekana wazi kwamba maisha ni magumu katika soka la Russia na katika anga za kimataifa kwa sasa inajidhihirisha hivyo kwa kiasi kikubwa.

Arshavin kuwa kando yangu pia kuna jambo nilikumbuka. Baada ya kuondoka England ilitajwa kwamba Arshavin alikuwa ni mpelelezi wa siri wa serikali ya Russia. Naam. Imenikumbusha namna ambavyo nchi hii karibu kila mtu muhimu anatajwa kuwa katika orodha ya watu wanaolipwa na serikali ya Putin.

Nchi ya kimafia ambayo unaambiwa kuwa mchezaji ni mpelelezi, bondia ni mpelelezi, mwanamitindo ni mpelelezi. Imenikumbusha mbali tangu wakati ule unaposoma kuhusu maisha ya vita baridi kati ya Magharibi na Mashariki. Sina uhakika kama Arshavin alikuwa hivyo, lakini alipoondoka England mafaili yalivuja kwamba alikuwa anafanya kazi hiyo.

Columnist: Mwanaspoti