Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Corona ilivyokuja na gia ya kusambaratisha mtangamano

Mkutano.webp Corona ilivyokuja na gia ya kusambaratisha mtangamano

Tue, 19 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JANGA la maambukizo ya ugonjwa wa COVID –19 limeendelea kuathiri sehemu kubwa ya mataifa duniani, huku kila nchi ikijikita kuvidhibiti virusi hivyo, kwa kutumia mbinu, rasilimali na desturi zake.

Maambukizo hayo yaliyoanzia kwenye mji wa Wuhan jimbo la Hubei nchini China, yameharibu mifumo ya maisha ya watu katika nyanja tofauti zikiwamo za kisiasa, kiuchumi, michezo, imani na dini.

Kwa mfano, nchini Ethiopia, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu, uliahirishwa kutokana na athari zilizochangiwa na mlipuko wa virusi vya corona.

Bodi ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo (NEBE) ilitangaza kuahirisha uchaguzi huo wa rais na wabunge ambao ungekuwa kipimo kwa serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, baada ya mashauriano na vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi huo.

Hivyo, jambo kubwa lililopo sasa kwenye mataifa mengi (kama si yote duniani) ni kuvidhibiti virusi vya corona kupitia njia zinazowezesha upatikanaji wa tiba, wakati watu wakiendelea kujikinga dhidi ya maambukizo.

Bara la Afrika lenye jumla ya nchi 55 halikukwepa kupata na kuthibitisha maambukizo ya virusi vya corona yalitokea nchini China, ama katika nchi nyingine ambazo raia ama wageni wake waliingia kutoka mataifa yaliyoathirika, na wao wakiwa miongoni mwa wenye virusi hivyo.

Ndivyo ilivyokuwa pia kwa Tanzania ambayo Machi 16, mwaka huu, ilitangaza rasmi kuwa na mgonjwa wa kwanza wa COVID – 19, Isabella Mwampamba, mkazi wa jijini Arusha.

Ukweli ni kwamba, kutokana na asili ya kuenea kwake, maambukizo ya virusi vya corona hayakwepi umuhimu wa ushirikiano kuanzia ngazi ya familia, nchi, jumuiya za kikanda na kimataifa.

Lakini mikakati ya ‘mamlaka’ moja inaweza kutofautiana na ile inayotumiwa na ‘mamlaka’ nyingine, kama ilivyo kwa matumizi ya rasilimali zake, lakini lengo kuu likabaki kuwa ni kudhibiti maambukizo ya virusi vya corona.

Hivi karibuni, kumeibuka malumbano hasa kwa mataifa ya Afrika kuhusu namna bora ya ushirikiano barani humo na pia kwenye jumuiya za kikanda ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hali inayoweza kufifisha udhibiti wa maambukizo ya virusi hivyo.

Kama inavyoeleweka kwa wengi, mataifa ya Afrika yanatofautiana kwa namna nyingi, kama ilivyo kwa nchi za mabara mengine. Miongoni mwa tofauti hizo ni idadi ya watu na uwezo wa kiuchumi na rasilimali kwa nchi husika.

Ndiyo maana linapokuja suala kama la kuwafungia watu wasitoke nje ikiwa ni moja ya mbinu za kudhibiti maambukizo ya virusi vya corona, nchi hizo zimetekeleza kwa namna tofauti, huku nyingine zikishindwa kufikia hatua hiyo kutokana na sababu zinazowapa nguvu ya kufanya hivyo.

Mtaalamu wa masuala ya ushirikiano wa kimataifa asiyetaka kutajwa gazetini kutokana na nafasi yake katika utumishi wa umma, anasema tofauti za kimitazamo na mikakati ya mataifa ya Afrika havipaswi kuwa sababu ya kuvuruga uhusiano uliodumu kwa miaka mingi sasa.

“Wapo wanaodhani umoja na ushirikiano miongoni mwa nchi za kikanda kama Afrika, unakuwa imara pale tu mnapokuwa na mkakati unaofanana katika kushughulikia kero za umma kama ilivyo sasa kwa corona, hali haipo hivyo duniani kote,” anasema mtaalamu huyo ambaye kitaaluma ni mwadiplomasia.

Anatoa mfano kuwa hata nchi za Ulaya na Marekani waliopo kwenye mazungumzo ya uboreshaji wa uhusiano wa kibiashara, lakini wakikabiliwa na changamoto kadhaa zinazotokana na maambukizo ya virusi vya corona, bado wana ‘makandokando’ yanayoathiri azma nia, lakini wanavumiliana ili kufikia lengo hilo.

“Kwa hiyo Waafrika hawapaswi kugawanywa kwa sababu ya tofauti za mitazamo ama mikakati ya kushughulikia corona, badala yake wajiimarishe kwa kusikilizana na kuheshimu kila kinachofanywa na upande mwingine. Na zaidi ni wakuu wa mataifa na mamlaka za nchi husika kuwasiliana kwa njia sahihi zisizoweka mianya ya utengano na mafarakano,” anasema.

Johnson Mwikabe, mtafiti katika masuala ya diplomasia ya uchumi anasema zipo taarifa nyingi zilizotolewa na viongozi wa mataifa ya Afrika, na hatua kadhaa zinazolenga kudhibiti kasi ya maambukizo hayo, akitoa mfano wa kufungwa kwa mpaka wa Nakonde unaozitenganisha Tanzania na Zambia.

Mtandao wa Lusaka Times ulimkariri Waziri wa Afya wa Zambia, Dk Chitalu Chilufya, aksema Rais Edgar Lungu, wa nchi hiyo aliagiza kufungwa kwa muda mpaka wake kuanzia Mei 11, mwaka huu, ili kutoa fursa kwa utekelezwaji wa mikakati mipya ya kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona.

Kwa upande wa Tanzania, Rais John Magufuli, alishasisitiza msimamo wake wa kutofunga mipaka ya nchi akisema kuna nchi ambazo hazina bandari zinazotegemea mizigo yao kupita kutokea bandari ya Dar es Salaam.

Wakati Zambia ikichukua hatua hiyo itifaki ya nchi za SADC katika kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona inaonyesha kila nchi inaruhusiwa kudhibiti maambukizo hayo kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa na hali halisi ya nchi husika huku usafirishaji wa bidhaa muhimu ukitakiwa kuzingatiwa kwa nchi wananchama.

Ni kutokana na hali hiyo, madereva kadhaa wa Tanzania waliokwama mpakani hao baada ya hatua iliyofikiwa na Zambia, wameelezea kusitikishwa kwao na kwamba wanapata usumbufu na matumizi makubwa ya fedha yaliyo nje ya bajeti zao.

Taarifa za ndani ya Zambia zinadai kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kasi ya kuenea kwa maambukizo ya corona kwenye eneo hilo la mpaka ni vitendo vya ngono vikiwahusisha zaidi madereva wa malori na wanawake wanaofanya biashara ya ngono.

Miongoni mwa madereva hao, Kaijage Method kutokea jijini Dar es Salaam anakaririwa na BBC, hivi karibuni akisema kuwa, walipata taarifa hizo baada ya kukutana na wakala wa uvushaji magari mpakani hapo.

Kwa mujibu wa Kaijage, wakala huyo aliwajulisha kuhusu kuzuiliwa kwa magari kulikotokana na kufungwa kwa mpaka huo na kwamba idadi ya malori yaliyokuwa yakiwasili mpakani hapo kuingia Zambia ama kupita nchini humo kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilikuwa inaongezeka.

Anasema hali hiyo ni tofauti na ilivyo kwenye mpaka wa Kasumbalesa unaozitengenisha Zambia na DRC ambapo inajulikana kwa muda wa madereva kuwapo hapo kwa sababu za kutimiza vigezo kuwa ni siku mbili.

Mbali na hali iliyopo Zambia, wapo viongozi na wanasiasa wa mataifa wengine kama Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na kinara upinzani, Raila Odinga, waliokaririwa kutoa matamko yenye viashiria vya ‘hali kutokuwa nzuri’ kwa ushirikiano wa kikanda katika kuikabili corona.

Mathalani, Rais Ramaphosa aliitisha kikao cha viongozi wa ‘nchi jirani wa Afrika Kusini’ na kusema kilifanyika baada ya kuwasiliana na Mwenyekiti wa SADC, Rais Magufuli, akataka washiriki watume hoja zao kwa njia ya maandishi.

Lakini Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stergomena Lawrence Tax, anasema Rais Magufuli hakupaswa kuhusishwa moja kwa moja na mkutano ulioitishwa na Rais Ramaphosa kwa vile haukuwa ‘umebeba’ ajenda ya jumuiya hiyo.

“Huo ulikuwa mkutano wake binafsi Ramaphosa aliouitisha na kuwashirikisha viongozi wa nchi zilizo jirani na Afrika Kusini,” anasema Dk Tax.

Columnist: www.tanzaniaweb.live