Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Chukueni tahadhari msimu huu wa sikukuu

30624d230cb354d88c431cb000b11a26 Chukueni tahadhari msimu huu wa sikukuu

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZIKIWA zimebaki siku chache Watanzania kuungana na watu wengine duniani kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya, tayari maandalizi na shamra shamra za sikukuu hizo yameanza.

Kila kona ya nchi kumejaa mapambo huku mitaani hususani madukani na masokoni kukiwa na mlundikano wa watu wanaofanya manunuzi mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya sikukuu hizo.

Mara nyingi kipindi kama hiki cha mwishoni mwa mwaka huwa na pilika pilika za hapa na pale ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kuumaliza mwaka unaoisha na kuanza mwaka mwingine mpya.

Pia huwa ni wakati wa familia nyingi kukutana na kusheherekea pamoja hivyo wengine hujikuta wakisafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Ikiwa ni pamoja na maandalizi makubwa katika eneo la chakula na mavazi kwa ajili ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Ukweli ni kwamba kipindi hiki kinahitaji watu kuchukua tahadhari zaidi kuliko kipindi kingine hasa wale wanaosafiri, lakini pia wale wanaoenda kwenye maeneo ya starehe.

Msimu huu watu wengi hujipanga kuhakikisha wanafurahia sikukuu hizo za mwisho wa mwaka hivyo wengine hupenda kusafiri kama familia kwa usafiri binafsi na wengine hutumia usafiri wa umma kwa maana ya mabasi, treni na hata ndege.

Bahati nzuri mwaka huu kutokana na mikakati mizuri ya serikali, eneo la usafiri wa umma limeandaliwa vizuri ambapo pamoja na mabasi pia kuna usafiri wa treni unaotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wa anga wa ndege za Shrika la Ndege Tanzania (ATCL).

Pamoja na ukweli huo, kipindi hiki kwa bahati mbaya kimekuwa ni cha ajali ambazo nyingi zinatokana na uzembe wa madereva ama kwa kutozingatia sheria za barabarani au kutojiandaa vyema kwa maana ya kutoyafanyia uchunguzi mapema magari yao kabla ya safari ndefu.

Hivyo, mamlaka husika kama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) pamoja na polisi zina wajibu wa kujipanga kuhakikisha zinafanya ukaguzi wa magari ya binafsi na ya abiria ili kudhibiti mapema ajali zinazoweza kuepukika.

Lakini pia kipindi hiki hususan kwa mikoa ya Kaskazini kama vile Kilimanjaro na Arusha kimekuwa maarufu kwa kuwa na abiria wengi wanaokwenda likizo katika mikoa hiyo hali inayosababisha kuwapo kwa urasimu wa tiketi.

Kipindi hiki ambacho wenye mabasi hukiita cha mavuno ndio hukitumia kupaisha bei za nauli kuliko kawaida kutokana na wingi wa abiria jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiwaumiza abiria wakati wa kwenda lakini pia pindi wanapomaliza sikukuu hizo na kurejea makwao.

Latra takribani kila mwaka imekuwa ikionya wamiliki wa mabasi ya mikoani kuzingatia taratibu na bei zilizowekwa huku ikisisitiza kuwachukulia hatua wote wanaokiuka.

Pamoja na upande huo wa usafiri pia kipindi hiki tahadhari inahitaji kuchukuliwa katika eneo la wanaoshehekea sikukuu hizo katika maeneo mbalimbali ya starehe zikiwamo kumbi za starehe na fukwe.

Maeneo hayo pia yanahitaji tahadhari kubwa ikiwamo usimamizi makini kuanzia kwa wananchi wenyewe hadi mamlaka husika kama vile wamiliki na polisi ili kuepusha ajali zisizo za lazima kutokana na wingi wa watu.

Pamoja na kwamba ni kipindi cha furaha lakini ni vyema mwananchi mwenyewe akachukua tahadhari kwa kunywa pombe kiasi kwa wanaokunywa hususani anapoendesha gari, kuchukua tahadhari anapokuwa na watoto, kuepuka makundi ya uhalifu kama vile wizi na uchomaji wa matairi pamoja na uvunjifu wowote wa sheria na kubwa zaidi ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka na kuanza mwaka mpya.

Columnist: habarileo.co.tz