Hatima ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kuendelea kushika nafasi hiyo iko njia panda baada ya taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya chama hicho kueleza, amewasilisha barua ya kujiuzulu.
Swali kubwa linalobakia kwa makada wa chama hicho na wafuatiliaji wa masuala ya siasa ni nani atarithi mikoba ya kiongozi huyo.
Chongolo alichaguliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Aprili 30 mwaka juzi, baada ya kupendekezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na kuthibitishwa na Halmashauri Kuu na hadi jana alikuwa amefikisha siku 942 za utumishi wake kwenye wadhifa huo aliorithi kutoka kwa Dk Bashiru Alli.
Barua iliyosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii inaonyesha Chongolo amemwandikia barua Mwenyekiti wake, Rais Samia, akimueleza uamuzi wake wa kujiuzulu akidai kuchafuliwa kupitia mitandao ya kijamii.
Katika barua hiyo ya Novemba 27, mwaka huu, ambayo Mwananchi imeiona mitandaoni, Chongolo amekaririwa akisema hali hiyo imemkumbusha wajibu wa kiongozi kuwajibika kwa masilahi ya chama wakati wote anapotuhumiwa au kuhusishwa na jambo lolote.
Hata hivyo, siyo chama, viongozi wake au Chongolo mwenyewe waliothibitisha kuhusu barua hiyo hali iliyosababisha mjadala kuwa mpana mitandaoni huku akihusishwa na kashfa iliyohusisha ajali ya gari katika daraja la Tanzanite, jijini Dar es Salaam.
Uvumi huo wa kujiuzulu kwa Chongolo ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Njombe, ulishika kasi hasa baada ya jana kutokuonekana katika semina ya mafunzo kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) jijini Dar es Salaam iliyofunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana.
Katika picha zilizotumwa na CCM kwa vyombo vya habari, Chongolo hakuonekana na chanzo chetu kilitudokeza kuwa: “Katibu mkuu hakuhudhuria kwa sababu nimesikia anaumwa. Pia nimesikia sijui alikuwa na wageni ila tetesi ni kwamba ameshindwa kuhudhuria kwa sababu anahudhuriaje na ameshajiuzulu.”
Semina hiyo ya wajumbe walifundishwa mada zinazohusu uongozi na maadili ili kuongeza uwezo na ufanisi kwa viongozi kuwajibika kwa chama na Serikali.
Leo asubuhi kitafanyika kikao cha Kamati Kuu na saa 6 mchana, Halmashauri Kuu itakutana na vikao hivyo vyote vitakuwa chini ya uenyekiti wa Rais Samia.
Chanzo kingine kilidai kuwa Chongolo aliyeteuliwa katika nyadhifa hiyo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu: “Si hiyo inayoonekana mitandaoni na mwenyekiti ameipokea. Sasa hatujui je, amekubali ombi lake ama ataikataa, ila ni kweli ameandika barua."
“Unajua CCM ni chama kikubwa, ni chama dola, haiwezekani barua isambae mitandaoni halafu hakuna kanusho lolote kufanyika, sasa tusubiri kesho (leo) kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu tutajua kwani hakuna uficho tena. Kikubwa kilichotokea kwenye siasa tunasema ni ajali ya kisiasa,” amesema
Mtoa taarifa huyo ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa vikao hivyo vya chama alisema: “Kuna vita kubwa ndani, kuna makundi mengi, mambo mengi yanatajwa tajwa na wanamitandao wanataka mtu wao awe Katibu Mkuu, lakini nasikia mwenyekiti anaweza asimtafute mbadala wake, hadi mwakani ili kupisha joto. Hilo tunasubiri mwenyewe sasa atakavyoamua.”
Mmoja wa mawaziri waliozungumza na gazeti hili alisema, katika barua hiyo lolote linaweza kuwa, inaweza kuwa ukweli au uongo huku akisisitiza: “Mimi mwenyewe nimeshtuka, lakini ukimya huu unatushtua sana, kwa nini kama ni uongo hakuna kanusho? Hebu tusubiri kwani kesho (leo) tutajua kila kitu ila na mimi nasikia sikia kama unavyosikia wewe (akimaanisha mwandishi).”
Wanaotajwa kumrithi
Vyanzo kutoka ndani ya chama hicho, wanatajwa makanda wanaoweza kurithi nafasi hiyo ni waziri wa zamani, Balozi Emmanuel Nchimbi, Wakuu wa Mikoa, Amos Makalla wa Mwanza na Martin Shigella wa Geita.
Pia, washauri wa Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Abdallah Bulembo ambaye amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi na William Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani na waziri mwandamizi mstaafu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema kulikuwa na utabiri kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kile kilichokuwa kikiendelea ndani kwa ndani.
Mwanazuoni huyo alieleza anadhani kuna sababu nyingine mbali na hiyo aliyoeleza kwenye barua yake kwani kuna wengi wanachafuliwa lakini bado wapo kwenye uongozi, pia, alisema hajafanya kosa kubwa la kumsukuma kujiuzulu, bali kuna msukumo ndani ya chama.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kakobe alisema katika siasa lolote linaweza kutokea huku akisema anasubiri kikao cha halmashauri kuu ndicho kitakachotao majibu sahihi.
“Bado sijaamini kama hii barua ni kweli, nilitarajia mamlaka itoe ufafanuzi, lakini wa sababu kesho (leo) kuna kikao pamoja na mambo mengi hili litazungumzwa kama ni kweli au la. Tusubiri mamlaka ituambie kama ni kweli au hapo nitakuwa na mengi ya kuzungumza.
“Hadi sasa hatujasikia mamlaka ikitoka hadharani kusema kama amejiuzulu au, kesho (leo) tutajua kama ni kweli au… Maana hata mimi nimeona hiyo barua mtandaoni,” amesema Dk Kakobe.