Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Chanjo ya Uviko 19 ni bora kuliko tiba

Ed3ec25d9c547c137d8a75f6dfc6e35b.jpeg Chanjo ya Uviko 19 ni bora kuliko tiba

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“WATU wanaitikia vizuri wito wa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (uviko 19),” anasema Mganga mkuu wa hospitali ya Mwananyamala mkoani Dar es Salaam, Dk Zavery Benela alipozunguimza na gazeti hili.

“Hii chanjo ya ni salama. Mpaka sasa hatujapata mtu aliyepata tatizo lolote kutokana na chanjo hii,” anaongeza.

Dk Benela anasema siku ya kwanza ya kutoa chanjo hiyo walichanja watu 220 wenye vigezo vilivyoanishwa na Serikali. Siku iliyofuata hadi gazeti hili linaondoka maeneo hayo watu zaidi ya 220 tayari walikuwa wamepata chanjo na wengine wakiendelea kufika hospitali hiyo yenye hadhi ya rufaa kwa ajili ya kupata chanjo hiyo.

Dk Benela anasema kutokana na umuhimu wa chanjo hiyo, hospitali hiyo ya Mwananyala imeteua maofisa maalumu wenye uzoefu wa kutoa chanjo ili kuhakikisha watu waonaofika katika hospitalini hapo wanapata chanjo hiyo kwa njia salama.

Pelagia Baturulimi anayechoma chanjo hiyo anasema kutokana na uzoefu wake wa kuchoma chanjo mbalimbali, chanjo ya Uviko haina tofauti na chanjo nyingine.

Mganga mkuu wa hospitali hiyo anafafanua kuhusu chanjo hiyo akisema kwamba ni dawa ya kibaolojia ambayo inajenga kingamwili dhidi ya virusi vinavyosababisha Uviko-19, kama zilivyo chanjo nyingine.

Anasema kwamba chanjo hiyo inapoingizwa katika mwili, mfumo wa kinga unaanza kutegeneza kinga dhidi ya ugojwa huo. Anasema chanjo ni njia bora zaidi kuzuia magonjwa ya kuambukiza, hivyo basi chanjo ya Uviko 19 ni sawa na chanjo nyingine zinazokinga mwili wa mwanadamu dhidi ya magonjwa.

Kwa mfano kinga inayoenea kutokana na chanjo kwa kiasi kikubwa inawezesha kuepukana na kifua kikuu duniani na chanjo kinga nyingine za magonjwa kama vile polio, pepopunda, tetekuwanga nakadhalika, Anasema Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) inafuatilia kwa ukaribu zaidi watu wanaopata chanjo ya uviko 19. Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma Bi. Gaudensia Simwanza anasema fomu ya Mamlaka hiyo inayojazwa baada ya chanjo ni kufuatilia maendeleo ya watu wanaopata chanjo hiyo.

Anasema mtu yeyote atakayepata tatizo lolote atoe taarifa kituo cha afya kilicho karibu au alipopata chanjo hiyo au apige simu Na. 0800110084 ambayo ni namba maalum ya mamlaka hayo.

Timothi Nkondola (81) anayesumbuliwa na shinikizo la damu anasema amepata chanjo hiyo akiwa kwenye kiti cha magurudumu anaielezea chanjo hiyo kuwa itamuwezesha kuendelea na matibabu ya shinikizo la damu na sukari bila hofu ya maambukizo ya uviko-19.

Nkondola anawatoa khofu waoitilia shaka chanjo hiyo kuwa ni chanjo sahihi itakayowaezesha kuishi bila maambukizo ya ugonjwa huo hatari unaoangamiza watu duniani.

Dk Rehema Mtoi mmoja wa Madaktari wanaoendesha zoezi hilo la chanjo ya Uviko 19 katika hospitali hiyo ya Mwananyamala anawataka watu wote wenye vigezo kupata chanjo hiyo haraka, anasema iwapo watu hawatapata chanjo madaktari wanaweza kupata wakati mgumu wa kutoa matibabu ya uviko 19 ingawa chanjo hiyo ni hiari ya mtu mwenyewe.

Yeye kama mtaalamu wa magonjwa anatoa ushauri kwa watu kupata chanjo hiyo ili kujikinga na ugonjwa huo unaoteketeza maisha watu duniani kwani kinga ni bora kuliko tiba.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya anasema hadi sasa hakuna mtu nchini aliyechomwa chanjo ya kinga ya corona na kukutwa na tatizo la kuganda damu au jingine lolote.

Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Profesa Mgaya alisema tukio la kuganda damu hutokea mara chache sana na hata Marekani ambako inasemekana kulikuwa na watu waliokutwa na changamoto hiyo ilikuwa ni watu wanne kati ya watu milioni moja.

Akizungumza katika kipindi maalumu kuhusu chanjo ya corona kilichorushwa na chaneli ya TBC1 ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Profesa anasema chanjo inayochomwa nchini ya Johnson & Johnson ni salama na kama kuna changamoto baada ya kuchanjwa ni za kawaida.

“Hakuna taarifa za watu kudhurika kwa kiasi cha kupoteza maisha au kuganda damu ila ifahamike kuwa kama kuna changamoto ni zile za kawaida zinazoweza kutofautisha mtu na mtu. Mfano mimi nilichanjwa lakini sikusikia kichefuchefu kama wengine wala sikupata maumivu ya kichwa ila niliumwa kidogo mkono na kesho yake nikawa salama kabisa,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema chanjo zinazotolewa nchini zilipimwa kwanza na zimethibitishwa zina ubora, hivyo changamoto ndogo za kawaida zisisababishe mtu aamue kutochanjwa.

“Chanjo siyo dawa ndugu zangu, ni kinga sasa mhakikishe kuwa mnachanja mapema Watanzania na siyo kungojea kupata ugonjwa huo na ndiyo kuanza kutafuta chanjo hivyo nawasihi watu wakachanje sasa na kisha kuendelea kuchukua tahadhari zinazotakiwa,” anasema Profesa Mgaya.

Daktari Bingwa wa Mapafu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Pauline Chale anasema dhana ya kuwa chanjo ya corona

si salama haina nguvu kwa sasa kwani hata madaktari wanachanja chanjo hiyo ya Johnson & Johnson.

Dk Chale anasema wanaokataa kuchanja watajikuta wakiingia kwenye gharama zaidi hasa watakapoumwa na kulazimika kulazwa.

“Najua wapo watu ambao wanaodhania wakiumwa Uviko-19 ndiyo wataenda kuchanjwa hii siyo sawa kwa kuwa mtu akiumwa anapaswa kutochanjwa hadi akipona kabisa,” anasema na kuongeza:

“Hivyo mwende kuchanja sasa hivi kwani itazuia au hata kupunguza nguvu ya ugonjwa kuingia mwilini, mimi nimefanya kazi muda mrefu kwenye huduma za mapafu ninajua hali inavyokuwa mbaya kwa mtu akipatwa na tatizo la kupumua, ndugu zangu mkachanje.”

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe anasema suala la ugonjwa wa Uviko-19 si la wizara hiyo pekee, hivyo kama kuna dosari zikiwamo tuhuma za

rushwa kwenye utoaji chanjo wananchi watoe taarifa.

“Taarifa za wahudumu wa afya kuchukua rushwa wakati wa utoaji chanjo hatujazipata, lakini cha msingi suala la uviko-19 siyo la wizara ya afya pekee, ni la kila mtu, idara, taasisi na wizara mbalimbali,” anasema.

Anaongeza: “Pia wananchi watambue kuwa chanjo hii ni bure, hivyo kutoa rushwa siyo tu kujinyima haki yako ya msingi, bali utakuwa unatenda kosa la kutoa rushwa.”

Anasema mikoa yote nchini imepokea chanjo ya uviko-19 na kwamba kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kupata kinga hiyo.

“Wizara kupitia MSD (Bohari ya Dawa) ilifanya usambazaji wa chanjo za Uviko-19 na vifaa katika mikoa yote nchini na mpaka jana (Agosti 3), mikoa yote 26 nchini ilikuwa imepokea chanjo.”

Alisema kazi ya kutoa chanjo ni endelevu hadi wananchi zaidi ya asilimia 60 watakapochanwa.

“Wizara pamoja wadau wote yakiwamo mashirika, NGO na makundi binafsi mbalimbali na mtu mmoja mmoja, wanaendelea kutoa elimu ya chanjo katika makundi mbalimbali na ngazi tofauti nchini,” alisema Dk Sichalwe.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shedrack Mwaibambe aliwataka watumishi wa afya wenye tabia ya kuomba rushwa kwa wananchi wanaokwenda kupata chanjo waache mara moja.

Mamia ya wananchi wanaendelea kupata chanjo hiyo kwenye mikoa yote nchini.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi alisema mwitikio wa watu kupata chanjo ni mkubwa.

“Tulipewa jukumu la kutoa chanjo kwa viongozi wastaafu, waliopo kazini na kwa wananchi wa kawaida ambao wamejisajili mtandaoni na tukiangalia mwitikio ni mkubwa jana (juzi) walikuwa watu 250 lakini leo namba ni kubwa zaidi imejitokeza.”

“Utaratibu ni kwamba wakifika tunatoa elimu kuhusu covid-19 ni kitu gani, chanjo imepatikanaje, hali ilivyo kwa sasa duniani, wangapi wanapata chanjo, bara la Afrika limepata chanjo kiasi gani, madhara ya chanjo na faida za chanjo, baada ya kufanya hayo yote tunaruhusu maswali,” alisema.

Alisema chanjo ni kitu bora na imesaidia wengi na kwamba kuna chanjo 9 zinazokinga magonwa 13.

“Chanjo ya Johnson uhifadhi wake ni rahisi kwenye friji ya kawaida na inafaa kwa mazingira yetu, kwenye friji inakaa miezi minne na nusu muhimu tuendelee kumuomba Mungu kila mtu kwa imani yake na tuchukue tahadhari za kiafya,” alisema Profesa Janabi.

Columnist: www.habarileo.co.tz