Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Chama la Wana warudi na moto

Chama La Wana Chama la Wana warudi na moto

Mon, 15 May 2023 Chanzo: mwaspoti

Unaikumbuka Stand United ‘Chama la Wana’, namna hata mashabiki wake walivyokuwa wanafunga baadhi ya mitaa mjini Shinyanga wakati timu hiyo inacheza mechi mbalimbali, ilikuwa ni amsha amsha ya kutosha kuanzia asubuhi hadi jioni haikuwa kazi rahisi kuzima mziki wa masela hao.

Siku hiyo stendi kuu ya mabasi ya pale mkoani na ile ya wilaya shughuli ilisimama masela hao watacheza na vingoma vyao kisha jioni mabasi yanawapakia na kwenda Uwanja wa CCM Kambarage kuipa sapoti timu yao.

Ilikuwa ni shangwe la kutosha hawa jamaa walikuwa wanashangilia mwanzo mwisho timu ngeni inayokuja kucheza nayo ilikuwa na kazi nzito ya kufanya kwa sababu hawa masela walikuwa hawachoki kushangilia huku kichwani ikionekana wameishakunywa bia za kutosha.

Usidhani vibe hilo linafanyika nyumbani pekee kwani hata mechi za ugenini walikuwa wakitimba huku wakipewa sapoti na masela wenzao wa vituo vya mabasi vya mkoa husika walipokwenda kucheza mechi hiyo.

Lakini ghafla msimu wa 2018/19 timu hiyo ilishuka ligi kuu na mambo yakaanza kuwa mabaya kwao, migogoro ikaanza kuiandama klabu hiyo na ikashuka kutoka daraja la kwanza (Championship) hadi Ligi ya Mkoa wa Shinyanga na ikabaki historia pekee.

Sasa wadau na mashabiki wa soka waliokuwa na mapenzi na timu hiyo wameanza mikakati mizito ya kuhakikisha timu hiyo inarudisha heshima yake waliitoa mkoani ilipokuwa inashiriki ligi ya mkoa wakaipandisha hadi Championship ambapo itashiriki msimu ujao.

MKAKATI WAO UKO HIVI

Katibu msaidizi ambaye pia ni mratibu wa timu hiyo, Fred Masai anasema wakati wanaamua kurudi upya walijiwekea malengo manne ambayo ni kutwaa ubingwa wa mkoa, kucheza First League na kupanda Championship na baada ya hapo wapambane ili kupanda Ligi Kuu.

Anasema ndoto yao kubwa ni kutaka kurejesha heshima ya klabu hiyo ambayo iliipata miaka tisa iliyopita ambapo anaamini kwa ushirikiano wa wadau,mashabiki na wao viongozi watafanikisha malengo yao ambayo ni kupanda Ligi Kuu.

“Kwanza tuwashukuru mashabiki wetu ile hamasa ya 2014 imeanza kurudi, jukumu letu ni kuhakikisha hii timu inafanya vizuri tulishuka hadi mkoani lakini sasa tumeanza kuona mafanikio baada ya kupanda hadi Championship,” anasema Masai.

Masai ambaye yuko na timu hiyo takribani miaka nane anasema wamepambana sana kuifikisha timu hiyo hapo ilipo lakini anaona bado wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanafanya vizuri na kupanda daraja.

Kuhusu kocha wao Ally Mngazija, katibu huyo anasema bado wanamhitaji hivyo msimu ujao atakuwepo kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mashindano ya Championship hivyo hawana mpango wa kutafuta mwalimu mwingine.

“Mngazija ni kocha mzuri tuko naye toka kwenye ligi ya mkoa na ametupandisha hapa tulipo hivyo tutakuwa naye msimu ujao ni bonge la kocha huyu naamini atatusaidia sana,” anasema Katibu huyo.

WANARUDI KAMBARAGE

Stand United ilikuwa inatumia Uwanja wa Mwadui Complex kwenye michezo yake ya First League ambao uko wilayani Kishapu lakini sasa wamepanga msimu ujao kurudi Shinyanga mjini Uwanja wa CCM Kambarage ambao waliutumia miaka ya nyuma kwenye harakati zake za kupanda daraja.

Masai anafafanua kuwa lengo la kutaka kupeleka mechi zao Uwanja wa Kambarage ni kuwapa nafasi mashabiki wa soka Shinyanga kutazama michezo yao kutokana na Mwadui Complex kuwa mbali na mjini hivyo uwalazima kusafiri takribani kilometa 50.

“Mpango wetu msimu ujao wa Championship kutumia Uwanja wa Kambarage ambao utawapa nafasi kubwa mashabiki wetu kuja kutupa hamasa kwenye michezo mbalimbali ambayo tutacheza hapa nyumbani unajua kule Mwadui Complex ni mbali sana,’’ anasema.

MNGAZIJA AFUNGUKA

Anasema atakuwa na furaha siku akiona timu hiyo imerejea Ligi Kuu hivyo atapambana sana kuhakikisha mkakati huo unakamilika ambapo anaamini kwa ushirikiano wa wachezaji,uongozi na mashabiki lengo hilo litakamilika.

“Kikubwa ni kufanya maandalizi mapema, tunatakiwa kusajili wachezaji wapya ambao wataongeza nguvu unajua Championship ni mashindano magumu sana yanahitaji matokeo kuliko kitu kingine hivyo ni lazima uwe na kikosi bora,’’ anasema Mngazija na kuongeza;

“Kikosi nilichonacho si kibaya kina wachezaji wazuri lakini inahitajika nisajili, nitaandaa ripoti yangu ambayo itaweka kila kitu kwangu natamani sana kuona Stand United inarejea Ligi Kuu.’’

NAHODHA HUYU HAPA

Nahodha wa timu hiyo, Ismail Salehe anasema wao wachezaji wanajua kazi kubwa waliyokuwa nayo ni kuhakikisha wanakomaa ili kufanya vizuri kwenye Championship na kupanda daraja hivyo watajiandaa vya kutosha ili wawe fiti.

“Tutapambana tunajua mashabiki wetu wanatamani kuona Stand United inacheza Ligi Kuu hivyo lazima kwetu tukomae sana ili tufanye vizuri Championship,’’ anasema Salehe.

Columnist: mwaspoti