Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Chama la Wakongo mziki wake Yanga si mchezo!

Mayele X Lomalisa Mayele wakipongezana na Lomalisa

Thu, 9 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Simba wameanza kuliimba jina la straika mpya wa timu hiyo kutoka DR Congo, Jean Baleke baada ya kufunga mabao mawili katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Straika huyo amekuwa mchezaji wa nne kwa miaka ya karibuni kutoka nchini humo kukipiga Simba, akitanguliwa na Deo Kanda, Chris Mugalu anayecheza kwa sasa Irak na Henock Inonga.

Licha ya wachezaji hao kukipiga Simba rekodi zinaonyesha mastaa wengi kutoka nchi hiyo wamekuwa wakikimbilia na kukipiga Yanga kuliko klabu nyingine yoyote nchini.

Sio kwa wachezaji tu, hata makocha kutoka DR Congo wamekuwa wakiinoa Yanga kwa mafanikio, kiasi kwamba ni ngumu kuitenganisha na DR Congo katika ulimwengu wa soka. Rekodi zinaonyesha Wakongo na Yanga hawajaanza hivi karibuni baada ya ujio wa kina Fiston Mayele, Mukoko Tonombe na Yannick Bangala, bali ulianza miaka ya 1970.

Mwanaspoti linakuletea kikosi cha nyota 11 sambamba na wachezaji wa akiba na makocha kutoka DR Congo waliowahi kukipiga au wanaendelea kuichezea Yanga katika kuthibitisha kuwa, klabu hiyo ya Jangwani na Wakongoman ni damudamu na kama hujui orodha ya wachezaji waliowahi kuichezea Yanga tangu miaka ya 1970 hadi sasa unaunda vikosi viwili pamoja na makocha wao. Tiririka nayo...!

DOYE MOKE/ KLAUS KINDOKI

Tuanzie langoni. Achana na Klaus Kindoki aliyesajiliwa misimu mitatu iliyopita na kuchemsha, Yanga imewahi kuwa na kipa mahiri kutoka DR Congo, Doye Moke.

Kipa huyo ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara anayefanya shughuli zake kati ya Tanzania na nchi jirani za Zambia na DR Congo, aling’ara miaka ya 1990 kabla ya kuhamia Simba na baadaye Majimaji Songea na kote huko alipata mafanikio.

Bado anakuwa kipa Mkongo aliyefanya vyema ukiacha mbwembwe zake ikiwamo kupenda kuvaa msongo kichwani.

DJUMA SHAABAN

Ndiye beki wa kulia wa sasa wa Yanga akiwa anacheza kwa msimu wa pili mfululizo akitokea AS Vita ya DR Congo.

Kwa kizazi cha sasa, Djuma ni beki wa shughuli, japo ni kama amepunguza makali kulinganisha na alipokuwa AS Vita kiasi cha kuzitoa udenda Simba na Yanga na kuanzisha vita ya kuisaka saini yake na hatimaye Yanga kumnasa msimu uliopita na kuwa mmoja ya walioipa mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la ASFC na Ngao ya Jamii waliyoibeba misimu miwili ikiwamo ya msimu huu, zote wakiizidi akili Simba.

Djuma ni beki anayegombea namna sambamba na beki kiraka mzawa Kibwana Shomary ambaye pia anamudu kushoto.

JOYCE LOMALISA

Huyu ni beki wa kushoto aliyetua Jangwani msimu huu akitokea klabu ya FC Onze Bravos do Maquis ya Angola. Mwanzoni alichukuliwa kawaida, pengine alisajiliwa akitokea kwenye majeraha, lakini kwa sasa moto wake ni balaa kiasi wale waliokuwa wakimbeza wameamua kumkaushia kwa soka analopiga hasa kupandisha timu na kupiga krosi zenye macho zilizoibeba Yanga.

Beki huyo anabadilishana namba na nyota wengine kushoto, wakati mwingine na Kibwana. Pia kuna wakati anapishana na David Brayson na winga Farid Mussa ambaye kocha Nasreddine huwa anamtumia tangu msimu uliopita.

BANZA TSHIKALA/ YANNICK BANGALA

Kwa beki wa kati anayesimama kama namba nne, kama unataka kupanga kikosi cha Wakongo basi kuwa na machaguo mawili. Unaweza kuanza na Banza Tshikala, moja ya mabeki wa kati waliokuwa wamejaliwa miili iliyoshiba na mtu wa shughuli kwelikweli.

Beki huyo kwa sasa ni mchungaji akiendesha kanisa la kilokole lililopo Tegeta. Enzi zake alikuwa beki haswa aliyesimama sambamba na wazawa Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ au Willy Martin ‘Gari Kubwa’ ambao nao walijaliwa miili mikubwa kipindi hicho wakicheza miaka ya 1990.

Kama utaona vipi, bado una chaguo la kumtumia Yannick Bangala anayekipiga ndani ya kikosi hicho tangu msimu uliopita baada ya kusajiliwa kutoka FAR Rabat ya Morocco.

Bangala ni kati ya wachezaji muhimu wa Yanga akimudu kucheza pia kiungo mkabaji kwa usahihi na ndiye aliyechangia kumuweka nje nahodha Bakar Mwamnyeto aliyekuwa akicheza sambamba na Dickson Job. Bangala na Job ndio wamejihakikishia namba kwenye eneo hilo la kati.

CONSTANTINE KIMANDA

Ni mmoja wa mabeki waliotamba miaka ya 1990 akiwa na Yanga unaweza kumsimamisha kama beki wa kati na mambo yakaenda freshi. Kimanda ni mmoja wa wachezaji wa Kikongo aliyeitungua Simba kwenye mechi za watani nchini. Pia ni mmoja wa mabeki waliokuwa makini katika kuosha mipira kwa kutumia akili, huku akiwakaba vyema washambuliaji wasumbufu. Sifa yake nyingine ilikuwa ni uwezo wa kupiga friikikii za kiufundi.

Mkongo huyo alidumu na Yanga kwa misimu zaidi ya mitatu kabla ya kusepa kurudi kwao akiwa ameacha alama kubwa.

MUKOKO TONOMBE/ PAPY TSHISHIMBI

Utasema nini juu ya kiungo huyo wa kati, Tonombe Mukoko aliyeng’ara na kuibeba Yanga msimu wa 2020-2021 kabla ya kuchemsha uliofuata baada ya ujio wa Bangala kiasi cha kutolewa kwa mkopo TP Mazembe kupishana na Chicco Ushindi. Mukoko alikuwa kiungo mkabaji aliyejua kuwadhibiti wapinzani, yaani alikuwa mkata umeme kweli na alisaidia kuipandisha timu mbele kwa kuanzisha mashambulizi yenye akili na pia alikuwa akifunga mabao.

Hadi anaondoka Yanga alikuwa Mchezaji Bora wa kikosi hicho, akiwa pia amefunga mabao manne yakiwamo matatu ya msimu wa 2020-2021 na moja la 2021-2022 mbali na mabao ya Kombe la ASFC yaliyoiwezesha kufika fainali msimu wa 2020-2021 na kufungwa na Simba mjini Kigoma, huku akilimwa kadi nyekundu iliyochangia kumuondoa kikosini.

Kama unaona Mukoko hakufai basi unaweza kumpanga Papy Tshishimbi aliyesajiliwa misimu minne iliyopita akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini na kutamba msimu wa 2017-2018 hadi mwaka 2020 alipoachwa na kurudi kwao.

Kwa sasa kiungo huyo anakipiga Ihefu iliyopo Ligi Kuu Bara baada ya kutamba msimu uliopita na klabu ya Ligi ya Championship, Kitayosce. Unaweza kumpa nafasi ya kiungo mkabaji akawasha freshi.

TUISILA KISINDA/ JESUS MOLOKO

Utasema nini juu ya Tuisila Kisinda ‘TK Master’ katika msimu wake wa kwanza Yanga. Alikuwa ana kasi, chenga na kupiga krosi zilizoibeba Yanga katika Ligi Kuu Bara na ASFC, akikumbukwa zaidi penalti aliyosababisha kwenye Kariakoo Derby akimburuza Joash Onyango.

Baadaye aliuzwa RS Berkane ya Morocco na kutwaa nayo Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya Yanga msimu huu kumrejesha, lakini akiwa kapungua makali. Ukitaka unaweza kumuanzisha winga ya kulia na kama utaona vipi, mbadala wake aliyesajiliwa msimu uliopita wakati TK akiuzwa, yaani Jesus Ducapel Moloko naye ni fundi haswa kwenye wingi hiyo sambamba na ile ya kushoto.

SAMMY BITUMBA | LAURENT KABANDA

Katika kiungo cha kati, Yanga ya Wakongo unaweza kumuanzia Sam Bitumba Iyela, mmoja wa viungo waliotamba miaka ya 1990 akija kikosini na straika Nonda Shaaban ‘Papii’. Alikuwa fundi haswa akiiunganisha timu na pia kupiga pasi zenye macho kabla ya kutimkia Afrika Kusini.

Kama huyo unaona sio, bado unaweza kumpanga Laurent Kabamba fundi mwingine aliyetamba na Yanga miaka ya 2000 kabla ya kurudi kwao na kukipiga TP Mazembe. Uwezo wake wa kumiliki mpira na kuchezesha timu ulimpa jina kubwa Jangwani.

FISTON MAYELE/ HERITIER MAKAMBO

Linapokuja suala la straika wa Kikongo wa kumpanga kama namba tisa unaweza kubabaika kwani Fiston Mayele anayeichezea Yanga kwa msimu wa pili mfululizo ni balaa kizazi cha sasa. Anatumia nguvu na akili kuibeba Yanga inayoongoza msimamo ikitaka kutetea taji la Ligi Kuu msimu wa pili mfululizo.

Ndiye kinara wa mabao wa Yanga kwa misimu hiyo - msimu uliopita alifunga mabao 16 na kushika nafasi ya pili nyuma ya George Mpole aliyekuwa Geita Gold. Kwa msimu huu hadi sasa amefunga mabao 15 akiwa kinara akiwaacha mbali wanaomfukuzia.

Hata hivyo kabla yake kuna mwamba mwingine, Heritier Makambo alijitengenezea ufalme msimu wa 2018-2019 akifunga mabao 17 na kuwa mchezaji wa Kikongo kuwahi kufunga mabao mengi kwa miaka ya karibuni kwa wageni waliokipiga Yanga, japo Mayele alikaribia kuifikia msimu uliopita na akiwa na nafasi kuivunja msimu huu.

Baada ya msimu huo alinunuliwa na AC Horoya ya Guinea alikoshindwa kuonyesha makali kabla ya msimu uliopita kurejeshwa na kushindwa kuonyesha makali akifunga bao moja na manne ya Kombe la ASFC ambayo Yanga ilibeba taji kwa kuitungua Coastal Union katika fainali. Msimu huu ameshindwa kumsaidia Mayele na kutemwa katika dirisha dogo. Ameondoka akiwa bado anakumbukwa kwa staili yake ya kuwajaza.

DAVID MOLINGA/ NONDA SHAABAN

Katika eneo la mshambuliaji namba mbili, una machaguo mawili. Kwa kizazi cha sasa unaweza kumuanzisha David Molinga ‘Falcao’ a.k.a Ndama mshambuliaji aliyekuwa na mwili mkubwa.

Ukimwangalia mwili aliokuwa nao alionekana mzito, lakini uwanjani aliifanya kazi kwa ufanisi kwani kabla ya ujio wa Mayele hakuna aliyefunga mabao mengi kama yeye kwa misimu miwili mfululizo iliyopita. Molinga aliyeichezea Namungo msimu uliopita aliondoka Yanga kama mfungaji bora 2019-2020 akifunga mabao 11.

Lakini kama unaona Molinga hakufai, una chaguo la kumtumia Nonda Shabaan ‘Papii’. Jamaa alijaliwa mwili mkubwa kama Mayele na Molinga na alikuwa mahiri miaka ya 1990 akicheza kwa muda mfupi kabla ya kwenda Afrika Kusini na baadaye barani Ulaya na kufikia hatua ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alianza kukipiga Uswisi kabla ya kwenda Ufaransa, Italia na baadaye Uingereza. Ni uamuzi wako kumuanzisha Molinga kisha Nonda akaanzia benchi au akaanza Papii na kumweka Molinga nje, japo Nonda alikuwa balaa zaidi.

MAYAULA MAYONI/ PATRICK KATARAY

Kwenye winga ya kushoto una hiyari ya kumtumia nani katika kikosi cha Wakongomani, kwani kwa kizazi cha miaka 1970-1980 unaweza kumuanzisha Fredy Mayaula Mayoni, nyota aliyetamba na timu ya taifa ya nchi hiyo enzi ikiitwa Zaire kabla ya kucheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji. Kwa mashabiki wa soka nchini wanamkumbuka kwa umahiri wake kwenye muziki, kwani alipokuwa Ulaya aliamua kujifunza muziki hasa kutunga na kupiga magitaa na kugeukia muziki na kutamba na ngoma kama Cherie Bondowe, Mbongou na Nabari Misere. Ndiye mchezaji wa kwanza wa Kikongo kufunga bao katika Kariakoo Derby, akifanya hivyo katika nusu fainali ya Kombe la Karume 1970 alipofunga mara mbili na kuizamisha Simba kwa mabao 2-1.

Bao la kufutia machozi la Simba liliwekwa kimiani na kiungo Rashid Gumbo. Kwa kizazi cha 2010 unaweza kumuanzisha Patrick Kataray aliyetamba na Yanga na kwa kizazi cha sasa unaweza kumpa shavu Ushindi aliyesajiliwa msimu uliopita akipishana na Mukoko Tonombe katika klabu ya TP Mazembe, japo hakutamba sana kwani alifunga mabao mawili tu na kutemwa mwanzoni mwa msimu huu kupisha majembe mengine ya Kikongo.

AKIBA:

Kama utakipanga kikosi chako kwa wachezaji hao wa juu, bado kuna nyota wengine wa akiba wanaoweza kuwasha moto kama wale utakaowaanzisha ukianzai kwa kipa Sadick Kalokola aliyewahi kukipiga pia Pan Africans.

Pia kuna Pitchou Kongo mmoja ya wachezaji waliowahi kufunga pia kwenye Kariakoo Derby, aliyesumbua sana miaka ya katikati ya 2000 kwa soka lake lake kiasi cha kuimbwa hadi ha African Stars ‘Twanga Pepeta’ kupitia kwa rapa, Ige Muyaba.

Wengine ni Delo Ntumba, Nebboh Bukumbi, Aime Lukunku, Chicco Ushindi na Alou Kiwanuka.

MAKOCHA

Kwa upande wa makocha unaweza kuwa na machaguo mengi, kwani Yanga imekuwa na bahati ya kufundishwa kwa mafanikio na makocha kutoka DR Congo akiwemo Tambwe Leya aliyeinoa kwa vipindi tofauti miaka ya 1970 na kisha kurudi tena katikati ya miaka ya 1990.

Kocha huyo kwa sasa ni marehemu, lakini ameacha alama kubwa ndani ya Yanga ikiwamo kutajwa kwenye mgogoro wa mwaka 1975 ulioivunja timu hiyo na kuzaliwa kwa Pan African na kurudi tena mwaka 1994 na kuibuka mgogoro ulioigawanya Yanga katika makundi ya Asili na Kampuni na kuja kufukuza wachezaji karibu wote wa kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa 1975.

Pia unaweza kumpa nafasi Raoul Pierre Shungu aliyeipokea timu katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 na kukaa nao hadi mwaka 2001 akiipa ubingwa wa Bara.

Kocha mwingine anayeweza kusimama miongoni mwa makocha wa Kikongo kuinoa Yanga ni Jean Polycarpe Bonganya aliyedumu kwa muda mchache na kutimuliwa klabuni kikatili na wanachama kwa kumfungia kufuli uwanja wa Kaunda mwaka 2008.

Kwa hivi karibuni bado kuna kocha mwingine fundi, Mwinyi Zahera aliyempokea Mzambia George Lwandamina na kwa sasa anainoa Polisi Tanzania baada ya kuachana na Yanga iliyomrejesha na kumpa ukurugenzi wa soka la vijana klabuni hapo.

Columnist: Mwanaspoti