Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

CCM kunani kwenye kupambana na CORONA?

Gwajima Polepole Humphery Polepole na Josephat Gwajima

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna kosa kubwa wanalofanya wabunge wa CCM, wanaokinzana na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu chanjo ya Covid-19. Kosa hilo limechambuliwa kifalsafa na mtaalamu wa sayansi ya fikra, Robert Greene, kupitia kitabu chake “The 48 Laws of Power” – “Sheria 48 za Nguvu”.

Katika sheria hizo 48, Greene aliandika sheria namba moja “Never Outshine Your Master” – “Kamwe using’are kuliko bosi wako”. Greene alichambua kuwa ni kosa kubwa kujipambanua kuwa na uwezo mkubwa kuliko bosi wako. Sheria hiyo imekuwa mwongozo wa fikra kwa kila mtu mbele ya bosi wake.

Bosi anaweza kukupenda sana, lakini haimaanishi ukijipambanua kwamba unajua kuliko yeye, atakuchekea. Mtu ambaye hujitambua kuwa yeye ndiye namba moja, akitokea yeyote anayejionesha kuwa hodari zaidi, humchukulia kuwa amemdhalilisha.

Rais Samia anapigia chapuo chanjo ya Covid-19, wabunge wawili; Josephat Gwajima na Humphrey Polepole wanasema kwa msisitizo kwamba hawatachanjwa. Wanataka kuvuna nini?

Gwajima na Polepole wangeweza kunyamaza na wasingepungukiwa chochote. Kutokeza hadharani kupinga chanjo ambayo inahamasishwa na Rais Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa chama chao, CCM, kwa namna yoyote ni dhahiri wanajaribu kujipambanua kuwa wao wanajua zaidi.

Je, shabaha yao ni kutaka Watanzania waone Rais Samia ameruhusu chanjo bila kufikiri vizuri? Kwanini wamvimbie mwenyekiti wa chama chao? Wanajaribu kujenga picha kwamba ndani ya CCM si shwari, kila mtu anazungumza lake? Mwenyekiti akisema twende kulia, mwanachama akapaza sauti kuwa uelekeo wake ni kushoto, huo sio uasi kwenye chama?

Oscar Kambona alikuwa rafiki wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tena, Nyerere alikuwa mpambe wa bwana harusi, siku Kambona alipofunga ndoa na mkewe, Flora Moriyo. Nyerere aliposimama na Azimio la Arusha, huku Kambona akipinga, urafiki uliisha. Unategemea nini Rais Samia anahamasisha chanjo, wabunge wa chama chake wampinge?

Rais Samia aliingia madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake, Dk John Magufuli. Hakuna wakati wowote Samia alisimama kupingana na kauli ya bosi wake. Inawezekana Samia hakukubaliana na msimamo wa Magufuli kuhusu Covid-19 na chanjo, ila alinyamaza. Maana kupingana na Rais inatakiwa uende pembeni.

Hata ukimweka kando Samia, msimamo wa Rais Magufuli kuhusu Covid-19, pengine haukuwafurahisha wabunge wengi CCM. Hata hivyo, walikaa kimya. Wengine ndio hao wanachangamkia chanjo hivi sasa.

Ukivuka mpaka unaweza kuwaita wanafiki. Binafsi nawaita watunza maadili. Kwa maana, wangesimama na kutambulisha msimamo wao ulio kinyume na mwenyekiti wao, wangepaswa kuondoka.

Othman Masoud Othman alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Akiwa kwenye nafasi hiyo, alitofautiana mtazamo na bosi wake, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Haikuchukua muda, Rais Shein alimfukuza kazi. Othman akaondoka, akajiunga na CUF, sasa ACT. Leo, Othman ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar.

Wabunge CCM wanaoona wanajua kuliko Rais Samia, ama wakae kimya kama wameshindwa kupenyeza ushawishi wao ndani kwa ndani au wahame kuliko kukinzana na mwenyekiti wao waziwazi.

Mwishoni mwa Karne ya 16, ilikuwa mwaka 1591. Aliyekuwa Mfalme wa Japan, Hideyoshi, alimpenda sana mshauri wake aliyeitwa Sen no Rikyu, ambaye alikuwa msanii wa sanaa ya chai ya Kijapan ambayo kwa Kijapan inaitwa Chanoyu.

Kwa mapenzi makubwa ambayo Hideyoshi alikuwa nayo kwa Rikyu, alimpa mpaka nyumba kwenye makazi ya mfalme. Waliishi vizuri mno. Hata hivyo, siku Hideyoshi alipogundua kuwa Rikyu alikuwa na sanamu lililochongwa taswira yake, alikasirika mno.

Uamuzi wa Hideyoshi ulikuwa ni adhabu ya kifo kwa Rikyu. Kweli, Rikyu aliuawa. Watu walishangaa mno kwa uamuzi huo kutoka kwa Hideyoshi na Rikyu, ukifika Tanzania, unagundua kwamba pengine Gwajima na Polepole wanataka kuchonga sanamu lenye sura zao, ambalo hata Rais Samia hana. Wanajua zaidi? Wanawapenda zaidi Watanzania?

Columnist: www.tanzaniaweb.live