Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

CAF ijitenge na uhuni huu

USM Uhuni CAF ijitenge na uhuni huu

Sat, 10 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Anga la jiji la Algiers ni jekundu likichochewa na baruti na milio ya kutisha iliyotokana na fataki. Kwenye Uwanja wa 5 Juliet, hali inatisha kiasi amabacho kinatosha kumtisha mgeni ambaye ni mara yake ya kwanza katika viunga vya Algiers au katika viwanja vya nchi za Algeria, Morocco ,Tunisia, Libya au Misri.

Ni mchezo wa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya USM Alger ya Algeria na Yanga ya Tanzania. Yanga wanapata penalti ya mapema, anasogea Djuma Shabani kwenda kuipiga, milipuko ya fataki inaendelea huku akimulikwa na miali ya kijani ya vikurunzi.

Djuma Shabani anafanikiwa kuukwamisha mpira wavuni lakini wingu jekundu na moshi mweupe na mweusi bado vinatemwa uwanjani kadri mchezo unavyoendelea. USM Algiers wanapata pigo la penalti, miali ya kijani inaelekezwa kwa mlinda mlango Djigui Diara wa Yanga. Mpira unakwenda kupigwa inasikika milio ya fataki kama miwili. Golikipa anahimili na kudaka pigo hilo.

Mpira unaendelea USM Algiers wakiwa nyuma kwa goli moja lakini wakiwa na faida ya ugenini. Mpira unapotoka, watoto waokota mipira (ball boys) wanaiingiza mingi uwanjani kiasi kwamba mchezo hauwezi kuendelea mpaka ubaki mpira mmoja.

Kwa tuliopata bahati ya kusafiri na timu katika baadhi ya mataifa ya Kaskazini mwa Afrika, vitendo hivi tunaweza kusema ni vya kawaida na vinafanyika mbele ya viongozi wa chama cha mpira cha nchi husika, viongozi wa shirikisho la soka Afrika (CAF) na viongozi wa FIFA.

Viongozi wa serikali pia huwapo uwanjani wakishuhudia vitendo hivi ukiachia mbali vingine vingi vinavyofanyika nje ya mchezo kama kucheleweshwa katika dawati la uhamiaji kwa timu ngeni inapowasili, vurugu kwenye hoteli za timu ngeni, kucheleweshwa misafara ya kwenda mazoezini, kupewa uwanja mbovu wa mazoezi na hata kuzimiwa taa wakati wa mazoezi ya timu ngeni.

Kilichowapata Yanga siyo kigeni hapa Afrika. Inaonekana kana kwamba vitendo hivi na nchi zinazofanya zimepewa ruksa kufanya hivyo. Vitendo hivi vinaonekana sasa kuwa sehemu ya utamaduni wa mataifa hayo kiasi cha kuanza kuvifanya hata wanaposafiri nje ya nchi zao.

Haishangazi kuona mashabiki wachache wanaosafiri na timu hizi za Maghreb wakifyatua fataki kwenye viwanja vya ugenini. Tuliwaona mashabiki wa Wydad Casablanca wakifyatua moshi wa mafataki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam timu yao ilipokuwa ikicheza na Simba kwenye mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati wa Kombe la Dunia la Fifa 2014, mashabiki wa Algeria walituhumiwa kummulika kwa miali ya tochi golikipa wa Russia wakati ukipigwa mpira wa adhabu kiasi cha kupelekea Algeria kupata bao katika mchezo huo ulioisha kwa sare.

Misri, ambao ni kati ya wanaoongoza kwa vitendo hivi na hata vile vya kibaguzi uwanjani, walijikuta wanakuwa waathirika wa utamaduni huo pale timu yao ilipokosa tiketi ya kwenda Kombe la Dunia dhidi ya Senegal.

Mshambuliaji wao anayechezea Liverpool, Mohamed Salah alimulikwa kwa miali ya kijani wakati timu zilipoenda kwenye mapigo ya penalti ya muda wa ziada. Salah alikosa penalti na lawama zikaenda kwa miali ya tochi.

Misri walilalamika kwa FIFA lakini haikutosha kuwapatia tiketi ya kwenda Qatar 2022. Hii ilitosha kuwaonyesha mashabiki wa Misri ubaya wa vitendo hivi lakini kama ilivyo kawaida ya manazi wa mpira, vitendo hivi bado vinafanyika sana kwenye viwanja vya Misri na hata mashabiki wa klabu zao bado wanatembea na tochi zao.

Wengi tunakumbuka uhasama uliokuwepo, na bado upo, kati ya Algeria na Misri kiasi cha mchezo wao wa kufuzu Kombe la Dunia 2010 kupelekwa nchi ya tatu Sudan.

Mpaka sasa mchezo kati ya mataifa haya huwa ni suala kubwa na linalotishia usalama na diplomasia kati ya mataifa haya. Hii ni matokeo ya kuvumiliwa vitendo vidogovidogo na mamlaka zinazohusika na mchezo huu.

Vitendo hivi, kama nilivyosema, vinafanyika mbele ya viongozi wa mpira na mbele ya sheria za mpira ambazo zinakataza vitendo hivyo. Vitendo hivi ni kama vimebarikiwa kiasi kwamba baadhi ya mashabiki hata wa hapa kwetu wanaanza kujifunza na kuona kama polisi wetu wanakosa uzalendo pale wanapozuia vitendo hivi kwani wameona kwamba ushindani wa timu zetu dhidi ya mataifa yanayoonekana yameendelea kisoka hapa Afrika unakwamishwa na upole wetu.

Vurugu hizi zinaonekana kuwa na faida kwa wafanyaji, hasa hapa Afrika, pamoja na kutokuwa na faida kwa mpira wenyewe na kuzuiliwa na kanuni za usalama viwanjani za CAF na FIFA.

Wenzetu wa Ulaya (Uefa) wanaonekana angalau kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya kihuni katika mchezo wa mpira wa miguu pamoja na kwamba hawajafanikiwa kuvikomesha kabisa. Mfano mzuri ni pale England walipocheza na Denmark katika mashindano ya Euro 2020.

Ilionekana golikipa wa Denmark, Kasper Schmeichel kuchomwa na miali ya kijani machoni wakati akijiandaa kudaka penalti ya Harry Kane ambayo alifanikiwa kuidaka na Uefa wakathibitisha hilo kwa kuwatwanga England faini ya Euro 30,000 kutokana na kitendo hicho, kuzomea wakati ukiimbwa wimbo wa taifa wa Denmark na kupiga fataki za moto.

Ni muda mwafaka sasa kwa CAF kutoka na kuonyesha mamlaka yake kwa kuzichukulia hatua klabu, viwanja na vyama vya mpira pale vitendo vya kuvuruga mchezo vinapofanyika.

Hatua hizi zikionekana kuwanyima wenyeji ushindi au kuwanyima mashabiki nafasi ya kuingia uwanjani kuiunga mkono timu yao basi zitakuwa zimesaidia kuusafisha mchezo.

Vitu vingi vinaonekana sasa kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia hasa ya televisheni hivyo ni wakati mwafaka wa kuvishughulikia. Kinyume chake, teknolojia hii itatumika kueneza vitendo hivyo jambo ambalo ni la hatari.

Viwanja vya mpira vitakuwa viwanja vya vita na mpira utachezwa dakika 50 badala ya dakika 90. CAF isisubiri maafa yatokee kwa mashabiki na hata wachezaji na maofisa wa mchezo. CAF isafishe taswira yake kabla haijachafuka zaidi. Hatua zichukuliwe sasa kuua utamaduni huu wa kihuni.

Columnist: Mwanaspoti