Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Brigedia Jenerali Luwongo mstaafu mwenye kipaji cha gofu, soka

Gofu Brigedia Jenerali Luwongo mstaafu mwenye kipaji cha gofu, soka

Mon, 27 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

“Nilipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, sikuwa mchezaji gofu, ilikuwa ni mwaka 2016, mlezi wa klabu akiwa Mkuu wa Majeshi wakati huo, Jenerali Davis Mwamunyange aliniteua kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali, Ernest Galinoma (aliyefariki),” anasema Brigedia Jenerali, mstaafu Michael Luwongo alipozungumza na Mwanaspoti na kuongeza;

“Uteuzi wangu haukuzingatia nacheza gofu au la! kijeshi unapopata uteuzi wa namna hiyo kiongozi wako anapokupangia kazi maana yake unaukubali kimaandishi uteuzi, ndivyo nilifanya pia.”

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na Brigedia Jenerali mstaafu huyo ambaye alifunguka mambo mengi na kufafanua baada ya uteuzi huo nini kilifuata.

“Wiki ya kwanza baada ya uteuzi niliitumia kujifunza sheria za gofu, baada ya hapo nilianza kuyafahamu mazingira ya uwanja kwa kuutembelea, kuyafahamu mashimo na viwanja vyote 18 vya gofu na vifaa vyake, hadi 2017 sikuwa nacheza zaidi ya kuusoma huo mchezo,” anasema.

Anasema miaka miwili baadae hadi 2018 ndipo alianza kucheza mchezo huo na hakupata shida kuumudu kutokana na mazingira ya kimichezo aliyopitia awali.

“Nilikuwa nacheza soka tangu shule, chuo na hata jeshini, nimecheza kwa kiwango kikubwa kwenye nafasi ya midifildi, wakati huo sikuwa na mwili huu na nilifurahia kuwa kwenye nafasi ya kuichezesha timu uwanjani hadi nilipostaafu soka.

“Hata nilipoanza kujifunza gofu, sikupata tabu kwa kuwa ni mwanamichezo, habari njema kwenye gofu kuna viwanja maalumu vya kujifunzia, unapoanza unatumia viwanja hivyo vinavyokujenga kumudu kupiga mbali na mambo mengine, lakini pia kipo kiwanja cha kumalizia hadi unaingiza mpira kwenye shimo.

Mwaka 2019 ndipo Brigedia Jenerali mstaafu, Luwongo alipata rasmi ‘golf handicap’ ambayo inawatambulisha wachezaji wa gofu duniani kulingana na madaraja yao.

“Ili kutambuliwa na kuingia kwenye mfumo wa gofu duniani, popote pale utakapokuwa ukijitambulisha kwa handicap yako wanakuona kwenye mfumo,” anasema.

GOFU SI WA VIBOPA TU

Katika fikra za wengi, uamini gofu ni mchezo maalumu kwa ajili ya jamii yenye hadhi fulani na kipatocha juu, jambo ambalo Brigedia Jenerali, mstaafu huyo anasema si kweli.

“Hapa Dar es Salaam kabla ya mkuu wa majeshi wakati huo, Jenerali Waitara kuja na wazo la kuanzisha Uwanja wa Lugalo, kulikuwa na uwanja mmoja pekee wa Gymkhana.

“Klabu ya Lugalo tulifungua milango kwa mtu yeyote anayependa kucheza, tulifundisha vijana pia ambao ndio wanatusaidia (ma-ked) ambao mbali na kubeba mabegi, lakini ni wachezaji wazuri na ukiwa naye uwanjani ni mshauri, wanaijua gofu na ni wachezaji pia.

“Japo ili kuwa Ked sio lazima uwe mchezaji, lakini unapaswa kuwa na uelewa na mchezo wa gofu, kitengo hiki kina kiongozi wao (ked master), ambaye ili kujiunga huko unapitia kwake,” anasema.

Anasema klabu ya Lugalo ina wanachama 361 na ni rahisi kujiunga kwa mgeni, utaonana na golf captain atakayekupa muongozo, ingawa kuna ada na baadhi ya michango kama huna uelewa kabisa na gofu, unapangiwa ked mzuri ambaye atakuongoza na kukushauri pia.

“Tuna programu ya watoto pia, lengo ni kutengeneza timu ya taifa imara, tulianza na watoto wachache na sasa tunao 52 ambao hawalipii gharama zozote kujifunza.

“Katika programu hii, wapo miongoni mwao wako kwenye timu taifa, hivyo ile dhana gofu inachezwa na watu fulani tu, haipo tena,” anasema.

MAVAZI YA GOFU

Bila fulana yenye kola, huwezi kucheza gofu, Brigedia Jenerali, mstaafu Luwongo anasema huo ni mchezo wa kiungwana hivyo unapaswa kuwa na mwonekano wakati ukiwa uwanjani.

“Mfano leo (wiki iliyopita), tuko uwanjani lakini kuna ki-baiskeli kinapita wakati mnacheza kinagawa vinywaji kutoka kwa mdhamini wetu kampuni ya Serengeti, huu ni mchezo wa kiungwana na lazima uonekane kiungwana uwanjani, uchomekee vizuri na mtu anapopiga mpira mnaomzunguka mnapaswa kunyamaza kimya.

“Kuvaa kofia sio lazima, ni mtu mwenyewe akiamua, lakini mavazi ya gofu ni fulana ya kola, bukta au suruali ‘smart’ na raba,” anasema.

Anasema begi la kila mchezaji linapaswa kuwa na fimbo zisizopungua 14, kuna fimbo mbalimbali zipo za wood, iron na nyinginezo na kila moja ina sehemu yake mfano mpira umeingia kwenye miti unataka kuutoa kuna fimbo yake, ukiingia kwenye mchanga, ukikaribia kumaliza kama mita 50 pia kuna fimbo zake.

“Unapaswa kuwa na seti ya tee ambazo sasa hawataki tutumie za plastiki tunatumia za miti ambazo ukipiga mara mbili tatu inavunjika hivyo unatumia nyingine, lazima uwe nazo seti,” anasema.

Anasema seti ya vifaa vya gofu, zikiwa zile profesheno kama zile zinazotumiwa na nyota wa dunia, Tiger Woods si chini ya Sh5 milioni.

“Lakini vipo mpaka vya Sh500,000, ingawa pia sio lazima uwe na begi lenye vifaa vyote, unaweza kuwa na fimbo chache kama tano za kuanzia kama driver moja, iron mbili na zile za kumalizia, baadae unajazia kidogo kidogo,” anasema.

SIRI YA MAJI VIWANJANI

Umewahi kujiuliza mabwawa ya maji kwenye viwanja vya gofu yana kazi gani? Unaambiwa madimbwi hayo yanatengenezwa makusudi ili mtu aharibu na kupata penalti.

“Unahitaji kutumia akili nyingi sana unapopiga mpira ili usiingie kwenye maji, ukikosea kidogo ni penalti, mpira ukiingia kwenye maji, badala ya kupiga shot mbili, utalazimika kupiga tatu na uwezekano wa kupata shot tano ni mgumu hivyo utapata sita.

Shoti tatu ziko hivi, kwenye gofu anayepiga shot chache ndiye kinara, ili mpira uingie kwenye shimo utapiga shot tatu kuendelea, japo wapo wanaopiga mbili.

Inaelezwa kwenye mashindano makubwa ya kimataifa, wanaopiga shot moja na mpira ukaingia moja kwa moja kwenye shimo wanawekewa zawadi ya gari hapo hapo, wengine wapiga shot mbili na kuingiza mpira shimoni.

Kocha Rodrick John anasema Tiger Woods ni miongoni mwa nyota wa dunia wanaoweza kupiga shot moja na kuingiza mpira kwenye shimo.

“Ni mazoezi tu yanahitajika ili kupiga shot moja, mchezo wowote ni mazoezi na hata kwenye gofu iko hivyo,” anasema kocha huyo.

Hata hivyo, Brigedia Jenerali, mstaafu Luwongo anasema mpira ukiingia kwenye maji ni pelnati na badala ya kupiga shot mbili utalazimika kupiga tatu.

Columnist: Mwanaspoti