Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bradford City kama Yanga tu England

Brentford FC.jpeg Wachezaji wa Brentford

Sat, 25 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika miaka michache iliyopita hadi sasa tumekuwa tukisikia mashabiki wa Yanga wakitajwa na kujiita “Wananchi” na tayari jina hilo limekuwa maarufu kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo kama ilivyowahi kupewa jina la Kanda Mbili miaka ya 1970.

Simba nayo ambayo siku hizi mashabiki wameipa jina la utani la Mnyama siku hizo iliwahi kupewa jina la Underline (Sisitiza) au Abidjan (Jiji Kuu la Ivory Coast).

Kila ninaposikia kauli za kujiita mashabiki wa Yanga jina la Wananchi huikumbuka Klabu ya England iitwayo Bradford City iliyong’ara miaka ya 1950 na 1960. Jina maarufu la mashabiki wa klabu hiyo hadi leo ni Wananchi na utawasikia mashabiki wao wakitamka Citizens - Citizens (Wananchi - Wananchi) pale inapokuwa uwanjani.

Klabu hiyo ilitamba katika medani ya soka ya England miaka ya nyuma pamoja na zile za Blackpool, Wolverhampton Wanderers, Manchester United, Manchester City, West Ham United, Newcastle United na Bolton Wanderers.

Bradford iliwahi kuwa na wachezaji wazuri ambao waliitwa kujiunga na kikosi cha England kilichoshiriki Kombe la Ulaya na Dunia.

Kwa muhtasari, Bradford ilikuwa mashuhuri na kuwa miongoni mwa timu zilizotawala kandanda la England kama ilivyokuwa kwetu miaka ile kwa timu za Coastal Union na African Sports za Tanga, TPC ya Arusha Chini huko Moshi na Cosmos ya Dar es Salaam.

Wakati baadhi ya klabu zilizokuwa zinachuana nazo zinang’ara Ligi Kuu ya England, Bradford hivi sasa inagaragara daraja la nne.

Wakati ligi hiyo ya timu 24 ikiwa inamaliza mzunguko wa kwanza inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 48, Leyton inayoongeza imejipatia pointi 67. Hii ina maana nafasi ya kupanda daraja msimu ujao ni ndogo.

Mara ya mwisho kucheza Ligi Kuu ya England ilikuwa msimu wa 2000-2001 na iliponea chupuchupu msimu uliofuata baada ya kufanya maajabu ya kuifunga Liverpool 1-0 mchezo wa mwisho.

Lakini tangu kuporomoka katika Ligi Kuu 2001 imekuwa ikijipapatua katika madaraja ya chini na sasa safari ya kupanda kwenda Daraja la Tatu inaonekana ngumu.

Sifa kubwa ya klabu iliyoanzishwa 1903 ni kwamba asilimia kubwa ya wanachama wake ni watoto, wajukuu na virembwe vya wanachama wa miaka ya nyuma.

Mnamo Mei 11, 1985 klabu hiyo ilikumbwa na maafa makubwa pale moto ulipowaka kwenye uwanja wake unaochukua wazamaji 25,000 na mashabiki wake 56 walipoteza maisha.

Tangu wakati ule Bradford haishiriki mchezo wa kirafiki wala mashindano kila Mei 11 ya kila mwaka kama kumbukumbu ya maafa hayo. Sanamu kubwa la ukumbusho wa maafa hayo ipo nje ya uwanja wa klabu hiyo. Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kubeba Kombe la FA 1911 baada ya kuifunga Newcastle kwa 1-0 katika mchezo wa pili.

Katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bila ya kufungana. Siku zile mchezo ulikuwa wa dakika 60, nusu saa kwa kila nusu ya kwanza na hakukuwa na dakika za nyo-ngeza wala kupigiana matuta.

Bradfrord iliteremka daraja 1922, ikapanda tena msimu uliofuata na kuporomoka a 1927, lakini ikarudi msimu uliofuata na kuteremka 1939. Baadaye ilipanda na kubaki huko hadi 1972 ilipoporomoka na kurudi kucheza Ligi Kuu msimu wa 1998-99 na tangu ilipoporomoka msimu wa 2000-2001 imekuwa inahaha madaraja ya chini.

Lakini mashabiki wake hudai kuwa wamezowea kupanda na kushuka na ipo siku sio kurudi tu Ligi Kuu, bali watachukua ubingwa.

Kama zilivyo baadhi ya timu nyingine za madaraja ya chini Bradford imekuwa wakati mwingine inatoa ushindani mkali katika mashindano ya Kombe la FA kwa kuzitoa jasho timu kubwa.

Kwa mfano 2015 timu hiyo iliwashangaza watu wengi ilipoiendesha mchakamchaka Chelsea ambayo ilikuwa klabu bingwa na kuifunga mabao 4-2 katika Kombe la FA.

Katika mashindano hayo, Bradford pia iliitupa nje Sunderland kwa ushindi wa mabao 2-0, lakini ikasalimu amri katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo kwa kufungwa na Reading mabao 3-0 mchezo wa marudiano. Mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bila ya kufungana.

Wakati timu hiyo ilipoteza umaarufu iliokuwa nayo ikijitahidi kurejesha hadhi yake ya zamani tukumbuke kwamba japo usemi maarufu wa Kiswahili wa “Mpanda ngazi hushuka” wapo walioshuka na wakaja kupanda tena.

Tusubiri, lakini kwa msimu huu uliofika nusu matumaini ya Bradford kupanda hiyo ngazi ni madogo, lakini maajabu ni mambo ya kawaida kwenye kandanda.

Itakumbukwa kwamba hata matokeo ya Ligi Kuu ya England 2015-16, Leicester iliyokuwa ikitarajiwa kuwa miongoni mwa timu zitazoteremka daraja na haikuwemo kwenye orodha ya timu 10 bora zilizokuwa na mweleko wa kuwa mabingwa, ndio iliyokuja kuibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa.

Columnist: Mwanaspoti