Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Boulmerka mwanamke jasiri aliyevunja mwiko wa Kiarabu Olimpiki

IMG 4332.jpeg Hassiba Boulmerka

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Habari za michezo zinazotawala vyombo vya habari katika nchi za Kiarabu siku hizi ni mafanikio ya wanawake katika mashindano ya kimataifa, jambo liliokuwa kama ndoto ya mtu kichaa miaka michache iliopita.

Wanawake walikuwa sio tu hawaruhusiwi kushiiki katka michzo na hasa mashindano, bali hata kuwa watazamaji.

Miongoni mwa nchi ambazo zilikawia sana kuwaruhusu wanawake kushiriki michezo ni Saudi Aradia, nchi za Ghuba, Oman na Iran.

Kwa mfano, mwishoni mwa mwezi Januari, mwaka huu, timu ya kandanda ya wanawake wa Saudi Arabia ambayo tangu kuundwa kwake ilikuwa chini ya miaka miwili ilibeba kombe katika mashindano ya kwanza ya mchezo huo ulioshirikisha nchi sita.

Raneem El Welily wa Misri hivi sasa ni miongoni mwa wanawake wanaoutawala mchezo wa boga (squash) duniani. Alikuwa bingwa wa dunia mwaka 2017.

Haikuwa kazi rahisi kwa wanawake wa nchi hizi kupata mafanikio tunayoyaona na kama yupo mtu ambaye unayeweza kusema alipanda mbegu ya mavuno haya sio mwengine isipokuwa mwanamama shupavu wa Algeria, Hassiba Boulberka.

Siku hizi kila ikisimuliwa historia ya Olimpiki ujasiri wa huyu mama katika michezo ya Olimpiki ya 1992 iliyofanyika Barcelona, Hispania huelezwa kwa urefu.

Alipambana na misukosuko, ikiwa pamoja na kutishiwa yeye na familia yake kuuawa kwa kuambiwa haiwezekani mwanamke kukimbia hadharani akiwa na kivazi kisichokubalika. Hassiba alijifanya kiziwi na kukataa kurudi nyuma na juhudi zake katika riadha zilifungua ukurasa mpya wa historia kwa kushinda medali ya dhahabu ya mbio za mita 1,500. Mafanikio hayo yalimfanya kuwa mwanamke wa kwanza wa Kiarabu kubeba medali ya dhahabu ya Olimpiki na wa kwanza kutoka Afrika kuwa bingwa katika michuano ya dunia.

Wakati wa michezo ya Olimpiki ya 1992 viongozi wa Kiislamu wa Algeria walifanya kampeni ya kukataa akina mama kushiriki michezo kwa vile mavazi yaliwafanya wawe nusu uchi. Hali hii ilimlazimisha Hassiba kutoka nje ya nchi kufanya mazoezi na kila alipoambiwa anasakwa ili auawe hakujali. Alipokuwa anafanya mazoezi nchi za nje alilindwa na askari wenye silaha na alipokwenda uwanjani kushiriki michezo alifuatana na wanajeshi.

Mwana mama huyu aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (OIC) sasa anamiliki kampuni ya vifaa vya michezo Algeria yenye matawi nchi za jirani.

Katika maduka yake zipo picha za alipokuwa akikimbia na alizopiga na wanariadha mashuhuri wa zamani na watu mashuhuri wengi, akiwemo Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Hivi sasa yuo mstari wa mbele kutetea haki za wanawake na watoto na hutembelea shule na vyuo kuwataka wanawake wa Kiislamu kuheshimu mafunzo na maelekezo ya dini kama kutojiiingiza katika mambo ya usagaji au ndoa za wanawake wawili, lakini washiriki kila mchezo.

"Urafiki wa karibu na mwanamke mwenzio ni mzuri, lakini musiishi kama mke na mume. Heshima kwa mume haistahiki kudharauliwa," mwanamama huyu anasema.

Michezo ilianza zaidi ya miaka 500 iliopita na wanawake walishiriki kwa maraya kwanza katika michezo iliyofanyika Ufaransa1900.Nchi ya kwanza ya Afrika iliyoshiriki ni Afrika ya Kusini katika mwaka1908, wakati huo ikitawaliwa na makaburu.

Waafrika wa nchi nyengine walishiriki katika vikosi vya watawala wa nchi zao - Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Ureno na Hispania. Mashindano ya 1890 yalikuwa na wana michezo 241, lakini siku hizi zadi ya 10,000 na hushirik zaidi ya michezo 300 kwa wanaume na wanawake.

Kwa miaka mingi wanawake wa Afrika walijitahidi angalau kupata medali ya fedha, lakini hawakufanikiwa. Mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1990 walikuwa washindikizaji na wachache waliopata medali za shaba walionekana kufanya miujiza.

Hatimaye katika mwaka 1992 ndipo Hassiba alipofungua ukurasa mpya wa historia kwa kubeba medali ya dhahabu ya mita 1,500. Hapo kabla alibeba medali ya dhahabu ya mbio hizo katika mashindano ya Dunia yaliyofanyika Japani 1991. Alitumia dakika 4:2.21 na mafanikio yake yaliwashajiishaa wanawake wa Afrika kufanya vizuri.

Magazeti ya Ulaya yaliyoelezea ushindi wake kwa vichwa vya habari vya: Mwanamke wa Kiafrika anasema basi; Dada wa Algeria awafungia mlango wazungu na Dada wa Algeria awateka nyara wazungu. Hassiba, akiwa na miaka 20 alikuwemo katika kikosi kilichokwenda Korea ya Kusini 1988 kushiriki michezo ya Olimpiki, lakini alitolewa mapema katika mbio za mita 800 na 1,500. Aliporudi nyumbani alijinoa na mnamo 1991 alikwenda Rome, Italia, kushiriki Tamasha la Dhahabu na kushinda mbio za mita 800 kwa dakika 1: 58.72.

Katika michezo ya Olimpiki ya 1992 alitarajiwa kutokea wa tatu au wa nne katika mita 1,500 ziliosheheni wakimbiaji nyota lakini aliushangaza ulimwengu kwa kutimua mbio za kasi wakati masafa ya kufikia utepe yakibakia mita 200, kama vile ndio kwanza aliingia uwanjani. Alichuana na Lyudmila Rogachova wa Urusi aliyekuwa nyota wa masafa haya na watu wengi walisubiri kujua nani angetokea wa pili.

Lyudmila aliongoza na hakuna aliyetarajia mkimbiaji mwengine kumkaribia, lakini yalipobakia nusu ya masafa Hassiba aliyekuwa wa sita alijivuta na kuwaweka pembeni wakimbiaji mmoja baada ya mwengine.. Zilipobakia mita 300 alikuwa nyuma ya Lyudmila na aliongeza kasi kama gari iliokolezwa mafuta na katika mita 100 za mwisho alikuwa bega kwa bega na Mrusi na wakimbiaji wengine wawili. Aliongeza kasi na kumuacha Mrusi haamini kilichotokea.

Mbio hizi ziliotengenezewa filamu iitwayo “Mapinduzi ya Riadha” zilikuwa na ushindani mkubwa na wakimbiaji wanne walimalizia kwa chini ya dakika nne. Aliporudi Algeria alipata mapokezi kama shujaa na kupewa zawadi na serikali na watu mbali mbali.

Kijana mmoja wa miaka 11 alimfurahisha alipomtaka afunge naye ndoa na Hassiba alimjibu: "Maliza masomo... nitakusubiri”. Mwingine alimwambia ana mke, lakini alitaka kumuongeza yeye (Hassiba) kuwa wa pili.

Huku akitabasamu alijibu: "Ukitaka nifurahi, kama ulivyofurahi, ninakuomba uishi vyema na mkeo. Usimkimbie kwani hakuna medali ya dhahabu wala shaba kwa anayoongeza mke wa pili”. Viongozi wa Afrika walimmwita balozi wao katika riadha kwa kuuonyesha ulimwengu uwezo wa mwanamke wa Kiafrika, lakini wapo viongozi wa Kislamu wa Algeria walimlaani kwa kuweka maungo yake ya siri hadharani kutokana na kivazi alichotumia kukimbia.

Kauli hizi zilimnyima raha na muda mwingi alikuwa Ulaya akishiriki mashindano, lakini alikataa vishawishi vya nchi hizo vya kumtaka abadili uraia. Alisema alifurahia kuzaliwa Algeria na alipenda kukimbia na bendera ya nchi yake na alifanya hivyo mpaka alipostaafu.

“Tusidanganyane. Nyumbani ni nyumbani. Ninafurahi watu wa Algeria na Afrika wananifurahia na sina ubaya na wanaofikiri nimepotea njia. Nomba waelewe ninakimbia kutetea heshima ya nchi yangu”, alisema huku machozi yakimtoka.

Alipoona vitisho vya kuuawa vimezidi alikwenda Cuba na kuishi kwa muda. Hassiba alistaafu baada ya mashindano ya Mabara yaliyofanyika Marekani, 1996 baada ya kuumia kisigino alipowekewa mkwara wakati akikimbia.

Alichaguliwa mjumbe wa Kamati ya Riadha ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), akiwa na miaka 28. Hassiba alizaliwa katika mji wa Constantine, Algeria, tarehe 10 Julai, 1968 na kushiriki mashindano ya shule na kuwa bingwa wa mbio za masafa ya kati.

Katika mashindano ya Afrika ya 1988 alishinda mita 800 (dk.2: 06.16) na mita 1500 (dk.4:12.14). Siku hizi anashughulikia biashara zake na kutembelea shule na vyuo kuzungumza na wanafunzi juu ya umuhimu wa kufuata maadili mazuri.

Columnist: Mwanaspoti