Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bodi ya Ligi na ubabe uliopindukia

Simba Mbeya Duh Bodi ya Ligi na ubabe uliopindukia

Wed, 18 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hapo zamani za kale ligi yetu ilikuwa ikisimamiwa na kuendeshwa moja kwa moja na TFF (FAT).

Lakini mwanzoni mwa miaka ya 2010 au nyuma yake kidogo, zikaanza harakati za kuundwa chombo huru cha kusimamia na kuendesha ligi ili TFF ibaki ikisimamia timu za taifa na maendeleo ya mpira wenyewe.

Ndipo ikaundwa kamati ya ligi na baadaye ikaja kuwa Bodi ya Ligi Kuu. Chombo hiki kiliundwa mahsusi kuhakikisha ligi yetu inaendeshwa kibiashara huku ikimilikiwa na wadau wenyewe ambao ni vilabu.

TFF kama mwenye dhamana ya mpira nchini, anakuwa mwanahisa kwenye chombo hiki. Ili kiweze kutimiza majukumu yake, chombo hiki kikaunda kamati mbalimbali, ikiwemo ya usimamizi na uendeshaji wa ligi ambayo zamani ilifahamika kama kamati ya saa 72.

Kwa bahati mbaya ni kwamba kamati hii badala ya kijikita hasa na majukumu yake ya msingi, imegeuka kuwa kamati ya kulipana posho, kula korosho na kuwafungia watu.

Mambo mengi ya msingi ambayo kamati hii ilipaswa kuyapa umuhimu, yanaendelea kuwa ya hovyo huku watu wakifungiwa kila uchao.

Kamati hii ilipaswa ije na mbinu mbadala za kuboresha viwanja vyetu. Na jambo kubwa kwenye hili siyo kamati au bodi ya ligi kukarabati viwanja, hapana.

Kamati au Bodi haiwezi kuwa na hiyo bajeti, na wala hatutarajii hilo. Wanatakiwa kukabati kanuni na miongozo yao ili kuhakikisha miundombinu ya soka hapa kwetu inakuwa bora hasa.

Kwa mfano, kanuni za ligi yetu zinataka timu za ligi kuu zifundishwe na makocha wenye Diploma A ya CAF yaani makocha ambao Wana vigezo vya kufundisha Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sasa kwanini kanuni pia zisiseme kwamba uwanja wa ligi kuu unatakiwa uwe na vigezo vya kuchezewa ligi ya mabingwa Afrika?

Hii haihitaji elimu ya chuo kikuu kuiona. Unamtaka kocha mwenye hadhi ya ligi ya mabingwa afundishe timu inayocheza uwanja wa Ndondo Cup, uko siriasi' wewe?

UBABE

Kamati hii hukutana kila baada ya raundi moja ya ligi kuu, kupitia matukio yote yaliyojiri kwenye raundi husika.

Shida huja pale inapotokea kuna mtu kalalamikiwa na moja ya ripoti za aidha waamuzi au wasimamizi wa baadhi ya mechi.

Kamati hii itachukua hayo malalamiko na kutoa hukumu.

Yaani kamati inahukumu kesi kwa kuusikiliza malalamiko tu, yawe ya kweli au siyo ya kweli siyo kazi yao.

Watu wengi wanaofungiwa na hii kamati huwa wameonewa aidha kwa kutohusika kabisa au kuhusika kwa sehemu ndogo lakini huku inakuwa kubwa kuliko kosa.

Hii yote ni kwa sababu mlalamikiwa hapewi nafasi ya kusikilizwa akajitetea na kutoa simulizi ya upande wa pili.

Kusikilizwa ni haki ya msingi ya mlalamikiwa au mshitakiwa yoyote yule. Pia ni haki ya kikatiba katika nchi yetu. Mtu hawezi kushitakiwa na kuhukumiwa pasipo kusikilizwa lakini kwenye kamati hii inawezekana.

Mwenyekiti wa kamati hii ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu. Makamu wake pia ndiyo Makamu wa Bodi ya Ligi Kuu.

Karibu wa hii kamati ndiyo mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu.

Maana yake hiki ni chombo kinachosimamiwa na kuendeshwa na klabu zenyewe, na wanapokutana na hii kadhia mara nyingi ni watu kutoka kwenye klabu hizo hivyo hivyo lakini hakuna anayejali.

Hapa sasa ndipo tunarudi kwenye posho na korosho.

Wajumbe wa vikao vyote vya kamati hii hulewa korosho muda wote wa vikao na kujikuta wakikosa cha kujadili.

Akili zao zipo kwenye kusaini tu ili wapate posho zao na kusubiri raundi ijayo. Hukumu za upande mmoja ndizo hutumiwa na madikteta kuwazima wapinzani wao. Dikteta Sani Abacha wa Nigeria alitumia mbinu kama hiyo kumnyonga mwanaharakati Keni Sarowiwa.

Kuna ugumu gani wa kumuita mtuhumiwa na kumsikiliza?

Ina maana kamati inawaamini waamuzi wao na wasimamizi wao kiasi hicho? Mara ngapi ripoti zao zinakuwa na makosa?

Waamuzi wengi hukosea kuandika hata majina ya wachezaji waliofunga mabao, na kutaja jina tofauti na mfungaji husika.

Januari 15, 2019 mwamuzi Fikirini Yusuf na yule wa akiba, Bakary Rashid, walimnyima bao Salimu Aiyee wa Mwadui dhidi ya Yanga.

Hawakumnyima kwa kulikataa, hapana, walilikubali bao lake lakini kwenye ripoti yao wakamtaja Ibrahim Irakoze.

Yaani mfungaji alikuwa Salim Aiyee, waamuzi wakaandika mfungaji ni Ibrahim Irakoze.

Sasa hiyo ingekuwa kesi mbele ya kamati, maana yake Irakoze angehukumiwa lakini kumbe kosa hakufanya yeye.

Kwa hiyo ili kujiridhisha ni muhimu kuwatia watuhumiwa na kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kamati.

Hii itasaidia sana kamati kujua upande wa pili wa shauri lililopo mezani kwao. Kamati iache ubabe. Kamati iliendelea na ubabe, inaichafua Bodi ya Ligi, nayo inakuwa ya kidikteta.

Columnist: Mwanaspoti