Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Blatter anapoamua kutubu katika dakika za majeruhi

Blatter Sepp Rais wa zamani wa FIFA, Sepp Blatter

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Rafiki yetu, Joseph Blatter, najua unamfahamu kwa jina la Sepp Blatter ghafla aliibuka kutoka kusikojulikana hivi majuzi. Nimecheka sana. Amedai lilikuwa kosa kubwa kuipa nchi ya Qatar kuandaa fainali za Kombe la Dunia. Amenichekesha.

Sijui kama Blatter anakaribia kufa lakini ukweli ni kwamba Machi mwakani atatimiza umri wa miaka 87. Hana miaka mingi ya kuishi mbeleni kuliko miaka iliyobaki mbele yake.

Nadhani ameamua kutubu. Ameamua kutubu dhambi zake za hatari alizowahi kufanya duniani. Kuipa Qatar fainali za Kombe la Dunia ni miongoni mwa madhambi yake.

Akiwa Rais wa Fifa aliongoza kundi la wahuni wenzake kuipa Qatar fainali za Kombe la Dunia. Nchi ambayo ina kilomita za mraba 11,571.

Wakati huo huo Mkoa wa Morogoro Tanzania una kilomita za mraba 73,039. Kuna wilaya moja ya Morogoro ni kubwa kuliko Qatar.

Blatter na wenzake waliamua kuipa nchi hii Kombe la Dunia. Fifa ni wakubwa sana na wameandaa fainali nyingi za Kombe la Dunia. Walijua walichokuwa wanakifanya. Basi tu katika dakika hizi za majeruhi Blatter anajifanya kuwageuka wenzake na kujitoa fahamu kana kwamba alikuwa hafahamu alichokuwa anakifanya.

Kilichofanyika kilitokana na mlungula. Wakati huo Blatter na wenzake walikuwa katika ubora wao wa kupokea milungula. Walikutana mahala wakachukua pesa za Warusi na Waarabu kwa ajili ya kuwapa uenyeji wa Kombe la Dunia 2018 na 2022. Ni mpaka pale Wamarekani walipoamua kuisambaratisha Fifa na Blatter wao.

Leo Blatter anatuambia kwamba fainali za mwaka huu zilipaswa kufanyika Marekani na sio Qatar. Sio mbaya kutubu lakini tunafahamu hasemi neno jipya. Waingereza na watu wa mataifa mengine walipiga sana kelele kwa Blatter na wenzake wasipeleke kombe Qatar.

Kuikusanya dunia Qatar ni jambo la kushangaza. Nchi ambayo imepitwa kwa ukubwa na Wilaya Morogoro inaikaribisha dunia. Kuna timu 32 na mashabiki wake. Halafu kuna watalii ambao hawana timu zao lakini wanataka kwenda Qatar na ni haki yao ya msingi. Unawamudu vipi?

Matokeo yake na Dubai nayo imejaa. Bahraini nayo imekaa. Saudi Arabia nayo ni hivyo hivyo. Imefika mahala sasa wameamua kuleta meli ili watu wengine wakalale katika meli. Imefika mahala sasa kuna wakazi wa Qatar wanahamishwa kinguvu ili kupisha wageni. Hii sio haki.

Ninachofahamu ni kwamba Blatter na wahuni wenzake walifahamu yote haya isipokuwa nguvu ya pesa ilikuwa kubwa. Leo Blatter anatuambia kitu ambacho dunia ilifahamu mapema na wao walifahamu mapema. Sijui alidhani ni kitu gani kingebadilika katika nyakati hizi.

Leo Kombe la Dunia la Qatar litakuwa ghali kuliko michuano yoyote ya Kombe la Dunia iliyowahi kufanyika hapo awali. Chupa moja ya bia ni Pauni 10. Wageni wajiandae kunywa chupa moja ya bia kwa Sh 30,000. Wajiandae kula sambusa moja kwa Sh20,000.

Chumba kimoja kwa sasa kinafika Pauni 1,000 kwa siku. Hata vyumba vya melini ndio bei zake. Yote haya yanasababishwa na ukweli kwamba Waarabu wa Qatar wamelipeleka Kombe la Dunia sebuleni kwao. Wana uwezo wa kumudu gharama hizi hata kama wageni hawatakuja. Wana utajiri huo.

Waarabu wenyewe wa falme za Kiarabu wana uwezo wa kuchukua hoteli zote za Qatar na wakatazama mechi zote za Kombe la Dunia wenyewe. Nia yao kubwa ni kuwaona mastaa wakubwa wakicheza ndani ya ardhi yao. Pesa sio tatizo kwao. Lakini ukweli ni kwamba hii itakuwa adha kubwa kwa mashabiki mbalimbali.

Lakini pia sheria za Kiislamu zitaendelea kuchukua mkondo wake na nadhani kutakuwa na mvurugano mkubwa wa kiimani kati ya utawala wa Qatar na watu wa imani tofauti. Makundi ya mashabiki walevi na wapenda ngono wataingia katika mgogoro mkubwa na Serikali ya Qatar ambayo imeahidi kuendelea kutumia sharia.

Ukweli ni kwamba Kombe la Dunia linapaswa kufanyika katika nchi kama Marekani, Afrika Kusini, Uingereza, Brazil na mataifa mengine makubwa ambayo yamejitosheleza katika masuala ya huduma kwa wageni. Leo hata ukihamishia Kombe la Dunia Marekani wanaweza kuandaa bila ya kuhitaji muda mrefu wa maandalizi.

Rafiki zangu Warusi licha ya kwamba waliiba suala la maandalizi kutoka kwa Waingereza ambao walikuwa wapinzani wao wakuu katika mbio za kuwania uenyeji lakini walimudu na hakukuwa na malalamiko mengi kwa sababu Russia ni kubwa.

Lakini pia hakukuwa na mgongano wa kiimani na watu wa mataifa mengine. Nadhani wazo bora ambalo Blatter alipaswa kufanya ni kuhakikisha Kombe la Dunia la mwaka huu lingefanyika katika nchi nyingi za Falme za Kiarabu kwa pamoja. Labda nchi za Qatar, Oman, Dubai na Bahraini zingeandaa kwa pamoja. Ni nchi ambazo zipo karibu na walau ingeongeza ufanisi wa huduma.

Kinachochekesha ni kwamba Blatter na wenzake wakazipa nchi kubwa tatu, Marekani, Canada na Mexico kuandaa kwa pamoja fainali za Kombe la Dunia 2026. Hapo hapo kumbuka kwamba mara mbili, 1970 na 1986 Mexico pekee ilimudu kuandaa fainali mbili za kombe la dunia. Marekani peke yake ilifanikiwa mwaka 1994.

Blatter ametufanyia uhuni mwingi katika soka ingawa binafsi bado namkubali kwa kutoa upendeleo mwingi katika soka la Afrika. Ni kwa sababu alikuwa anazihitaji kura za Afrika kama dawa pindi chaguzi zake zilipokaribia.

Hata hivyo, miongoni mwa uhuni aliowahi kufanya ni huu hapa wa kuipa Qatar uenyeji halafu leo anajifanya anatubu.

Kitu pekee ambacho tutakiona katika fainali hizi ni ufahari wa Waarabu katika viwanja vya kisasa pamoja na hoteli zake.

Tutaona pia miundombinu ya kisasa ingawa haitasaidia kwa sababu vitu vyote hivi vitapatikana kwa uchache.

Columnist: Mwanaspoti