Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Biashara United na mwaka wa shetani

Mazoezi Biashara United (600 X 366) Kikosi cha Biashara United

Thu, 14 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya misimu minne kwenye Ligi Kuu hatimaye Biashara United ya Mara imeshuka rasmi daraja na kwenda Championship.

Dalili za kushuka zilianza kuonekana mapema kwani mambo mengi yakienda kombo kuanzia uwanjani, benchi la ufundi na uongozi na kusadifu msemo wa waswahili kuwa siku ya kufa nyani miti yote huteleza unaweza kuhitimisha kuwa ulikuwa mwaka wa shetani kutokana na yale iliyoyapitia, tofauti na msimu uliopita ikifanya vizuri na kushika nafasi ya nne kwenye ligi na kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kulikuwa na kila dalili za kushuka daraja;

USAJILI WA KUBAHATISHA

Katika dirisha kubwa la usajili kujiandaa na msimu timu hiyo iliwaleta nyota wapya ambao walikuwa na uwezo wa kawaida na walishindwa kuingia kikosi cha kwanza moja kwa moja na kutotoa msaada kwa kikosi hicho.

Iliwasajili Atupele Green aliyetemwa Geita Gold, Notikely Masasi na Aniceth Revocatus kutoka Mwadui iliyoshuka daraja, Kassim Mdoe kutoka Tanzania Prisons, Tayo Odongo na Opare Collins ambaye walau raundi ya pili alitoa msaada kwa timu.

Ilimchukua David Kameta kwa mkopo kutoka Simba lakini dirisha dogo akatimka zake Geita Gold, Omary Chibada kutoka Yanga na wengine huku ikiwaongezea mikataba Daniel Mgore, Ramadhan Chombo, Mpapi Nasibu na Leny Kissu.

UTULIVU BENCHI LA UFUNDI

Biashara United haikuwa na utulivu kwenye benchi lake la ufundi na imehitimisha msimu ikipita mikononi mwa makocha wakuu watatu, wasaidizi watatu na mameneja wawili wa timu katika vipindi tofauti.

Ilianza msimu na Mkenya, Patrick Odhiambo ambaye alijiunga nayo mwaka 2021 na kudumu kwa takribani miezi nane kabla ya kutimuliwa Januari, 2022, ikamchukuwa Mrundi, Vivier Bahati aliyepewa mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu.

Juni 6, mwaka huu Bahati akafungashiwa virago pamoja na msaidizi wake, Gilbert Daddy na meneja, Frank Wabare wakibakiza michezo minne kumaliza ligi na baadaye wakamchukuwa Khalid Adam, Omary Madenge na Omary Hamis ambao walianza kazi Juni 8 wakimalizia mechi nne zilizobaki na kuambulia ushindi mmoja, sare moja na kufungwa mbili wakishindwa kuinusuru timu hiyo isishuke daraja.

MAJERAHA

Majeraha yalikuwa moja ya vikwazo kwa timu hiyo ambapo wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza akiwemo kipa James Ssetuba, Ramadhan Chombo, Deogratias Mafie, Leny Kisu na Ambrose Awiyo walikumbwa na majeraha na kushindwa kuisaidia timu michezo mingi.

Inaweza isiwe sababu yenye mashiko lakini kuondoka kwa kinda, Denis Nkane aliyetimkia Yanga dirisha dogo huenda imechangia kuzorota kwa timu hiyo katika eneo la ushambuliaji huku ikishindwa kupata mbadala wake ambaye angetengeneza muunganiko hatari na Ramadhan Chombo na wenzake kama ilivyokuwamsimu uliopita na mwanzoni mwa msimu huu.

MATOKEO MABOVU

Tofauti na msimu uliopita ambao ilikuwa kwenye kilele cha ubora ikimaliza nafasi ya nne kwa kuvuna pointi 50 ikishinda mechi 13, sare 11 na kufungwa tisa, huku kipa wake, Mgore akiwa hajaruhusu bao katika mechi 11 kati ya 24 alizodaka mambo yako tofauti msimu huu.

Timu hiyo imeshinda michezo mitano pekee kati ya 30 ya ligi msimu huu ikishinda mmoja kwenye Uwanja wake wa Karume mkoani Mara, ikishinda mmoja ugenini huku ikishinda minne nyumbani.

Iliambulia sare 13 na kupoteza michezo 12, ikifunga mabao 23 na kufungwa 25 na kipa wake, Mgore aliambulia Cleensheet moja katika mechi saba alizodaka na kuondoa heshima iliyojengeka ya kuwa miongoni mwa timu za kuogopwa zikiwa nyumbani.

KATIBU AFUNGIWA

Wakati ikihaha kutafuta namna ya kujiokoa kwenye zahama ya kushuka daraja, ikapigwa tena na nyundo kichwani, Aprili 11 Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilimfungia katibu wa timu hiyo, Haji Mtete kutojihusisha na soka kwa miaka mitano.

Adhabu hiyo ilitolewa na kamati ya maadili ya TFF baada ya Katibu huyo kushindwa kutii maagizo ya FIFA kuhusu usajili wa wachezaji ndani ya klabu hiyo kufuatia shirikisho hilo kuizuia kusajili kuanzia dirisha dogo la Januari 2022 kutokana na kutomlipa mchezaji wake, Thimothy Omwenga aliyeishtaki.

Mambo yaliendelea kwenda kombo baada ya kushushiwa rungu lingine la kufungiwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA kusajili wachezaji kwa madirisha mawili baada ya kushindwa kuheshimu uamuzi wa awali wa FIFA ya kumlipa Omwenga.

UKATA/SAFARI YA LIBYA

Ukata ni moja ya sababu za kuvurunda kwa timu hiyo, inaelezwa wachezaji walikuwa wanadai mishahara ya miezi miwili na ada za uhamisho pamoja na maslahi mengine.

Hili linathibitishwa baada ya timu hiyo kushindwa kwenda nchini Libya Oktoba 22, 2021 kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli na kupelekea waarabu hao kupewa ushindi wa mezani na kufuzu hatua ya makundi na hatimaye kufika nusu fainali.

Kabla ya sakata hilo la Libya, klabu hiyo manusura ishindwe kwenda Djibouti kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya FC Dikhil na baadae ilifanikisha kwenda lakini ikafika siku ya mchezo huo.

Mmoja wa wachezaji (jina linahifadhiwa) anasema wachezaji wanaidai klabu mishahara ya miezi miwili pamoja na ada za uhamisho huku uongozi ukiwa kimya, akitahadharisha hali hiyo huenda ikawakimbiza nyota wengi kikosini hapo na kuiacha timu njia panda.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Salma Thabit anasema; “Timu ikishuka kila mtu anamtafuta mchawi nani, wachezaji watadai shida ni uongozi na wao watalaumu wachezaji, tuache yapite tukajipange upya hatukuwa bora tu msimu huu ukweli haupingiki,”.

Baada ya kuhitimisha mechi zake na kushuka daraja, uongozi wa klabu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii imewaomba radhi mashabiki wake kwa kilichotokea wakiangusha matumaini yao.

Kwa maoni yako ni nini kimeiponza Biashara msimu uliopita na kukumbana na majanga hayo makubwa yaliyowakuta. Tupe maoni yako.

Columnist: Mwanaspoti