Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Balozi Mahiga: Lulu iliyoondoka

43998 Pic+mahiga Balozi Mahiga: Lulu iliyoondoka

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

INAWEZEKANA watu wengi hawakumjua Balozi Augustine Mahiga kwa undani, kuhusu maisha yake, taaluma na utumishi wake kwa taifa, kikanda Afrika na kimataifa.

Kifo chake kilichotokea alfajiri ya Mei Mosi, mwaka huu nyumbani kwake mjini Dodoma, kimemuibua ‘Mahiga mpya’ katika fikra za watu, akiwa Mtanzania ambaye wasifu, salamu za rambirambi na mijadala iliyojikita kuanzia ngazi za msingi kwenye jamii hadi kimataifa, vimekuwa sehemu ya kudhihirisha kwamba nchi bado ina watu wanaoweza kuacha alama chanya duniani.

Balozi Mahiga aliyezaliwa Agosti 28, 1945 na kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kifo chake kimetokana na kuugua ghafla alfajiri ya Ijumaa iliyopita.

Rais John Magufuli ndiye aliyetangaza kifo cha Balozi Mahiga, kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.

Kwa masikitiko akamuelezea Mahiga kwamba alikuwa mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika nyanja za kimataifa kwa miaka mingi.

"Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa, alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nililomtuma," ameeleza Rais Magufuli katika salamu zake rasmi za rambirambi.

Rais Magufuli anasema kifo cha Balozi Mahiga kilitokea baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma na alifikishwa hospitalini akiwa tayari ameshafariki dunia.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, pamoja na mambo mengine anamtaja kama mzalendo wa kweli, aliyeitumikia nchi yake kwa uadilifu mkubwa.

Mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee, anaguswa na kifo hicho na kwa ufupi akaandika kupitia ukurasa wake wa twitter, "upumzike kwa amani Balozi Mahiga. Ulikuwa mtu mwema sana."

Kwenye Mahojiano na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kutokea jijini Dar es Salaam, Mbunge wa Kigoma Mjini -ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, anasema Mahiga hakuwa mtu mwenye kuweka kinyongo, bali kuitetea hoja yake katika mazingira yanayofikia ukomo wa kuelewana kwa pande husika.

Zitto anatoa mfano wa hoja moja aliyowahi ‘kumbana’ bungeni, lakini wakati wa mapumziko, Balozi Mahiga alimuita kwenye mgahawa wa bunge na kumpa maelezo ya ziada yaliyomridhisha.

Salamu za rambirambi zimetumwa kwa kutumia ukurasa wa twitter kutoka balozi za Uingereza, Canada, Ufaransa, Sweden na China, miongoni mwa nyingine.

UTUMISHI UN

Balozi Mahiga hakukumbukwa hapa nchini pekee, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ni miongoni mwa walioguswa na kifo chake akasema kupitia kwa msemaji wake, “tunahuzunishwa na kifo cha Balozi Mahiga na tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania na familia ya marehemu.”

Msemaji huyo, Stephane Dujarric, anawaambia waandishi wa habari kwa njia ya video jijini New York, Marekani, kwamba Guterres anamtambua Balozi Mahiga kwamba alikuwa mtumishi wa umma aliyekamilika, mwanadiplomasia aliyejizatiti hata aliposhika wadhifa wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia kati ya 2010 hadi 2013.

Kwa mujibu wa Guterres, wakati akihudumu kwenye jukumu hilo, Balozi Mahiga alikuwa na dhima ya msingi katika kusongesha uundwaji wa serikali ya Somalia na kusaidia kukamilisha Katiba ya muda na maandalizi ya uchaguzi nchini humo.

Mbali na uwakilishi huo, Balozi Mahiga alikuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye UN kati ya 2003 hadi 2010. Balozi Mahiga pia alifanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), akiongoza ofisi zake nchini Liberia, India, Italia, Malta, Vatican na San Marino huku akiratibu shughuli za shirika hilo katika ukanda wa maziwa makuu.

Kwa upande wake, shirika la habari la Uingereza (BBC), linamuelezea Balozi Mahiga kama mmoja kati ya watu wachache ambao wamefanya kazi katika ngazi za juu na awamu zote tano za serikali ya Tanzania, kutoka kwa Rais wa kwanza, hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi John Magufuli wa awamu ya tano.

Kwa mujibu wa BBC, licha ya utajiri wake wa maarifa na uzoefu mkubwa ndani na nje ya Tanzania, alikuwa mtu asiyejikweza kwa mamlaka na hivyo kuwa moja ya sababu ya kifo chake kuombolezwa sehemu nyingi duniani.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi nchini, Furaha Dimitri, anasema, taarifa za maisha ya Balozi Mahiga zinatolewa kama tunu iliyokuwa imefichwa, na sasa inaibuliwa kwa manufaa ya nchi.

“Nina hakika vijana wa kizazi cha hivi karibuni hawakuyajua mengi kumhusu Balozi Mahiga hadi mauti yalipomkuta, sasa ni vizuri kama taifa tukajenga mfumo wa kuwatambua watu wa aina yake na kuwatumia ipasavyo badala ya kusubiri hadi mauti yawakute,” anashauri.

Dimitri anasema, kifo cha Balozi Mahiga kinaweza kuwa sababu kwa taifa kuweka mfumo wa kuwatambua watu wenye taaluma na uzoefu katika ngazi tofauti, bila kuhusisha tofauti za aina yoyote zilizopo.

“Tunapoijenga nchi, hakuna sababu ya kuwaona hawa wa kule na wale wa huku, sote tunapaswa kuunganisha nguvu zetu na kutumia rasilimali wakiwamo wa aina ya Balozi Mahiga,” anasema.

MAJUKUMU MUHIMU

Mpaka anafariki alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi ambayo alikuwa akihudumu tangu Machi 2019.

Kabla ya hapo, Balozi Mahiga alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jukumu alilolishika tangu kuapishwa kwa baraza la kwanza la mawaziri la serikali ya awamu ya tano mwaka 2016.

Aliteuliwa kwenye nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kama mbunge wa kuteuliwa. Karibuni zilikuwapo habari kuwa alikuwa anajindaa kugombea ubunge Iringa Mjini.

Columnist: www.tanzaniaweb.live