Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bado Doumbia hajachelewa, tumsubiri

Mamadou Doumbia Gh Mamadou Doumbia akiwa na Rais wa Yanga, Hersi Said

Thu, 2 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mhuni mmoja akaamka asubuhi moja na kuamua kuichangamsha nchi kwa bando lake. Huenda Tanzania bando ni bei rahisi sana. Mhuni mmoja akazusha kwamba, beki mpya wa Yanga kutoka Mali, Mamadou Doumbia hana furaha katika kikosi cha Yanga na ameomba kuondoka. Nilicheka sana.

Sababu ya kumkosesha Doumbia furaha? Kwa sababu amekosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Nafahamu kwamba wachezaji wote duniani wanatamani kuwepo uwanjani na hawalifurahii benchi. Kuanzia Hispania kwa Eden Hazard hadi Tanzania kwa Erasto Nyoni hakuna mchezaji anayefurahia kuwa nje ya uwanja kwa sababu yoyote ile. Hivyo hakuna lolote jipya kwa Doumbia kuumizwa kwa kuwa nje ya kikosi ya kikosi cha Yanga.

Kilichonichekesha kutoka kwa mwanzilishi wa taarifa ile ni pale aliposema Doumbia ameomba kuondoka Yanga. Inawezekana ni kweli Doumbia halifurahii benchi la Yanga, lakini sidhani kama amefikia hatua ya kuomba kuondoka. Nitaeleza kwanini.

Kwanza Doumbia ana muda gani tangu atue nchini? Hajamaliza miezi miwili. Yanga wamecheza mechi ngapi tangu afike? Kwa haraka haraka hazifiki mechi 10.

Katika timu ngeni, ligi ngeni na nchi ya ugenini ambayo inazungumza lugha ngeni unahitaji muda kuzoea. Nina uhakika Doumbia anafahamu hili na hata kabla hajatua nchini lazima hilo lilikuwepo katika mawazo yake. Huwezi kutegemea mazingira rahisi ugenini. Kuomba kuondoka baada ya miezi miwili tu haliwezi kuwa kichwani mwake.

Lakini hapohapo Doumbia mwenyewe atakuwa anafahamu kwamba sio rahisi kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha timu uliyoikuta katikati ya msimu, tena ikiwa inafanya vyema. Kumbuka kwamba ameingia Yanga ikiwa kileleni katika msimamo wa ligi - tena ikiwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ingekuwa rahisi kwa kocha wa Yanga kufikiria kumuingiza katika kikosi chake kwa haraka kama Yanga ingekuwa na matatizo ya kiulinzi au inapata matokeo mabaya. Bahati mbaya amekuta Yanga ina mabeki wawili imara wa katikati wanaoanza na wengine wawili wanaokaa katika benchi.

Bila shaka, Doumbia mwenyewe atakuwa anatazama hivi vyote na kuelewa kwanini hapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga. Kwa sasa anachohitaji ni kubeba moyo halisi wa watu wa kwao.

Nilipata bahati ya kufika Afrika Magharibi mara kadhaa. Nafahamu watu wa kule. Ni watu jasiri wanaothubutu kupambana na maisha. Ndiyo maana wanapopata bahati ya kucheza soka, huwa wanajitoa kucheza kwa asilimia zote ili wachume noti za kutosha kisha warejee kubadilisha maisha kwao.

Hawaishi kijamaa sana kama huku kwetu. Pengine ndiyo sababu wana mioyo migumu ya kupambana. Haishangazi kuwaona wachezaji wao wengi wanatafuta maisha nje ya nchi zao. Huwa hawaumizwi sana na mazingira. Ni wapambanaji. Jiulize Victor Akpan alisafiri vipi kutoka Nigeria kuja kucheza ligi ya Zanzibar. Wapo vijana wangapi waliokosa nafasi katika timu za Tanzania Bara ambao wangeweza kucheza Zanzibar lakini hawapo tayari?

Simfahamu Doumbia, lakini historia yake inaniambia aliwahi kuondoka Mali kwenda kucheza katika ligi za chini Morocco akiwa kijana mdogo. Ni ujasiri kama huu anauhitaji katika Yanga ili kupambana kupata nafasi ili ajiweke katika mazingira ya kuchuma pesa za soka zaidi.

Nina uhakika Yanga wanampatia pesa maradufu zaidi ya zile alizokuwa anapokea nchini kwao ndiyo sababu amekubali kuja nchini. Anahitaji kuendelea

kuchuma hizi noti kwa miaka sita au saba ijayo atakapotimiza miaka 34. Uzuri wa nchi yetu wachezaji waliowahi kufanya vizuri zamani huwa hawakosi timu hadi waamue wenyewe.

Ili afanikiwe katika hilo mchezaji huyo anapaswa kuwa uwanjani sasa hivi na kufanya vyema Yanga.

Binafsi sina wasiwasi na uwezo wake. Nilimtazama katika michuano ya Chan. Ni beki imara ambaye Yanga wanamhitaji. Kikubwa anachohitaji ni kukomaa kuzoea mazingira haraka na kuhakikisha anamchomoa Yanick Bangala au Dickson Job katika ule ukuta wa Yanga.

Sio kazi rahisi sana lakini inawezekana. Unakumbuka Lomalisa alivyoanza Yanga?

Columnist: Mwanaspoti