Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

BMU zilivyopandisha mapato halmashauri ya Pangani

C5d6ec25a63fade4aefe961b7c084e95 BMU zilivyopandisha mapato halmashauri ya Pangani

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TUNAPOZUNGUMZA maendeleo ya miundumbinu, afya, elimu na huduma zingine za jamii katika nchi yetu suala la uwepo wa usahihi katika ukusanyaji wa mapato kupitia kodi, tozo na ushuru mbalimbali huwa la muhimu sana.

Ili ufikie malengo hayo na ufanikiwe katika kukusanya mapato na ushuru huna budi kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa ukusanyaji wa mapato na ushirikishwaji wa jamii na kuonesha uwazi na matokeo ya unachokikusanya.

Katika kuliona hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imepiga hatua kubwa katika makusanyo ya mazao na rasilimali za bahari, shukrani kubwa ziviendee Vikundi Shirikishi vya Usimamizi wa Rasilimali za Bahari (BMU).

Vikundi hivi shirikishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani vilianzishwa kupitia mradi wa MACEMP mwaka 2009 huku utendaji wake ukizingatia sera ya uvuvi na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 pamoja na mwongozo wa kitaifa wa BMU wa mwaka 2005.

Wilayani Pangani vikundi hivyo ambavyo vimeundwa katika ngazi ya vijiji vinafanya kazi katika vijiji 12 vya ukanda wa bahari wenye urefu wa kilometa za mraba 127.

Wilaya ya Pangani ni moja kati ya Wilaya nane za mkoa wa Tanga. Ni wilaya kongwe iliyoanzishwa mwaka 1950 na mkuu wa kwanza kabisa wa wilaya hiyo akiwa marehemu Mrisho Kikwete, baba yake Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Mbali na rasilimali zinazotokana na mazao ya bahari ambazo makala haya yanaziangazia zaidi, vyanzo vingine vya mapato katika wilaya hiyo ambayo kwa upande wa Kusini Mashariki inapakana na Bahari ya Hindi ni kilimo, utalii na biashara.

Kwa upande wa makusanyo ya mapato katika sekta ya mazao na rasilimali za bahari, wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka sita imefanikiwa kukusanya Sh milioni 256.8 mwaka 2018 kutoka Sh milioni 23.8 mwaka 2016.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Issaya Mbeje, anasema kuwa siri ya makusanyo ya ushuru wa mazao ya bahari kupanda ni kutokana na kutumia vizuri BMU.

Mbenje amebainisha hayo alipofanya nazungumza na ujumbe wa vikundi vya BMU kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Chandika Dismas Chandika, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira wa Halmashauri hiyo.

Ujumbe huo ulifanya ziara ya siku moja ambayo imedhaminiwa kupitia Mradi wa Udhibiti Uvuvi na Maendeleo shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Tanzania bara, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Mbali na Tanzania, mradi wa SWIOFish pia unatekelezwa katika nchi za Msumbiji na Comoro.

Anasema kuwa wilayani humo kuna maeneo manne ambao vikundi hivyo vinafanya kazi katika vijiji 12 katika ukanda ambayo ni Mkwaja, Kipumbwi, Pangani Mashariki na Pangani Magharibi.

Mbenje anabainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2014/15 walipoanza kutumia BMU katika kukusanya mapato walipata Sh milioni 23.8, mwaka 2016 wakafikia Sh milioni 35,517,290, mwaka 2016/17 Sh milioni 128,178.567 na mwaka 2017/18 mapato yalipanda hadi kufikia Sh milioni 256.8.

Anasema katika mwaka wa fedha 2018/19 baraza la madiwani katika halmashauri hiyo liliamua kubadilisha wakusanyaji na kuwapa kazi hiyo maofisa watendaji wa vijiji ambapo walikusanya Sh milioni 162.051,600 lakini mwaka 2019/20 mapato yalishuka hadi Sh milioni 137,354,125.

“Utaona miaka ya nyuma wakati tuanaanza kukusanya mapato ya mazao ya bahari tuliwatumia BMU mapato yalikuwa yanapanda lakini walipopewa watendaji wa vijiji mapato yalipanda kisha yakashuka. Baraza la madiwani likaona bora tuwatumie tena BMU ambao wanafanya kazi kubwa kupitia serikali za vijiji husika. Hivyo tumezifufua tena BMU na kuwajengea uwezo na kuwapa mafunzo ya kukusanya mapato kupitia shirika la SeaSense,” anasema.

Anasema katika kipindi cha kuanzia Julai 1, 2020 hadi Januari 2021 tumefanikiwa kukusanya Sh milioni 93 na BMU wakishakusanya mapato tunawapa kamisheni ya asilimia 10.

Mwenyekiti wa BMU Pangani Magharibi, John Baya, anasema kuwa safari ya kuanza kukusanya mapato ilianza mwaka 2014 kwa majaribio ya muda wa miezi sita ambapo walifanya vizuri, ndipo baraza la madiwani wakaona wawape kazi hiyo kabla ya baadae kuwapa watendaji wa vijiji na kisha kuwarudisha tena.

Anafafanua kuwa siri kubwa ya mafanikio ya BMU katika kukusanya mapato ni kushirikisha wajumbe wote pamoja na kutoa elimu kwa jamii kijijini kuhusu umuhimu wa kukusanya mapato.

Anasema wengi wanatoa ushirikiano kutoka katika asilimia 10 wanayopata na hivyo asilimia tano wanairudisha kijijini ili kusaidia kuduma za jamii.

“Tunapokusanya ushuru tunashirikisha jamii katika kijiji husika pamoja wajumbe wote wa BMU na kutoa elimu hivyo hawakwepi ushuru na wavuvi wenyewe tunawaelimisha faida ya ushuru kwani pia unawasaidia wenyewe na wanatuelewa,” anasema.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Chandika anasema kuwa kupitia BMU za Pangani wamefurahi kujifunza kitu hususani jinsi halmashauri hiyo ilivyoweza kufanikiwa kukusanya mapato ya mazao ya bahari kupitia BMU.

Chandika anaahidi kwenda kutoa elimu kwa madiwani wa Bagamoyo na kuona namna wanavyoweza kutumia BMU katika kukusanya mapato yatokanayo na rasilimali za bahari.

Kwa upande wake, Adhri Mohamedi, mvuvi katika eneo la Kipumbwi, anabainisha faida wanazozipata kupitia BMU kuwa ni pamoja na kupewa msaada pindi wanapopata majanga.

“Tunapotoa mapato faida nyingine inarudi kwetu, kwa mfano hivi karibuni kuna mvuvi mwenzetu alipotea lakini tulitoa taarifa BMU walitusaida fedha na mafuta hadi tukafanikiwa kumpata,” anasema.

Columnist: www.habarileo.co.tz