Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

BANDARI ZETU, MAENDELEO YETU

4d73f4eff6ad56a04ad6dae899f5d0cb BANDARI ZETU, MAENDELEO YETU

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Bandari ni moyo wa taifa letu

KUANZIA wiki hii tutakuwa tunawaletea makala kuhusu 'Bandari Zetu, Maendeleo Yetu'. Kwa kuanzia tunawaletea makala kuhusu mambo muhimu ya kujua kuhusu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kama yalivyowahi kuelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko katika mahojiano na gazeti hili.

Bandari nini?

Bandari ni eneo lolote lile ambalo chombo cha majini, hata kama ni mtumbwi, kinakwenda. Chombo hicho kinaweza kwenda hapo kwa madhumuni ya kufanya biashara lakini pia inaweza kuwa kwa sababu ya kujihifadhi dhidi ya upepo mkali. Kipindi kile chombo kimesimama pale, kwa mujibu wa sheria, eneo hilo ni bandari.

Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mahali popote ambapo vyombo vya majini vinakwenda na kusimama kwa ajili ya biashara au shughuli nyingine panatakiwa kuwa chini ya TPA.

Hivyo kwa mujibu wa sheria, kila bandari nchini ni sehemu ya TPA na hivyo zinazoitwa bandari haramu au bandari bubu ni zile ambazo watu wanaanzisha bila kujua sheria inasemaje.

Kwa bahati mbaya, baadhi ya taasisi za umma nazo huanzisha bandari bila kuwa na uelewa kuhusu sheria inasema nini. Ni kwa mantiki hiyo, kila aliyeanzisha bandari au anayetia nanga kwenye bandari yoyote, ajiulize kama yuko pale kisheria au la. Ili mtu atambulike kwamba yupo kwenye eneo hilo kisheria ni pale atakapojiridhisha kwamba liko chini ya TPA.

Majukumu ya bandari

Kutokana na maana ya bandari kama tulivyoona hapo juu, moja ya jukumu kubwa la TPA ni kujenga, kusimamia na kuendeleza bandari kwenye bahari, maziwa na mito.

TPA imekuwa ikifanya kazi hiyo kwenye bahari na kwenye maziwa yetu, hasa yale makubwa kama Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Kwa mantiki hiyo, bandari inaweza kujengwa na kuendelezwa na TPA, lakini inaweza ikawa imejengwa na kuendelezwa na mamlaka nyingine lakini usimamizi kisheria unapaswa kuwa chini ya TPA.

Kazi nyingine ya TPA mbali na kujenga bandari ni kuzifanya matengenezo, kuzikarabati na kuzipanua. Katika makala zinazofuata tutaangalia namna bandari za Tanzania zilivyopanuliwa na zinavyoendelea kuboreshwa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani.

Kazi nyingine ya TPA ni kusimamia na kuendesha bandari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Kazi meli inapoingia

Kazi moja kubwa ya TPA ni kupokea chombo cha majini kutoka kinakotoka, yaani iwe meli au boti au kukiaga chombo kuelekea kule kinakokwenda. Hatua hii pia huzalisha kazi nyingine kadhaa.

Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa zinazosimamia biashara ya bandari, meli ikikaribia bandarini inachukuliwa na mabaharia wetu na hivyo nahodha anayekuja na meli, haruhusiwi kuingiza meli gatini.

Meli ikishafika gatini, kazi ya pili ya bandari baada ya kuipokea ni kuifunga, kuhakikisha kwamba hata upepo wa namna gani ukija meli haitikisiki.

Meli ikishafungwa, wadau mbalimbali huanza majukumu yao. Kwa mfano, watu kutoka Idara ya Uhamiaji huingia kwenye meli, watu kutoka Wizara ya Afya nao huingia kuhakikisha kwamba wale wote wanaokuja nchini wako salama kiafya na kufuatia wadau wengine kutegemeana aina ya bidhaa inayotarajiwa kuingia au kupitia nchini kwenda nchi zingine.

Baada hapo kazi ya kupakua mizigo au shehena huanza. Kazi nyingine inayofanywa na bandari ni kutunza mizigo na kufanya mawasiliano yote kipindi ambacho malipo yanakuwa yakifanywa na mawakala mbalimbali.

TPA ilianzishwa lini?

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ni mtoto wa iliyokuwa Tanzania Harbors Authority (THA).

Mamlaka hii ilianzishwa rasmi Aprili 12 mwaka 2005 baada ya kufutwa kwa sheria iliyoanzishwa THA namba 12 yua mwaka 1977 na kutungwa kwa sheria ya TPA namba 17 ya mwaka 2004.

Ikumbukwe kwamba THA ilizaliwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilikuwa na mamlaka za huduma za pamoja za Afrika ya Mashariki. Huduma hizo hazikuhusisha bandari pekee bali pia njia nyingine za uchukuzi na mawasiliano kama vile reli na posta.

Serikali iliamua kuanzisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kupitia sheria hiyo namba 17 ili kuleta ufanisi zaidi.

Kwa msingi huo, Aprili 12 mwaka kesho, TPA itakuwa inafikisha miaka 16 tangu kuanzishwa kwake.

Bandari kubwa nchini

Bandari kubwa kabisa nchini ambayo ukitaja bandari watu wanajua ni hiyo kwa sababu ndio lango kuu, ni Bandari ya Dar es Salaam.

Inakadiriwa kwamba asilimia 95 ya biashara yote ya bandari nchini inahusisha bandari hiyo. Bandari inayofuata kwa ukubwa ni ya Tanga kisha inakuja bandari ya Mtwara.

Tanzania pia ina bandari katika maziwa, kwa mfano Ziwa Victoria, kuna bandari ya Mwanza Kaskazini na Mwanza Kusini, lakini pia kuna bandari za kati katika maeneo mengine katika ziwa hilo kama vile Bukoba, Nansio (Ukerewe), Musoma na Kemondo.

Kuna bandari kadhaa pia katika Ziwa Tanganyika kama vile Kipili, Kasanga, Kabwe, Kibirizi na kadhalika lakini kubwa ni ile ya Kigoma.

Vivyo hivyo, kuna bandari kadhaa katika Ziwa Nyasa kubwa ikiwa ni iliyoko Kiwira wilayani Kyela na ile ya Kusini ya Mbamba Bay.

Tukirudi tena kwenye mwambao wa bahari ya Hindi kuna bandari kadhaa zenye ukubwa wa kati kama vile bandari ya Pangani ambayo iko katika mkoa huo wa Tanga.

Na upande wa Dar es Salaam, kuna bandari ya Bagamoyo na bandari nyingine ya mwekezaji ilioko Mbegani. Lakini pia kuna bandari ya Lindi, Kilwa Masoko, Mafia Kisiwani na bandari ya Kwale.

Umuhimu wa bandari

Bandari ni sawa na moyo wa Taifa kutokana na kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato vya taifa. Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na bandari katika bahari na maziwa.

Ziko nchi kama Singapore ambazo maisha yao wanategemea bandari kama chanzo muhimu kabisa cha mapato na Tanzania ya Magufuli inajielekeza huko.

Kijiogarafia Tanzania ndio nchi inayoongoza, kama siyo duniani basi ni Afrika kwa kuzungukwa na nchi nyingi.

Kwa upande wake wa mashariki, ziko biashara za dunia. Kuna nchi za Mashariki ya Kati, India, China na Japan, zote ziko upande huo wa mashariki na hivyo biashara zao ni rahisi kupitia Tanzania kwa njia ya bahari kwenda katika nchi nyingine.

Lakini Tanzania inapakana pia na nchi kadhaa upande wa kaskazini, magharibi na kusini wakiwemo hata tunaoshindana nao katika biashara ya bandari ambao nchi wanazopakana nazo hazizidi tatu.

Ukienda hadi kusini mwa bara hili bado utaona Tanzania inaongoza kwa kuwa na nchi nyingi tunazopakana nazo. Kwa uchache unakuta kuna nchi sita tunazopakana nazo.

Tukutane wiki ijayo kuendelea na makala maalumu kuhusu TPA na bandari zetu.

Columnist: habarileo.co.tz