Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

BANDA: Huku Sauzi kila mtu kivyake, ila kutamu

Abdi Banda Chippa Utd.jpeg Abdi Banda

Sun, 25 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiachana na elimu ya darasani, mazingira na kutembea sehemu mbalimbali ni mafunzo tosha katika maisha kama anavyoeleza beki Mtanzania, Abdi Banda anayekipiga Chippa United ya Afrika Kusini.

Banda ambaye ni mzoefu na ligi ya Afrika Kusini, kabla ya kujiunga na Chippa United (2022) aliwahi kuzichezea Baroka (2017- 2019), kisha Highland Park (2019/20), kisha alirejea Tanzania kujipanga upya, akajiunga na Mtibwa Sugar aliyoitumikia msimu uliopita.

Beki huyo ambaye aliwahi kuitumikia Coastal Union (2012-2014), Simba (2014-2017) na Taifa Stars kwa nyakati tofauti, anakiri kujifunza mambo mengi ya soka na maisha ya kawaida na amekuwa mtu asiyekata tamaa, akiamini kwa mapenzi ya Mungu atakuja kuishi katika uhalisia wa maisha ambayo yapo kwenye fikra zake.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti amezungumzia maisha yake ya nje na akisisitiza ni mwiko kukata tamaa ungali uhai, akiapa kupambana hadi dakika ya mwisho ili kufikia malengo yake.

“Kabla ya kurejea nyumbani na kujiunga na Mtibwa Sugar niliyoitumikia mwaka mmoja, nilikaa nje miezi sita na wengi wao walijua ndio mwisho wangu, kuna wakati hata ukipita mtaani unasikia watu wakisema yaani jamaa kalewa sifa soka limemshinda kazi yake kuzurura tu, nilikuwa nanyamaza na sasa wanaona kwa macho nilichokuwa nakifikiria kwa wakati huo.

“Pamoja na hayo yote sikuwahi kukata tamaa, ndio maana kwenye mkataba wangu wa Mtibwa Sugar niliweka kipengele cha kama nitapata timu nje, nitaondoka, nashukuru sana uongozi ulikuwa na ushirikiano mkubwa na mimi na ni timu iliyonisaidia kunipandisha kiwango na kurejea mchezoni.”

MAISHA YA UGHAIBUNI

Anasema maisha ya huko ni ghali, ila kwa sababu aliwahi kuishi awali hayamsumbui, kila kitu anakiona cha kawaida kabisa na hayazuii chochote kutimiza ndoto zake za soka na anapata morali ya kujituma kwa bidii kulingana na aina ya wachezaji alionao kwenye timu.

HAWAKAI KAMBINI Anasema kila mchezaji anakaa kwake, isipokuwa kama wakienda kucheza mbali ndipo wanakaa pamoja kwa muda na baada ya kumaliza majukumu yao kila mmoja anarejea anakoishi.

“Mimi naishi kwenye appartment ambayo nimeichagua mwenyewe, ipo mji wa Port Elizabeth karibu na ufukweni ili familia ikiwa huku isitembee umbali mrefu endapo ikitaka kuja uwanjani kunisapoti na nipo mjini kabisa.

“Timu ndio imenilipia kodi, inalipa wafanyakazi wa usafi wa mazingira ingawa chakula najitegemea mwenyewe na kinapatikana kila kitu kama dagaa, kuku wa kienyeji, bamia vinatoka Msumbiji na Zambia ni bei ya kawaida, ingawa vilevile vipo vya bei juu, mara nyingi mke wangu akija kutembea ndiye anapika, mimi ni mara moja moja huwa nanunua maana nakuwa na muda mchache sana.”

KAMA MFALME

Banda anasema kuna gari maalumu la kumpeleka mazoezini na kumrejesha anapoishi. “Kuna dreva anayeniendesha kwenda mazoezini, hivyo sijapewa gari moja kwa moja, lakini sipati shida kabisa maana kila kitu kinafanyika kwa muda sahihi kabisa.”

Anasema kitu kikubwa alichojifunza hakuna mchezaji anayesukumwa kufanya majukumu yake, kutokana na kutimiziwa kila kitu kwa wakati, hivyo kila mmoja anakuwa anatambua wajibu wake na kujichunga mwenyewe na hiyo ndio sababu ya kuwaachia huru bila kuweka kambi.

“Ukifanya vitu vya hovyo unakuwa unajidanganya mwenyewe kwa sababu mwisho wa yote kocha anakuwa anataka uisaidie timu kwa kiwango kikubwa, hivyo lazima nipambane kwani nimekuja kutafuta kwenye nchi ya watu na siyo kutalii,” anasema.

THAMANI SAWA

“Kiukweli huku maproo wanatuchukulia kawaida sana hatuna tofauti na wazawa, ingawa hiyo ni kama kengele kwa mgeni kufanya kazi zaidi ili kuendelea kusalia kwenye timu, ila ukitukuta mazoezini ama ninapokaa huwezi kuona tofauti yoyote.

“Wanachotaka ni kazi na siyo kunyenyekewa nje ya uwanja, tofauti na nyumbani Tanzania ambako mgeni anapewa thamani kubwa zaidi ya mzawa kwa maana ya aina ya sehemu wanazokaa, malipo, hivyo wakibadilika katika hilo litaongeza ushindani, kwa sababu hilo linawavunja moyo wachezaji wanapoona wanafanya kazi sawa ila mwingine anaonekana muhimu zaidi.”

Anasema katika ligi hiyo, mchezaji akifanya vizuri wanampongeza na siyo kumfanya mfalme zaidi ya wengine na kwamba kila mtu ana mambo yake hakuna anayeshughulika na mtu mwingine.

Jambo jingine ni kuhusu imani yake (Muislam) anaeleza kwamba hapati shida ya kuswali kwani inapofika muda wanaheshimu na kuwaacha waabudu.

Columnist: Mwanaspoti