Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Azam usingizi wa kibongo, ndoto za kizungu

Azam Tanga Azam usingizi wa kibongo, ndoto za kizungu

Wed, 9 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwenye moja ya simulizi zake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutoa kisa kimoja cha Sir George Kahama, mmoja wa mawaziri wa serikali ya kwanza baada ya uhuru, akihudumu kama waziri wa mambo ya ndani ya nchi.

Mwalimu alisema kwamba siku moja walikuwa kwenye ndege wakisafiri kikazi. Huko angani ndege ikayumba kidogo, Sir George Kahama akasema ‘My God‘.

Ndege ikatulia na safari ikaendelea vizuri. Ghafla ikayumba tena, Sir George Kahama akasema, ‘Mungu wangu’.

Hali ikatulia na wakaendelea na safari. Ndege ikayumba tena kwa mara ya tatu, na Sir George Kahama akasema ‘mama yangu’.

Somo linalopatikana hapa ni kwamba katika hali ya utulivu na amani, kila mtu ni wa kisasa lakini katika hali ngumu kupitiliza, kila mtu hukumbuka asili yake.

Sir George Kahama alianza na uzungu, ‘My God’, akaja na uswahili, ‘Mungu wangu’, kisha akamalizia kwa kihaya, na ‘mama yangu’

Hapa ndipo unapokuja msemo wa Kiswahili unaosema kwamba hata uwe msomi vipi, huwezi kuota ndoto za Kiingereza.

Au kama alivyosema Mjomba Mrisho Mpoto kwamba huwezi kwenda kwa jirani kama hutokei kwako.

Na hii ndiyo sababu ya makala hii ya leo ambayo itazungumzia kinachoendelea pale Azam Complex Chamazi, makao makuu ya klabu ya Azam.

Kwenye kuta za vyumba vya wachezaji, kumewekwa picha za wachezaji wa Ulaya pamoja na nukuu zao mbalimbali.

Kuna picha zaidi ya 30 lakini hakuna hata moja ya mchezaji wao yeyote.

Hivi Azam FC kweli hawana mtu ambaye angeweza kunukuliwa na kuwa mfano kwa wachezaji waliopo?

Azam FC haijazalisha mashujaa wake ambao wanaweza kutumika kama funzo kwa kizazi cha sasa?

Mbaya zaidi nukuu walizoweka zote ni za Kiingereza, hakuna hata moja ya Kiswahili.

Hivi wanaamini kweli kwamba wachezaji wao wote wanaweza kuelewa maana ya kilichoandikwa?

Mojawapo wa nukuu walizoweka ni ya Zinedine Zidane, nyota wa zamani wa Ufaransa.

Katika maisha yake yote, Zidane hajawahi kujua kuongea Kiingereza, yeye anajua Kifaransa, Kiitaliana na Kihispaniola.

Kwa maana hiyo Azam FC wameikuta nukuu hiyo kwa mtu ambaye aliitafsiri kutoka moja ya lugha hizo na kuiweka kwa Kiingereza.

Sasa kama ni hivyo kwanini na wao wasiitafsiri kwa Kiswahili ili ujumbe ufike kwa wachezaji wao?

Hapa ndipo kwenye kiini cha andiko hili...Azam wanataka kuota ndoto za Kizungu ilhali wanalala usingizi wa Kiswahili.

Hii inanikumbusha kauli ya mmiliki wa zamani wa Liverpool, John W. Henry, alipowapiga dongo Arsenal mwaka 2013.

Washika bunduki hao walitaka kumnunua mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez kutoka Liverpool.

Mkataba wa Suarez na Liverpool ulisema endapo timu inayoshiriki ligi ya mabingwa ikija na zaidi ya pauni milioni 40, inaweza kumnunua mchezaji huyo.

Kwa hiyo Arsenal ikapeleka pauni milioni 40 halafu wakaongeza pauni moja. Yaani ikawa Pauni 40,000,001.

Yaani hiyo moja ndiyo iwe zaidi ya milioni 40.

Hapo ndipo John W. Henry akakimbilia Twitter na kuuliza,

“What do you think they’re smoking over there at Emirates?”

Hivi unadhani wanavuta nini pale Emirates?

Na mimi ndiyo najiuliza hapa, hivi unadhani wanavuta nini pale Chamazi?

Wanashindwa kujua kwamba heshima yao ipo kwa mashujaa wao zaidi kuliko kina Mbappe?

Wamewakumbuka hadi wachezaji wa mpira wa kikapu kama Steph Curry, lakini hawajamkumbuka Aggrey Morris.

Tena kwa Aggrey Morris kuna jambo jingine muhimu. Ni mchezaji wao aliyeitumikia timu hiyo kwa zaidi ya miaka 10, lakini ameondoka kimya kimya kama mtoto wa akademi.

Wameshindwa kumfanyia tukio maalumu la kumuaga kwa heshima, lakini wameweza kuwaenzi wachezaji ambao hawajawahi hata kufika Tanzania.

Tunajua na tunaikubali sana Azam FC kama klabu inayotuletea maendeleo makubwa ya mpira Tanzania.

Lakini inapotoka nje ya mstari kama hivi lazima tuikumbushe.

Watengeneze ndoto zao ili waziishi, hawawezi kufanikiwa kwa kuishi kwenye ndoto za watu wengine, tena wa Ulaya.

Kwa mfano, katika nukuu hizo, Didier Drogba anasema:

Dream as if you will live forever, live as if you are going to die today.

Ota kama utaishi milele, ishi kama utakufa leo.

Sawa, huu ni ujumbe mzuri, lakini Himid Mao angehojiwa, asingeweza kutoa ujumbe wa maana ambao ungeishi maisha ya kiazam?

Ina maana Azam haiwaamini kabisa wachezaji wake wa zamani kwamba wanaweza kusema kitu na kikaishi kwenye nyoyo za wachezaji wao wa sasa?

Hivi kweli Kipre Tchetche hawezi kuwa mfano kwa Idd Nado?

Nadhani hapo wamekosea sana. Wazo lilikuwa zuri lakini utekelezaji wake umekuwa mbaya.

Walipaswa waifanye kuwa ya kwao. Wangenukuliwa wachezaji wao waliowapa ubingwa pekee wa Ligi Kuu.

Anukuliwe Gaundence Mwaikimba, mmoja wa wafungaji wa mabao yaliyowapa ubingwa pale Sokoine Mbeya ile jioni ya Aprili 14.

Anukuliwa Mrisho Ngassa, mchezaji wa kwanza wa Azam FC kuwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu.

Anukuliwe Mohamed Seif ‘King’, kocha wa Azam FC tangu inaanzishwa hadi inapanda Ligi Kuu.

Wachezaji wapya wanaosajiliwa au watoto wa akademi wanaokua pale wanatakiwa kuwajua mashujaa wa klabu yao...lakini wanawaona kina Zidane, kina Mbappe na kina Serena Williams.

Ni kweli watu hao ni mfano wa kupigwa na wameongea maneno mazuri sana...lakini tatizo ni kwamba kwa tabia zetu za Kiswahili, wachezaji wetu wanaweza kuona kama huo ujumbe ni wa Ulaya zaidi kuliko Tanzania, kuliko Afrika.

Azam FC iache kuota ndoto za Kizungu kama iko Ulaya ilhali inalala ndoto za Kiswahili pale Chamazi.

Columnist: www.tanzaniaweb.live