Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Azam Shirikisho safari hii ngoma ilikuwa ya kibabe sana

Clement Fr Mzize Azam Shirikisho safari hii ngoma ilikuwa ya kibabe sana

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Unaweza kusema ilikuwa raundi ya pili ya weka niweke kwenye Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) kutokana na mvua ya mabao iliyonyesha kwenye zaidi ya viwanja 10 huku miamba ya soka la Tanzania Simba, Yanga na Azam FC zikionyesha zipo siriazi.

Tofauti na misimu kadhaa nyuma ambapo nguvu ya ushiriki kwa Simba na Yanga hasa katika hatua za namna hii kuwa ndogo, safari hii wameonyesha kuanza kiaina yake kutokana na vipigo vizito walivyotoa kwenye michezo yao huku wakishuhudiwa washambuliaji wao, Moses Phiri (Simba) na Clement Mzize (Yanga) kila mmoja akitupia mabao manne.

Kama kuna kulala na viatu basi mabeki wa Kurugenzi iliyopo Daraja la Pili maarufu kwa sasa kama First League walilala navyo kutokana na kipigo cha mabao 8-0 ambacho walikumbana nacho dhidi ya Yanga huku wajeda nao, Eagle FC wakipigwa mabao 8-0 dhidi ya Simba ambao walitumia silaha zao muhimu kwenye mchezo huo, wakati pia Azam FC ilitoa kipigo kizito zaidi cha mabao 9-0 dhidi ya Malimao FC.

Huu ndio utamu ambao ulishuhudiwa kwenye ruandi ya pili ya ASFC kuanzia Desemba 8 hadi juzi, Jumatatu ambapo zilishuhudiwa Mbeya Kwanza na Pan African zilizokuwa ugenini zikitinga raundi ya tatu ambapo zitaungana na timu nyingine 30 ili kukamilisha idadi ya timu 32 katika hatua hiyo.

HAT-TRICK ZA KUMWAGA

Kulikuwa na hat-trick sita zilizofungwa na mastaa mbalimbali wa Ligi Kuu huku Adrew Sinchimba wa Ihefu akiwa baba lao kwa kuweka kambani mabao matano dhidi ya Mtama Boys akiwazidi kete Richardson Ngíondya wa Mbeya City, Sadala Lipangile wa KMC, Phiri wa Simba na Mzize wa Yanga ambao kila mmoja alitupia mabao manne.

Ngíondya alitupia mabao manne kwenye mchezo dhidi ya Stand FC wakati chama lake likiibuka na ushindi wa mabao 5-1, Phiri alimjibu kwenye mchezo wa Simba dhidi ya dhidi Eagle FC. Mzize alifunga mabao manne dhidi ya Kurugenzi FC, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kinda huyo kufunga mabao matatu au zaidi kwenye mchezo mmoja wa ushindani akiwa na kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Nyota wa KMC, Sadala Lipangile naye alitupia mabao manne katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya Tunduru Korosho timu yake ikiibuka na ushindi wa 6-1. Mgunda wa Tanzania Prisons aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Misitu huku yeye akitupia mpira kambani mara tatu.

VIPIGO VIZITO

Azam FC na Ihefu ndizo timu ambazo zilizotoa vipigo vizito zaidi kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho huku wakifuatiwa na Simba pamoja na Yanga.

Malimao FC ilikiona chamoto kwenye Uwanja wa Azam Complex kwani wenyeji wao Azam ni kama walikuwa na hasira nao wakiwapasua 9-0 katika mechi ambayo walienda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao 2-0, lakini waliporejea kipindi cha pili wakalowa kwa mvua ya mabao.

Licha ya mabao tisa kuwekwa kambani, hakuna mchezaji wa Azam aliyefunga mabao matatu, lakini Abdul Suleiman ‘Sopu’ alifunga mabao mawili, huku wengine wakipachika bao moja moja - Sospeter Bajana, Shaaban Idd Chilunda, Kenneth Muguna, Kipre Junior, Yahya Zayd, Kachwele na Chiwalanga.

Ihefu nayo ikaishindilia Mtama Boys mabao 9-0 huku Sinchimba akiwa mwiba mkali kwa kutupia mabao matano, Yanga na Simba zikajipigia Kurugenzi na Eagle kila mmoja mvua ya mabao 8-0, Phiri na Mzize wakiteka shoo za michezo hiyo.

NAMUNGO WAIPATA

Kama upinzani basi Namungo waliupata kwenye raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kutoka kwa timu ngumu ya Daraja la Kwanza (Championship), Kitayosce hadi mchezo wao kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Uzoefu wa baadhi ya wachezaji wa Kitayosce ambao waliwahi kucheza Ligi Kuu Bara kwa nyakati tofauti uliwabeba kwani walionekana kumudu presha ya mchezo huo ambao ulikuwa na kasi ya namna yake huku ufundi nao ukichukua nafasi yake.

Wababe hao walienda mapumziko wakiwa sare ya bao 1-1 na hata kipindi cha pili kilishindwa kuwaamua, mchezo ukamalizika kwa sare ya mabao 2-2 na kwenye mikwaju ya panalti Namungo ilifanya vizuri (3-1) na kusonga mbele.

WABABE WA MIKOA

Licha ya kuwa wanatazamwa kama vibonde kutokana na ngazi ya ligi walizopo, Nzega United, Mapinduzi, Polisi Katavi, Buhaya na New Dundee zimeonyesha kuwa zinaweza kutoa ushindani kwenye Kombe la Shirikisho kwa kutinga raundi ya tatu.

Buhaya ya Kagera ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika iliifunga Kigoma Kwanza bao 1-0, New Dundee ya Dodoma na yenyewe ikaifunga E4M bao 1-0 huku Nzega United ya Tabora ikiitandika KFC ya Mbeya mabao 2-0.

Polisi Katavi ikiwa kwenye Uwanja wa Azimio iliing’oa Mbeya Road kwa mikwaju ya penalti (3-1) baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

RAUNDI YA TATU

Timu 32 ambazo zimetinga raundi ya tatu ambayo itaanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi Januari ni Copco FC, Gwambina FC, Mapinduzi FC za Mwanza, Mbuni FC ya Arusha, Green Warriors, Azam FC, JKT Tanzania, Simba SC, KMC, Yanga na Pan African zote za Dar es Salaam, Rhino Rangers na Nzega United za Tabora.

Polisi Katavi (Katavi), Mbeya City, Kengold, Ihefu, Tanzania Prisons na Mbeya Kwaza zote za Mbeya, Mashujaa (Kigoma), New Dundee, Dodoma Jiji zote za Dodoma, African Sports na Coastal Union ya Tanga, Geita Gold (Geita), Kagera Sugar na Buhaya FC za Kagera, Ruvu Shooting (Pwani), Namungo (Lindi), Polisi Tanzania (Kilimanjaro), Mtibwa Sugar (Moro) na Singida Big Stars ya Singida.

Columnist: Mwanaspoti