Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Azam FC ni Manchester City ya ajabu

Azam Lamba Kikosi cha Azam FC

Fri, 21 Jan 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanamama mmoja raia wa Uingereza, Amanda Staveley anatajwa kuwa mwanamke hatari zaidi katika Ulimwengu wa soka, ambapo mwaka 2008 alisimamia dili la kuiuza Manchester City kutoka kwa tajiri wa Thailand, Thaksin Shinawatra kwenda kwa bilionea mwingine wa Kiarabu, Sheikh Mansour Al Mubarak.

Baada ya dili kukamilika alikabidhiwa hundi yenye msururu wa tarakimu kisha akatokomea Marekani kula fedha alizochuma kutoka kwenye mauzo ya timu hiyo na saa chache baadaye Man City waliizunguka Chelsea na kumnunua staa wa Kibrazili, Robinho kutoka Real Madrid. Hilo lilikuwa onyo kwa klabu za England kwamba kuna balaa jipya limeingia mjini.

Tangu siku hiyo Man City waligeuka kuwa tishio England na Ulaya nzima. Unahitaji kusikia nini zaidi juu ya hatari ya Manchester City?

Tangu Sheikh Mansour aichukue Man City imetwaa mataji mengi kuliko klabu kibao England. Katika kipindi hicho wameshinda mechi nyingi kuliko klabu nyingi England. Man City wanakosa taji moja tu wanalohaha kulitafuta mpaka sasa - Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, wakati tunawasifia Man City lipo hili jambo hatupaswi kulisahau. Tangu 2008 hakuna klabu ya England iliyotumia pesa nyingi kufanya usajili kama Man City. Wakati Sheikh Mansour anainunua Man City na kuifanya kuwa tishio England, klabu yenye maskani yake kule Chamanzi inayomilikiwa na tajiri mwingine kutoka Tanzania, Azam FC ilikuwa inapanda daraja mwaka huo.

Man City ni matajiri wa England, Azam ni matajiri wa Tanzania. Tofauti yao ni ukubwa na mafanikio. Kwa sasa kule Ulaya Man City ni wakubwa kama walivyo wakubwa wengine wa miaka mingi. Huku kwetu Azam hawajafanikiwa kuusogelea ukubwa wa wakongwe wawili wa miaka mingi nchini - Simba na Yanga.

Kitu pekee ambacho Azam wamefanikiwa ni miundombinu. Azam wanajitanua kwamba wana uwanja binafsi na rasilimali zingine. Tatizo linakuja wanapohitaji kuonyesha mataji waliyotwaa. Wana taji moja la Ligi Kuu Bara na moja la Kombe la Shirikisho. Baada ya hayo? Wana vikombe vingine kadhaa vya kujitetea kama vile vya Mapinduzi. Hiki ndicho kitu kinachowaangusha.

Ukubwa wa klabu unapimwa kwa mafanikio uwanjani, kisha mambo mengine kama miundombinu yanakuja baadaye. Kama ambavyo Man City wamefanya kule England. Wana miundombinu ya kueleweka, lakini pia ni wana mafanikio ya kueleweka.

Tangu Azam wamepanda Ligi Kuu hawajafanikiwa kushindana na klabu mbili kubwa nchini kama ilivyopaswa. Mara nyingi wamejikuta nyuma ya Simba na Yanga hata katika nyakati ambazo Simba na Yanga hawapo katika ubora wao. Kwa utajiri wa Azam FC walipaswa kuwa na mataji sawa na Simba na Yanga au zaidi kwa kipindi cha miaka 13 waliopanda Ligi Kuu. Kama ilivyo kwa Manchester City kule England.

Kitu kikubwa walichokikosa Azam kwa muda wote ni kutofanikiwa kuwa na timu bora uwanjani kuwazidi Simba na Yanga. Tofauti na ule msimu mmoja ambao Azam walitwaa ubingwa hawajawahi kufanikiwa kutengeneza timu imara inayoweza kupambana na Simba na Yanga. Wamekuwa wakijitosa sokoni, lakini hawajafanikiwa kupata wachezaji wa kuwatengenezea timu bora uwanjani kushindana na wababe hawa au hata kuwazidi.

Kuna nyakati lazima utamani kuwa na Clatous Chama katika timu yako halafu Luis Miquisone awe upande wake wa kushoto na mbele yao asimame Meddie Kagere. Kuna nyakati lazima uwe na watu kama Yanick Bangala na Khalid Aucho kwenye kiungo chako kisha katikati yao uwe na miguu ya Feisal Salum.

Wakati Simba na Yanga wakitengeneza timu imara, mara nyingi Azam wamekuwa usingizini, wakaishia kuota njozi ambazo hazijawahi kutimia. Kwa miaka mingi Azam hawajawa na utaratibu mzuri wa kupata wachezaji hasa wale wanaotoka nje.

Historia inaonyesha miaka ya karibuni Simba na Yanga wamefanikiwa zaidi kwa sababu ya kunasa wachezaji wazuri kutoka nje. Hata Yanga kwa miaka minne walichechemea kwa sababu ya kufeli kunasa wachezaji wa maana kutoka nje. Hiki ndicho kilichowafanikisha Simba katika michuano ya kimataifa. Hata kinachowapa kiburi Yanga msimu huu ni usajili mzuri wa wachezaji wa kigeni waliowapata.

Kinachosikitisha zaidi kwa Azam ni wanapokubali unyonge mbele ya Simba na Yanga, licha ya utajiri walionao. Klabu tajiri haikubali kupoteza wachezaji wake bora kwa wapinzani wake wa karibu. Azam walipaswa kuwaonea Simba na Yanga sokoni.

Lakini, hali imekuwa tofuti na ilivyopaswa kuwa kwani Simba na Yanga wamekuwa wakiionea Azam. Sijui utajiri wa Azam unawafaidisha nini? Huwezi kuruhusu wachezaji wako watano bora waende kwa mpinzani wako ndani ya msimu mmoja. Manchester City haiwezi kufanya hiki kitu kwa Manchester United au Liverpool.

Columnist: Mwanaspoti