Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Azam FC kwa Simba hatimaye imewezekana

Azam Vs 'nyama.jpeg Azam ilishinda kwa Simba baada ya miaka 5

Mon, 31 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Januari 28, 2017 ndiyo ilikuwa mara ya mwisho Azam FC kuifunga Simba kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara. Bao la dakika ya 70 la John Bocco lilikuwa tofauti kwenye mchezo huo. Baada ya msimu huo, Bocco akahamia Simba na kuondoka na ushindi wake dhidi ya Simba.

Bocco ambaye hilo lilikuwa bao lake la 13 dhidi ya Simba kwenye mashindano yote aliondoka Azam FC na kuhamia Simba akiwa na wenzake watatu kina Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe.

Wachezaji hawa ni kama walipeleka siri za ushindi wa Azam kwa Simba kwani kuanzia hapo Azam iliishia kuusikia redioni tu ushindi mbele ya Simba.

Azam imepiga michezo 10, Simba wakishinda mara nne na mara sita wakitoka sare. Katika mechi hizo Simba wamefunga mabao 14 huku Azam FC wakifunga mabao nane.

KWANINI HAIWEZEKANI

Miaka mitano bila ushindi ni mingi sana kwa mechi za upinzani wa dabi ya Mzizima na kuna mambo mengi yaliyoifanya Azam FC ikwame mbele ya Simba miaka yote hiyo.

UDHAIFU WA KIKOSI

Kuondoka kwa wachezaji sita kwa pamoja, watano wakienda Simba na mmoja yaani Gadiel Michael kwenda Yanga lilikuwa pigo kubwa sana.

Azam ilishindwa kuziba nafasi zao kwa mbadala sahihi na kujikuta ikikosa timu yenye muunganiko sahihi uwanjani.

Razack Abalora alikuwa mbadala sahihi wa Manula lakini alishindwa kudumu kwenye ubora wake. Hakukuwa na mbadala wa Bocco hadi ujio wa Prince Dube mwaka 2020. Hakukuwa na mbadala wa Kapombe japo Nicholas Wadada alikaribia lakini hakuwa na mwendelezo wa kiwango bora.

Wakati Azam FC wakihangaika na kikosi Simba waliendelea kuimarika kwa kusajili wachezaji bora kwelikweli walioisaidia nyumbani hadi kwenye mashindano ya Afrika. Meddie Kagere, Clatous Chama na Luis Miquisone waliifanya Simba iwe imara sana katika mashindano.

WAAMUZI

Licha ya ubora wa Simba, lakini kuna baadhi ya mechi walikuwa na siku mbaya na kupoteza mechi, lakini ikitokea hivyo siku ya mchezo wa Azam, waamuzi nao wakawa na siku mbaya. Kwa mfano, mechi ya kwanza Simba kuifunga Azam ilikuwa Februari 7, 2018 kwa bao la Emmanuel Okwi ambalo mtangazaji wa Azam TV, Hasheem Ibwe alilisherehesha kwa mbwembwe za ‘waya waya, waya waya.’

Mwamuzi alikuwa Jonesia Rukya ambaye aliikataa penalti ya Azam FC katika dakika 90 baada ya Yusuf Mlipili kumuangusha Enock Atta Agyei ndani ya eneo la hatari.

Endapo Jonesia angekuwa makini yawezekana Azam FC wangepata penalti na endapo wangefunga basi mchezo ungekuwa sare.

Machi 4, 2020 Azam FC walipoteza 3-2 kwa Simba.

Mwamuzi wa mchezo huu, Emmanuel Mwandembwa aliikataa penalti ya wazi ya Azam FC baada ya Pascal Wawa kumuangusha Idd Kipagwile ndani ya eneo la hatari.

Pia mwamuzi msaidizi namba mbili Helen Mduma aliipa Simba faida ya kushambulia licha ya mpira kutoka. Kapombe akapiga krosi na Kagere akafunga bao la tatu kwa Simba.

Mechi mbili za Chamazi ambazo ziliisha kwa sare Azam FC walistahili penati.

Ya kwanza ilikuwa ya Julai 15, 2021 ambapo Gadiel alimuangusha Ayoub Lyanga katika dakika ya 90 ilhali matokeo yakiwa bao 1-1.

Endapo mwamuzi Elly Sasii angetoa penalti kwa Azam FC na ikafunga, basi ingeshinda mchezo huo. Na pili ni mchezo wa msimu uliopita ambapo Elly Sasii tena alikataa kutoa uamuzi sahihi baada ya Kibu Dennis kuudaka mpira uliopigwa na Kenneth Muguna akiwa ndani ya eneo la hatari.

MIGOGORO YA NDANI

Kwa miaka mingi Azam FC imekuwa timu yenye minyukano mingi ya ndani kwa ndani tofauti na watu wanavyodhani.

Bodi ya wakurugenzi ambayo inaundwa na wana familia wa Bakhresa ina watu wanne ambao hawajawahi kukubaliana kitu wote kwa pamoja. Anaweza akapatikana mchezaji mzuri, lakini mmoja wa wakurugenzi akamkataa, basi hasajiliwi tena timu hiyo. Kwa mfano Fiston Mayele ni mchezaji ambaye aliitaka sana Azam FC aichezee kabla ya kutua Yanga.

Alipokuja nchini na AS Vita ya DR Congo kucheza na Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika basi walilotumia ni la Azam FC.

Akamwambia dereva wa basi hilo nia yake ya kutaka kuitumikia klabu hiyo ya Chamazi. Taarifa zikafika Chamazi na akatafutwa Mayele, akakubali. Lakini mmoja wa wakurugenzi hakumtaka licha ya wengine kumkubali. Mayele akaangukia Yanga na sasa anatetema huko.

Hawa wakurugenzi huwa na ukaribu na baadhi ya wachezaji. Hilo peke yake ni tatizo kwani huwapa viburi wachezaji wakiamini wako salama. Pia kocha yeyote akitofautiana na mmoja wa wachezaji wa aina hiyo atakiona cha moto katika utekelezaji wa majukumu yake klabuni hapo.

Ndiyo maana katika miaka 14 ya kwenye Ligi Kuu wametumia makocha zaidi ya 15.

SASA IMEWEZEKANA

Msimu huu kidogo mambo yanaimarika kikosini. Yusuf Bakhresa kaamua kuvaa mabomu na kujitosa mbele kuisaidia timu. Amesimamia usajili na sasa anasimamia matokeo.

Vipigo viwili kwenye Ligi kuu Bara na kutolewa kimataifa imekuwa kengele ya tahadhari kwake. Kuelekea mchezo dhidi ya Simba alirudi ghafla kutoka safarini ughaibuni kuja kuzungumza na wachezaji.

Alishuka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere moja kwa moja hadi Kigamboni kwenye jumba lake la kifahari la mapumziko ambako aliwaalika wachezaji.

Wakakaa, wakabadilishana mawazo na kuwaeleza matarajio yake kwao. Alifika mbali na kuwataka wamtetee kwani timu inapofanya vibaya hupokea matusi kwenye Instagram DM kutoka kwa mashabiki.

Akasema mchezo wa Simba unakuja, lakini yeye hana wasiwasi nao kwa sababu anajua uwezo wa wachezaji kwenye mechi za aina hiyo. Kilio chake kikubwa kilikuwa kucheza kwa kiwango kwenye mechi zote.

“Timu ilicheza vizuri sana dhidi ya Al Akhdar (ya Libya kwenye Kombe la Shirikisho Afrika), lakini inacheza vibaya dhidi ya KMC. Hiyo siyo sifa ya timu inayowania ubingwa,” alimaliza Yusuf.

Wachezaji wakamuahidi kuanza ligi dhidi ya Simba na mechi zinazofuata ambapo leo Oktoba 31 wameitandika Ihefu bao 1-0.

Columnist: Mwanaspoti