Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Athari za kitabaka, jinsia, elimu kusimama wakati wa corona

Wanafunzi.webp Athari za kitabaka, jinsia, elimu kusimama wakati wa corona

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KUNA hatari ya kupoteza mwaka mmoja katika mtiririko wa elimu kutokana na kuendelea kushamiri kwa homa ya corona, hivyo kulazimisha shule na vyuo kuendelea kufungwa.

Wakati shule zilipofungwa kwa mwezi mmoja kuwezesha serikali kuchukua hatua kadhaa kupambana na kuenea kwa janga hilo, hasa kutokana na kilichotokea nchi za mbali kimsingi wanafunzi walikuwa kama wamepata likizo ya ziada.

Ila kwa muda wote wa ziada ambako likizo hiyo inaendelea, na kulingana na kinachotokea katika familia za watu, zipo athari tarajiwa.

Maisha ya kuwa mwanafunzi kama zilivyo shughuli nyingine kijamii au kifamilia yana maeneo mawili, moja ni matazamio, ambayo hasa ndiyo yanatoa changamoto na hamasa ya kuendelea na maisha hayo, licha ya kuwa na sulubu za hapa na pale.

Upande mwingine ni kuvumilia, kuwa bado wakati mfupi tatizo hilo linakwisha na mtu anaanza maisha mapya, awe ni mzazi ambaye mwanae yuko shuleni, au kijana asiye na furaha eneo anapokaa na kusoma, anavumilia tu hali hiyo iishe ili asilete ugomvi endapo ataacha shule mapema. Livu ikiwa ndefu mno, ‘anabanjuka.’

Wakati kimsingi kipindi hiki cha vizuizi vya aina tofauti kutokana na corona ni mazingira ambayo kila mtu anatakiwa kuangalia yuko wapi na inabidi akutane na nani, kupungua kwa shughuli za kawaida pia kunaleta uhaba wa riziki katika maeneo mapana tu kijamii.

Shughuli za elimu kwa mfano zinaposimama, kuna mlolongo wa wahusika na shughuli hizo siku hadi siku ambao matazamio yao yanaathirika, kwa mfano washona nguo za shule, wasafirishaji wao, iwe ni kwa mabasi maalum au ya kawaida. Nauli zao siyo kubwa lakini zinajazia kwa kiasi si haba.

Kwa mazingira hayo, kupungua kwa vipato kutokana na vizuizi na kukwama kiasi fulani kwa shughuli tofauti kunaleta athari za utegemezi kuongezeka au kuwa hali ya kawaida kwa wale ambao walikuwa wanajimudu.

Ina maana kuwa katika familia ambayo mlezi – awe baba, mama au mhusika mwingine ambaye familia hiyo inamtegea anapokuwa katika mkwamo, athari tanzu zinaanza, kila mtu anatafuta mlango wa kutokea, au njia ya kujikimu.

Ni kuingiza uwezo wa kufanya kazi katika soko ambalo tayari limedoda kwa kutokuwapo shughuli za kutosha, hivyo bidhaa ya uwezo wa kufanya kazi inakosa mnunuzi, inabaki tu hitaji la kawaida, lipangiwe pesa.

Kutokana na ulazima wa jamii kuendelea kuhakikisha huduma za aina kadhaa zinapatikana, vinginevyo hata uhai wenyewe unakuwa mashakani, mikwamo hii ya kifamilia itaathiri zaidi wanafunzi, na hasa watoto wa kike.

Pale walipokuwa wamesimama kidete kufuatia masomo yao hadi yakamilike na kutazamia labda kuendelea zaidi siku za usoni, ngoja isiyo na mwisho inabadili hali hiyo.

Walio katika familia zinazojiweza ambako hakuna manyanyaso mapya kutokana na mikwamo ya corona, ambako mtoto wa kike atajihisi anathaminiwa kama ilivyo kawaida, hapawezi kuwa na athari za wazi. Ni pale mtoto akionekana mzigo kwa sababu mzazi au mlezi amekwama ndiyo hapo athari zinaweza kutokea, kwani ni msambaratiko wa kifamilia.

Taarifa zinazotoka nchi kadhaa ambako uzururaji wa watu nyumbani umesimamiwa kwa nguvu na vyombo vya dola kupunguza kasi ya maambukizo ya corona zinaonyesha kuwa udhaifu wa kifamilia na hata kuvunjika kwa amani kunaongezwa na hali ya kutotoka nyumbani.

Imefikia mahali ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliona azungumzie suala hilo mwenyewe, hali ya zuio la watu kubaki nyumbani. Imeongeza kwa kasi kubwa mifarakano.

Ni rahisi kuelewa hali hiyo kwani watu wengi wanaishi kwa kutegeana, kuondoka asubuhi na kurudi jioni au usiku kila mtu amechoka wanalala, hakuna wakati wa mazungumzo mengi na kukumbushana machungu.

Ni katika hali hiyo ambako mwanafunzi aliyekuwa akingoja mwaka uishe aanze maisha mengine, iwe ni kwa kufaulu au kupata cheti atafute kazi, au angalau awe huru kujiamulia hali yake ya baadaye bila kubanwa na sheria, atakapoanza kuchoshwa na ngoja ya corona. Halafu haina mpaka kuwa mwezi huu au ujao au hadi Oktoba itakuwa imekwisha.

Kwa maana hiyo kuna hitilafu ya uvumilivu inayowezekana kutokea, kuwa mwanafunzi akiona shule hazifunguliwi na nyumbani hapakaliki, siyo rahisi kuendelea kuvumilia.

Ni suala la utafiti ni njia gani zinaweza kutumika kumtenganisha na nyumbani endapo anaweza akafanya vingine, ingawa hali hiyo bado haijawakuta wengi, kwani bado ni mapema tangu shule zimefunguliwa.

Kimsingi ni kuwa siyo kila mwanafunzi atarudi shuleni zikifunguliwa, na kama itapita miezi kadhaa au hata kukaribia mwaka, wengi tu watakuwa wamebadili mazingira, siyo lazima kuwa yatakuwa bora zaidi bali wanaweza kuwa huru zaidi, kwani la msingi katika maisha ni riziki tu.

Ushauri unaotolewa na wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu namna ya kukaa katika mazingira ya kizuizi, kuhakikisha afya kiakili na kimwili ni wazi unawafaa zaidi walio na mazingira mazuri ambayo hayategemei shughuli za kila siku kupata riziki.

Wale ambao kukaa ndani kunavuruga vipato ni kazi ngumu kubakiza akili mahali pamoja na kuelekeza mawazo katika vitu kama televisheni, vitabu au hata maombi kwani kwa Afrika suala hilo ni muhimu, ingawa ng’ambo si rahisi likatajwa au kuona limezoeleka.

Ugumu wa maisha unapunguza utashi wa kukaa pamoja, na uanafunzi bila shule unageuka u-house girl au kuwa mzigo kwa ndugu, hivyo haitakuwa vigumu kuvumilia. Ni kukatisha masomo endapo shule hazifunguliwi mapema.

Columnist: www.tanzaniaweb.live