Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Athari za fataki, mabomu viwanjani

Mashabiki Pc Athari za fataki, mabomu viwanjani

Fri, 28 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Mkapa kati ya Simba na Whydad Athletic Club ya Morocco lilitokea tukio la uwashaji na ulipuaji fataki. Tukio hilo na mengine ya mashabiki wenye fujo wa klabu hiyo wanaojulikana kama Ultras ndio yalisababisha mchezo huo ambao Simba walishinda bao 1-0 kusimama kwa dakika 10 kabla ya mapumziko.

Mashabiki hao waliwasha fataki zilizomwaga moshi mwekundu angavu na mweupe kiasi cha kuwapa hofu mashabiki kutokana na anga la uwanjani kujaa moshi kiasi cha kuzuia kuona vyema uwanjani. Matukio ya uwashaji baruti na mabomu-moshi siyo utamaduni wa mashabiki wa soka wa Bongo, bali ni wa mashabiki wa ligi za nje kama vile zenye asili ya Kiarabu.

Katika soka utamaduni huo unaruhusiwa, lakini kwa tahadhari kubwa kwani yapo matukio ya watu kupata athari za muda mfupi ikiwamo kuungua na kuvuta moshi mara baada ya kuwasha fataki. Tukio lilipotokea katika mechi hiyo ya hapa nchini huko nyumbani kwao ndio itakuwa kubwa zaidi kwa kuwa watakuwa na mashabiki wengi.

Nia na lengo kubwa la utamaduni wa kuwasha fataki na mabomu moshi ni kuleta hamasa kwa timu yao, lakini pia ni mbinu za kuharibu saikolojia wachezaji na mashabiki wa timu pinzani.

Utamaduni huu sio wa kila sehemu, kuna baadhi ya nchi zilipiga marufuku fataki na mabomu moshi kutokana na kuhusishwa na ajali na majeraha kwa mashabiki viwanjani. Tayari Simba imewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutoa tahadhari dhidi ya mashabiki wa Wydad maarufu kama Ultras.

Leo jicho la kitabibu litalitamaza tukio la kuwasha fataki na mabomu moshi viwanjani ili kukupa ufahamu kama kuna madhara yanayotokana na muwako wa fataki na moshi wake pamoja na mabomu moshi.

ATHARI ZAKE

Moshi unaotoka mara baada ya fataki au mabomu moshi kuwashwa siyo tu upo kwa ajili ya kusambaa katika anga la uwanja, bali huleta athari za kiafya. Athari ambazo zinaweza kumpata mtu ni pamoja na zile za muda mfupi katika mfumo wa hewa ikiwamo kuvuta moshi wa fataki au bomu moshi kuweza kuchokoza pumu, shambulizi katika mirija ya hewa na hatari ya kupata uambukizi wa njia ya hewa.

Mtu ambaye tayari ana magonjwa ya moyo kuvuta moshi wa fataki au vijimlipuko kunahusishwa na kupata shambulizi la moyo na hitilafu ya mapigo ya moyo. Katika uvutaji wa moshi kwenye mazingira ya viwanjani mtu anaweza kupata hali ya kuchoka na kuishiwa nguvu ingawa kidogokidogo hali huweza kuboreka na hatimaye kuondoka kabisa.

Dalili na viashiria vinavyojitokeza baada ya kuvuta moshi huo ni pamoja na kukohoa au kupaliwa, kupata mkereketo wa koo na puani, kupiga chafya na kuchuruzika mafua mepesi. Dalili hizi zinajitokeza zaidi kwa wale watu ambao wana tatizo la mzio sugu yaani allergy. Vilevile wanaweza kupata hali ya mwili kuwasha na kuvimba hasa maeneo ya usoni na macho kuwa mekundu.

Kwa mtu ambaye ana tatizo la pumu anaweza kupata shambulizi la ghafla la pumu. Ikumbukwe kuwa pumu ni tatizo linalohitaji huduma za dharura na hatua zisipochukuliwa mtu anaweza kupoteza maisha. Moshi huo unaweza kumletea mtu tatizo la muda kutoona vizuri na pia hali ya kuwasha machoni.

Ukiacha madhara ya muda mfupi ya kuvuta hewa yenye moshi wa fataki na mabomu moshi, pia kuna matukio ya mashabiki na wachezaji kuwahi kujeruhiwa na vifaa vya kuwashia vitu hivyo.

Mfano fataki zinazowashwa huweza kuungua na kutoa joto kali linaloweza kumchoma mtu ambaye atagusana au kushika eneo lililopata moto. Pia yamewahi kuripotiwa matukio ya wachezaji au mashabiki katika viwanja vya soka kurushiwa na kupigwa na fataki hizo na mabomu moshi hatimaye kujeruhuia.

KEMIKALI ZILIZOMO NDANI

Kulipua na kuchomeka kwa fataki na mabomu moshi huweza kutoa kiwango kikubwa cha vichafuzi hewa ikiwamo hewa ya Sulphurdioxide (S02), Carbondioxide (CO2) na Carbonmonoxide. Vilevile ndani ya moshi huo huwa na vitu vingine vilivyobeba metaliki chumvi kama vile aluminium, manganese na cadmium. Baadhi ya tafiti zilizofanyika katika idara za huduma za dharura Ulaya zimewahi kubaini uwepo wa madini kama lead, copper na viambata sumu katika moshi huo jambo ambalo ni hatari kiafya.

Baruti hizo huwa na poda maalumu ambayo ikiwashwa hulipuka na kutoa chembechembe za metaliki ambavyo huwamo ndani ya moshi vinavyotosheleza kuelea angani na kuvutwa ndani ya mapafu. Utafiti mwingine uliofanywa katika matamasha yenye utamaduni wa kuwasha na kulipua fataki umeonyesha kiwango cha madini ya lead, copper, strontium, potassium and magnesium kuongezeka kwa watu walioshiriki.

Pamoja na kwamba bado tafiti zilizofanywa hazijitoshelezi kueleza athari za moja kwa moja katika mapafu za ulipuaji fataki viwanjani, lakini wanasayansi wanahusisha na madhara ya muda mrefu ya kuvuta moshi wa fataki hizo ikiwamo vifo vya saratani ya mapafu.

HATUA ZIPI ZICHUKULIWE?

Kampuni zinazotengeneza baruti na mabomu moshi maalumu kwa ushangiliaji katika viwanja vya michezo zimekuwa zikizingatia sheria za mazingira na afya ili kuhakikisha usalama wa bidhaa zao ndio maana hazijapigwa marufuku. Ili kujikinga na madhara ya moshi ni kuhakikisha kuwa unakwepa kuvuta moshi huo ikiwamo kukaa mbali na mashabiki wenye utamaduni wa kuwasha fataki na mabomu moshi.

Kwa yule ambaye amepata ajali ya kuvuta hewa ya moshi wa fataki na mabomu anatakiwa kutolewa eneo husika na kuwekwa katika sehemu yenye hewa safi au kupewa hewa safi na watoa huduma ya kwanza, na anapopata nafuu ni vizuri akapumzika na kulala muda mrefu kwa kuweka kichwa katika mto ili kuleta upumuaji mzuri na kufifisha kikohozi.

Inashauriwa watu wote wenye pumu au mzio na magonjwa ya moyo kuepuka kwenda katika viwanja ambavyo vinaruhusu ushangiliaji wa kuwasha fataki na mabomu moshi.

Ligi Kuu ya England na Chama cha Soka England (FA) walisaidia kutolewa kwa elimu juu ya hatari za shughuli za ulipuaji fataki na mabomu moshi viwanjani kutokana na tahadhari zilizotolewa na tafiti mbalimbali.

USHAURI

Utamaduni huu usiwape hofu mashabiki wanaokwenda kushangilia na kuzipa hamasa timu zao. Ikumbukwe kuwa madhara ya fataki na mabomu moshi siyoo makubwa kiasi hicho ndiyo maana hazijazuiwa.

Columnist: Mwanaspoti