Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Arsenal usajili ilioufanya baada ya kuwakosa mastaa wa maana

Trossard.jpeg Tossard

Sun, 29 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Arsenal wameonyesha kuwa na macho ya kuona wachezaji wenye vipaji vya juu, lakini ubahili wao wakati mwingine umekuwa ukiwakosesha fursa muhimu za kupata huduma ya wanasoka hao makini kabisa ndani ya uwanja.

Kuna baadhi ya mastaa wamekuwa wakitamba huko kwingineko ni kwa sababu tu Arsenal haikuwa tayari kutoa kiasi cha pesa kilichohitajika ili kunasa saini zao.

Kuna kundi kubwa la mastaa wa maana usiopungua 10, ambao Arsenal iliwataka, lakini wakashindwa kulipa kiasi cha pesa kilichotakiwa, wakakosa na kuishia kwenda kusajili wabadala wake. Cheki hapa orodha ya mastaa wa maana 10 ambao Arsenal ilitaka kuwasajili wakashindwa na kunasa wabadala wao katika kipindi cha miaka 13 iliyopita. Wangekuja Arsenal ingekuwaje? Wale waliokuja badala yao wamefanyaje?

2023 – Wamemkosa Mudryk, wakamsajili Trossard

Anafahamika kama Neymar wa Ukraine, Mykhailo Mudryk – staa ambaye alikuwa kwenye rada za Arsenal na kila kitu kilionekana kama staa huyo wa zamani wa Shakhtar Donetsk atua Emirates kwenye dirisha hili la Januari. Ofa zao tatu zilikataliwa, kabla ya Chelsea kuingia kati na kutoa pesa ambayo klabu yake ilikuwa inataka na kufanikiwa kumnasa Mudryk. Arsenal baada ya kufeli kwa Mudryk, waliamua kuvamia Brighton na kwenda kumsajili Leandro Trossard kwa mkwanja wa Pauni 27 milioni. Mudryk ana miaka 22, Trossard miaka 28.

2021 – Wamemkosa Buendia, wakamsajili Odegaard

Baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye Championship kwa kile alichofanya na Norwich City, Emiliano Buendia akawa staa mkubwa aliyesakwa na kila timu na Mikel Arteta alihitaji akacheze Arsenal.

Wakapeleka Pauni 30 milioni ikataliwa na Norwich. Aston Villa kuona hivyo, wakafanya fasta wakapeleka Pauni 38 milioni wakamchukua. Arsenal baada ya kumkosa Buendia, wakaamua kumchukua jumla Martin Odegaard baada ya mkopo wake kumalizika. Kwa Odegaard waliwalipa Real Madrid zaidi ya Pauni 38 milioni.

2017 – Wamemkosa Lemar, wakamsajili Mkhitaryan

Wakati Arsenal iliposhindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2017-18 michuano inayopewa kipaumbele kikubwa na wachezaji kuliwaponza na kukosa saini ya Thomas Lemar, mchezaji ambaye alikuwa moto kwa wakati huo akiwa AS Monaco iliyofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Liverpool nao walikuwa wanamtaka, lakini Atletico Madrid wakamnasa 2018. Badala yake, Arsenal wakaamua kumchukua Henrik Mkhitaryan kutoka Manchester United kwa dili lenye thamani ya Pauni 30 milioni kwa kubadilishana na Alexis Sanchez.

2016 – Wamemkosa Dembele, wakamsajili Lucas Perez

Arsenal kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi 2016 ilifanya mchakato wa kunasa saini za mastaa wa Leicester City, Jamie Vardy na Riyad Mahrez, lakini kuna straika mwingine kabisa aliyekaribia kutua Emirates, Moussa Dembele. Arsenal ilishindwa kukamilisha dili, staa huyo Mfaransa akatimkia zake Celtic ya Scotland kabla ya kumuuza Lyon kwa Pauni 20 milioni. Arsenal wao walipomkosa Dembele kitu ambacho walifanya walimsajili straika Lucas Perez, ambaye hata alipoondoka hakuna faida yoyote aliyoacha huko Emirates.

2015 – Wamemkosa Khedira, wakamsajili Elneny

Msimu wa 2015-16 ulikuwa wa mwisho Arsenal kuonyesha kuwa na uwezo wa kumchukua ubingwa, ambapo walikuwa kileleni wakati wanaingia mwaka mwingine, lakini wakapokea vichapo vichapo kutoka kwa Leicester City, ambao wakanyakua taji hilo la Ligi Kuu England kwa msimu huo. Pengine mambo yao yangekuwa tofauti kama wangekuwa na huduma ya kiungo Sami Khedira, ambaye walikaribia kabisa kumsajili kabla ya Mjerumani huyo kunaswa na Juventus. Walipomkosa Khedira, Arsenal waliamua kwenda kumsajili Mohamed Elneny kutoka Basel.

2014 – Wamemkosa Di Maria, wakamsajili Welbeck

Baada ya kupata mafanikio makubwa na Mesut Ozil, Arsene Wenger alivamia tena Real Madrid akihitaji wachezaji ambao hawakuwa wakihitaji klabuni hapo. Winga Angel Di Maria alikuwa anajiandaa kuachana na maisha ya Bernabeu mwaka 2014 baada ya Real Madrid kumsajili James Rodriguez. Lakini, shida ikawa moja, Arsenal hawakuwa tayari kulipa Pauni 75 milioni kumchukua Di Maria, ambapo wenzao Manchester United walilipa na kumchukua Muargentina huyo. Arsenal wao walienda kumchukua Danny Welbeck kutoka Man United.

2013 – Wamemkosa Suarez, wakamsajili Giroud

Wakati Arsenal ilipohitaji saini ya Luis Suarez kutoka Liverpool, waliambiwa wanahitajika kulipa zaidi ya Pauni 40 milioni iliyobainishwa kwenye mkataba wake. Kusikia hivyo, miamba hiyo ya Emirates ikaamua kupeleka Anfield ofay a Pauni 40,000,001 iliyotafsiriwa na Liverpool kama dharau kwamba kwenye Pauni 40 milioni, wao wameongeza Pauni Moja tu. Mwaka uliofuatia Luis akauzwa Barcelona kwa Pauni 75 milioni, wakati Arsenal wao walipomkosa straika huyo walikwenda kumsajili Olivier Giroud kutoka Montpellier ya Ufaransa.

2012 – Wamemkosa Hazard, wakamsajili Podolski

Arsenal kitendo cha kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimu wa 2011-12 kulitosha kumzuia Eden Hazard asienda Tottenham, lakini hiyo haikuwa ushawishi wa kumvuta Emirates. Hazard baadaye akanaswa na Chelsea, huku akisema Arsenal kuna kocha wa wachezaji wa Kifaransa pamoja na Thomas Vermaelen.

Msimu huo ulikuwa wa pigo pia Arsenal, ambapo Robin van Persie aliondoka na kwenda kujiunga na Manchester United. Arsenal wao badala yake walienda kumsajili Lukas Podolski, ambaye kiukweli si Eden Hazard.

2011 – Wamemkosa Sarabia, wakamsajili Joel Campbell

Wakati Arsenal wanamtaka Pablo Sarabia kwa mara ya kwanza hakuwa amejitengenezea nafasi Real Madrid kwa wakati huo, lakini kiungo huyo mshambuliaji alikuwa kwenye ubora mkubwa uliowafanya Getafe wamsajili fasta. Badaye alijiunga na Sevilla na kucheza dakika 90 wakati wanawachapa Man United uwanjani Old Trafford kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sasa yupo kwa mkopo Wolves akiwa amepita pia PSG. Arsenal walipomkosa Sarabia, walienda kunasa saini ya Joel Campbell – supastaa wa Costa Rica.

2009 – Wamemkosa Felipe Melo, wakampanisha Denilson

Arsene Wenger baada ya kutazama mechi ya kimataifa baina ya Brazil na Italia uwanjani Emirates akavutiwa na huduma ya kiungo mkabaji Felipe Melo na akaona ni wakati mzuri kwa staa huyo wa Fiorentina kwa wakati huo atue Arsenal. Wenger alihitaji kiungo ili kuziba pengo la Aaron Ramsey, aliyekuwa amevunjika mguu. Lakini, walipomshindwa kumnasa Melo, wakahamia nguvu kwa makinda, ambapo waliwapandisha kwenye kikosi Denilson na Alex Song. Hata hivyo, haukuwa uamuzi mbaya kuliko kufanya usajili wa kupaniki.

2003 – Wamemkosa Yaya Toure, wakamsajili Fabregas

Arsenal ilihusishwa na Yaya Toure na sio mara moja bali mbili na ilikaribia kabisa kumsajili baada ya kuchezea timu hiyo mechi ya kirafiki mwaka 2003. Uhamisho ukakwama kwenye vibali vya kazi, hapo Yaya akiwa bado kijana alitimkia zake Ukraine, kabla ya kwenda kujiunga na yake Kolo Toure huko Manchester City. Katika dirisha hilo la majira ya kiangazi, Arsenal baada ya kumkosa Yaya Toure waliamua kwenda kumsajili Cesc Fabregas na hakika haukuwa usajili mbaya kwani Mhispaniola huyo baadaye alikuja kuwa nahodha huko Emirates.

Columnist: Mwanaspoti