Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Arsenal, Arteta walikimbia kabla ya kuanza kutembea

Arteta Ms Kocha wa Arsenal Mikel Arteta

Mon, 29 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unatoka tumboni kwa mama. Unabebwa. Baada ya miezi kadhaa unaanza kutambaa. Unasimama dede halafu unaanza kutembea. Baadaye kabisa unatembea kutoka katika kona moja ya sebule kwenda katika kona nyingine.

Lugha rahisi ya kuielezea timu yangu ya Arsenal ni kwamba kuna hatua waliruka. Mikel Arteta, mzaliwa wa San Sebastian pale Hispania alifika katika milango ya London Colney yalipo makazi ya Arsenal akiikuta Arsenal ikiwa hoi.

Akajaribu kuisimamisha dede, ghafla ikaanza kukimbia kutoka kona moja ya sebule kwenda kona nyingine. Haikutembea. Ulikuwa ni mshangao wa wengi kuiona Arsenal ikiwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu.

Msimu wa 2021/2022 Arsenal walikuwa wameachwa pointi nane na timu iliyokuwa imeshika nafasi ya nne, Tottenham Hotspurs. Wao walikuwa wameshika nafasi ya tano. Lakini walikuwa wameachwa pointi 38 na mabingwa Manchester City.

Ghafla timu hii iliingia msimu huu na kuanza kuwania ubingwa. Kutoka kutoingia Top Four hadi kuongoza Ligi kwa miezi mingi. Ghafla namna hii? Ndio. Iliwezekana kwao. Kutoka kutokuwa katika Ligi ya Mabingwa kwa miaka sita, halafu ghafla ikajikuta katika mbio za ubingwa hadi April. Ndio kwao iliwezekana.

Lengo la timu ambayo imepotea katika Ligi ya Mabingwa kwa muda mrefu ni kurudi katika Ligi ya Mabingwa kwanza kabla ya kufikiria kugombea ubingwa. Lakini ghafla Arsenal wakajikuta katika mbio za ubingwa.

Kisa? Manchester City walianza kwa kusuasua lakini hapo hapo Manchester United, Chelsea, Liverpool na Tottenham wote wakajikuta ovyo ovyo. Arsenal angefanya nini? Kuwasubiri?

Hapana! Akajiongeza na kuongoza Ligi. Iliwahi kutokea kwa Leicester City wakati walipochukua ubingwa mwaka 2016. Wakubwa walikuwa wapi? Walizubaa.

Kuanzia hapo Arsenal akajikuta akikimbia badala ya kutembea. Uzuri wa msimu huu ni kwamba City alihakikisha hawi mbali sana na Arsenal. Alikuwa kama vile fisi ambaye anaunyemelea mkono wa mwanadamu. Pengo kubwa zaidi alilowahi kuachwa ni pointi nane.

Kuna kitu ambacho Manchester City walikuwa wanakisubiri na wakafanikiwa kukipata baadaye. City alikuwa anasubiri uchovu kwa wachezaji wa Arsenal kabla ya msimu kumalizika. Hiki ndicho ambacho kwa kiasi kikubwa kimeamua mbio za ubingwa msimu huu.

Arsenal walitumia nguvu kubwa mwanzoni mwa msimu hadi katika raundi ya pili wakiwa na kundi dogo la wachezaji. Manchester City walikuwa na kundi kubwa la wachezaji ambao ubora wao hautofautiani sana. Katika nafasi ya kulia angeweza kupangwa yeyote kati ya Riyad Mahrez na Bernardo Silva na usione tofauti.

Katika upande wa kulia wa Arsenal lazima acheze Bukayo Saka. Katika misimu miwili ameshindwa kuanza mechi moja tu. Hii ni moja kati ya tofauti kubwa ya Manchester City na Arsenal.

Pale City kama Kelvin De Bruyne hachezi basi atacheza Ilkay Gundogan. Dakika ya 68 ya mchezo anatoka Phil Foden anaingia Jack Grealish. Hawa ndio Manchester City. Tabu ipo pale pale. Anatoka Erling Haaland baada ya kutupia hat trick anaingia Julian Alvarez. Tabu ipo pale pale.

Arsenal hawajawahi kuwa na timu hii. Najua kwamba Arteta anajua anachofanya kwa sababu timu kama hii amewahi kuona Manchester City. Wiki iliyopita niliandika hapa kwamba mambo mengi Arteta anaiga kutoka kwa Pep Guardiola. Lakini suala la ubora wa kikosi sio suala la kuiga. Ni suala la matajiri wa Arsenal kutia pesa katika dirisha kubwa hili ambalo litafunguliwa baada ya Ligi kuu ya England kubwa rasmi wikiendi hii. Ni hiki tu ndicho ambacho Arteta anahitaji kwa sasa.

Mbinu za ufundishaji anazo. Tayari ameshaonyesha kile ambacho anaweza kufanya. kilichobaki kwa sasa ni matajiri wa Arsenal kumpa kikosi chenye wachezaji wengi ambao wana ubora ambao unalingana. Alipoumia William Saliba halafu nafasi yake ikachukuliwa na Rob Holding nikajua Arsenal ipo matatizoni.

Lakini ni kwamba pumzi ilikuja kukata mwishoni. Walijaribu kujiondoa katika michuano mbalimbali na kuelekeza akili yao katika Ligi kuu lakini bado pumzi ilikata. Dalili za kukata kwa pumzi zilianzia pale ambapo Arsenal waliongoza mabao mawili Anfield dhidi ya Liverpool yakarudi yote.

Wakaenda kucheza na West Ham wakaongoza kwa mabao mawili yakarudi yote. Hizi mechi zote mbili kama zingekuwa katika raundi ya kwanza mabao yasingerudi. Walikuwa na nguvu za kutosha katika miili yao. Wakarudi nyumbani kucheza na Southampton wakaongozwa 1-3. Baadaye wakapambana na kurudisha mabao yote. Kuanzia hapo walikuwa hoi. Wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Arsenal wamecheza mechi nyingi za ligi kuu kuliko wachezaji wa Manchester City.

City wana kikosi kipana chenye ubora na pia wana kocha bora. Wao ni kombinesheni ya vitu viwili. Hata Guardiola bila ya kikosi kipana asingeweza kuinyanyasa Ligi Kuu ya England kiasi hiki. Na sasa amekwenda mbali zaidi kwa kukaribia kuchukua mataji matatu. Anastahili.

Msimu ujo Arsenal wana msimu wa kuamua ukomavu wao katika Ligi Kuu ya England. Hapa walipofika wanahitaji kuwekeza wachezaji watano muhimu ambao wanakwenda kubadilishana nafasi katika kikosi cha kwanza na wale wachezaji wanaoanza.

Ifike mahala timu iwe na ubora ule ule hata kama Saka na Odegaard wapo benchi. Hiki ndicho kitu ambacho kimepeleka Manchester City iwe bora kuliko klabu nyingi za Ligi Kuu England. Rafiki zangu Manchester United asipocheza Marcus Rashford basi maisha yanakuwa magumu. Hauwezi kukuta kitu kama hiki pale Etihad.

Vyovyote ilivyo Arteta amefanya kazi nzuri Arsenal. Tatizo kubwa la mashabiki wa Arsenal waliovunjika moyo ni wale ambao hawajapiga hesabu hizi ambazo nimewaandikia leo. Kama Arsenal angechukua ubingwa wa Ligi kuu ilikuwa ni bonasi tu lakini mshahara hasa ambao waliustahili ni kuingia Top Four.

Wachezaji na Arteta walijichongea wenyewe kwa mashabiki kwa kwenda mbali zaidi huku wakiwa wanaongoza Ligi. Sikumbuki ni lini Arsenal iliingia katika mbio za kugombea ubingwa hadi Januari. Ni zamani. Nadhani ni tangu zama za Arsene Wenger kwa sababu hata katika zama za Unai Emery Arsenal haikuwahi kuingia katika mbio za kuwania ubingwa. Ilikuwa katika mbio za kuwania Top Four ambayo nayo ilikuwa ngumu kwao.

Columnist: Mwanaspoti