Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Aouita chui wa Jangwani' aliyetisha riadha

Mkimbiaji Riadha.jpeg Said Aouita

Sat, 6 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi karibuni nilipokuwa naangalia Nile TV ya Misri kupata uchambuzi wa mchezo wa Simba na Wydad Athletic Club ya Morocco niligundua jambo lililonikumbusha nilipokuwa mhariri wa Michezo wa magazeti ya Daily News na Sunday News miaka ya 1970 na 1980.

Klabu hizo mbili ni kongwe katika nchi zao. Simba ilianzishwa 1936 na Wydad 1937. Jambo lenyewe ni kuona katika kipindi hicho cha michezo maelezo ya mwanariadha maarufu wa zamani wa Morocco, Said Aouita akiwa anakaribia kulia kwa namna aliyekuwa mkewe alivyomharibia maisha.

Nilichokumbuka ni 1983 au 1984 nililetewa na Kinyunyu aliyekuwa dhamana wa chumba cha mashine za kupokea habari na picha za Aouita kupitia Shirika la Habari Marekani (AP) iliyokuwa na maandishi yaliyoandikwa hivi, "Smiling Desert Cheetah makes it again" yaani Chui wa Jangwani mwenye tabasamu afanya tena vitu vyake.

Wakati ule kule Marekani nadhani katika Jiji la Houston alitoroka kutoka kwenye bustani ya wanyama na alishaua watu wawili au watatu huku msako mkali wa kamkamata ukiendelea. Nilishangaa kwa nini picha ilikuwa ya mtu na sio chui, lakini wakati najadili suala hilo na wahariri wenzangu, Emmanuel Bulugu na Gabby Mgaya (wote marehemu), Kinyunyu alileta kikaratasi chenye habari za chui wa Jangwani, Said Aoita kuwa amevunja rekodi yake ya dunia ya mbio za mita 5,000.

Katika runinga wa Nile TV, Aouita aliyeonekana kuchoka hakuwa na tabasamu, bali sura yenye huzuni kubwa. Alikuwa akielezea kwa mara nyingine tena habari iliyotoka katika Moroco TV kwamba aliyekuwa mkewe kwa miaka 37, Khadija Skhir ambaye aliachana naye miaka miwili iliyopia ameghushi hati mbalimbali na kuchukua fedha na mali zake nyingi.

Alisema kosa alilofanya wakati wakiwa pamoja alijua kila kitu kuhusu fedha na mali zake na kwamba alifanya hivyo kwa kushirikiana na watoto wao watatu wa kike akiwemo mwimbaji maarufu, Zena Aouita. “How could you not trust your partner of 37 years?,” alihoji.

"Hivi sasa sina kitu benki. Nimekuwa masikini na sina akiba benki wakati nilitarajia kuishi kwa furaha nikiwa mzee," alisema.

Malalamiko ya Aouita yamepokewa kwa njia tafauti za masikitiko na furaha nchini Morocco. Wale waliomsikitikia waliona amedhulumiwa na mkewe, lakini wapo waliosema Mungu anamlipa hapahapa duniani.

Hii ni kwa sababu miaka mitatu iliyopita, baba yake Ahmed Aouita akiwa na miaka 83 aliviambia vyombo vya habari kwamba mwanawe Said hamjali na kwamba anaishi maisha ya shida wakati mwanawe anaishi maisha ya kifahari. Huyu aliyejulikana kama chui wa Jangwani alitawala mbio za masafa ya kati na marefu katika miaka ya 1980. Kila aliposhiriki mashindano ya mbio za mita 800 na 1,500 watazamaji walikuwa na hamu kujua nani angeshika nafasi ya pili kwa vile hakuna aliyeweza kumtia mkobani chui wa Jangwani.

Kila aliposhinda mkimbiaji aliyemfuata kumpa mkono aliyeshika mkia na kumwambia: “Leo ulikuwa wa kwanza kutoka nyuma jitahidi uwe wa kwanza tukianzia mbele.” Wataalamu wengi wa riadha walisema kama chui wa Jangwani angekimbia mita 1,500 na wakimbiaji nyota wa miaka michache nyuma kama Filbert Bayi wa Tanzania, Sebastian Coe wa Uingereza na John Walker wa New Zealand pangekuwepo na kazi pevu ya kutafuta mshindi.

Miongoni mwa rekodi za dunia alizoweka ni kunyakua medali ya dhahabu kwa mbio za mita 5,000 za mashindano ya Olimpiki zilizofanyika Los Angeles, Marekani ka 1984. Mwaka 1985 alikuwa anashikilia rekodi za dunia za mbio za mita 1,500 na 5,000 na kuwa mtu wa kwanza tangu 1955 kushika rekodi za mbio hizo mbili. Baadaye alivunja rekodi za dunia za mbio za maili 2, mita 2,000 na 3,000.

Katika mbio za mita 5,000 alivunja rekodi yake ya dunia mara mbili katika kipindi cha siku sita kwa kutumia saa 12:58.39.

Vilevile alishinda mashindano ya kimataifa kwa masafa ya kati hadi alipostaafu 1993. Kilichowashangaza wakimbiaji wengi ni kwamba alikuwa na ubavu wa aina yake na kukimbia kwa ustadi mkubwa. Wakati ule alikuwa mwanariadha pekee duniani aliyekimbia mita 800 kwa chini ya dakika 1 na sekunde 44, mita 1,500 kwa chini ya dakika 3 na sekunde 300, mita 3,000 kwa chini ya dakika 7 na sekunde 30 na mita 5,000 kwa chini ya dakika 13.

Wakimbiaji mashuhuri aliochuana nao siku zile ni pamoja na Joaquim Cruz wa Brazil, Peter Rono na John Ngugi wa Kenya na Alberto Cova wa Italia. Mwanariadha huyo ni mtu ambaye hutembea polepole na asiyemjua anapomtazama akimtazama anaweza kufikiri ana maradhi ya miguu au ameumia. Lakini enzi zake kila alipoingia uwanjani kwa mashindano miguu yake ilichanganya kama cherehani hasa yalipobaki masafa mafupi kuelekea kumalizia mbio husika.

Kabla ya kustaafu Septemba, 1993 Aouita alishinda mashindano 115 kati ya 119 aliyoshiriki. Hii ni rekodi ya aina yake isiyosahaulika. Aliendelea kushiriki mara mojamoja katika mashindano kwa mialiko ili wamuone na kumsalimu kwa ushujaa wake. Wakimbiaji waliofanikiwa mara chache kumshinda ni Steve Cram katika mita 1,500, Alessandro Lambruschini mita 3000, Joaquin Cruz na Paul Ereng (mita 800) na Yobes Ondieki (mita 5000).

Said Aouita alizaliwa Novemba 2, 1960 katika mji wa Kenitra, Morocco na alipenda riadha tangu alipokuwa shule. Mara nyingi akishinda alisema: "Nafasi ya kwanza ni yangu na zinazofuata nimetoa zawadi. Anayetaka nafasi ya kwanza ajue ananipora mali yangu na sitakubali."

Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kuvunja rekodi ya Henry Rono wa Kenya ya mita 3,000 iliyodumu muda mrefu kwa kutumia dakia 7 na sekunde 29.45.

Mwaka 1992 aliweka rekodi ya dunia ya mita 3,000 ya mbio za ndani, lakini Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha lilikataa kuikubali. Kutokana na maumivu alishindwa kushiriki michezo ya Olimpiki iliyofanyika Barcelona, Hisapnia 1992. Alijaribu kushiriki mashindano mbalimbali 1993 hadi 1995, lakini umri ulikataa na kuamua kustaafu.

Hapo ndipo alipoamua kuwa kocha wa wakimbiaji wa masafa ya kati nchini Morocco na baadaye Australia ambapo aliachia ngazi baada ya kudaiwa kwamba aliwahimiza wakimbiaji kutumia dawa za kuongeza nguvu - shutuma ambazo alisema zililenga kumpaka matope. Kwa kuheshimu mchango wake wa michezo kwa nchi yake treni ya mwendokasi inayotoka Rabat kwenda Casablanca imepewa imepewa jina la Aouita. Wengine wanaiita Chui wa Jangwani.

Hivi sasa yupo Morocco na anashiriki kuongoza michezo ya riadha huku akiheshimiwa na serikali na wanamichezo. Atabaki kuwa mmoja wa wanariadha mashuhuri walioshuhudiwa katika mbio za masafa ya kati.

Columnist: Mwanaspoti