Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ametoka Nabi, ameingia Nabi

Gamondi Ms Ametoka Nabi, ameingia Nabi

Fri, 8 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna kitu kilikuwa kinaleta sintofahamu pale Yanga kama kuondoka kwa mshambuliaji Fiston Mayele na kocha Nasredine Nabi. Wengine wote wangeweza kuondoka tu na hakuna ambaye angejali, sio Nabi na Mayele.

Ilifika mahali Nabi alikuwa anaitwa Profesa. Mtaalamu kutoka chuo gani? Yanga University. Hakuna kitu mashabiki hawatasahau hivi karibuni kama kutetema. Ni staili maarufu zaidi miaka ya hivi karibuni ya kushangilia Afrika. Ilikuwa inasubiriwa sana na mashabiki pale Fiston Mayele anapotupia mpira kambani.

Ikawa asubuhi ikawa jioni, Mayele anaondoka. Bado Yanga wanaendelea kujitafuta lakini mabao yanaingia kambani. Tayari wameshafunga mabao 10 kwenye mechi mbili tu za Ligi Kuu. Kwanini bado watamkumbuka Mayele? Ni rahisi tu. Mabao ya Mayele yalileta makombe ya kutosha pale Jangwani.

Kuna mtu alikuwa anaitwa Nasreddine Nabi. Hatari kabisa kocha huyu wa Kiarabu. Alikuwa fundi sana wa mabadiliko. Mabadiliko yake mengi ya mbinu na wachezaji hasa kipindi cha pili cha mechi yalikuwa yanamlipa. Mashabiki walimpenda sana. Alirudisha heshima ya Yanga iliyokuwa taratibu inaanza kupotea. Asikwambie mtu kitu, sifa ya timu kubwa zote duniani ni kushinda mataji makubwa.

Nabi alirudisha heshima ya Yanga kwa kuwapa mataji makubwa nchini. Ni kweli Yanga bado wanamkumbuka Nabi? Jibu ni ndiyo. Mataji aliyowapa ni kumbukumbu ya maisha. Itadumu vizazi na vizazi.

Kwa sasa pale Yanga kuna mtu mpya anaitwa Maxi Nzengeli. Sio mbadala halisi wa Mayele ila ana balaa. Ni fundi kwelikweli wa boli. Ni moja kati ya wachezaji wachache waliokamilika zaidi uwanjani. Ana nguvu. Ana kasi. Anafunga. Ana-assist. Ni mara chache sana utakutana na mchezaji wa aina hii. Hapa Yanga wamelamba kidume kwelikweli. Ni mapema sana wakati mwingine kumwaga sifa kwa mchezaji mpya, lakini mchezo wa soka unachezwa hadharani. Max Nzengeli ana balaaa.

Nadhani kadri timu zetu zinavyoanza kupata mafanikio, hata aina ya usajili wa wachezaji wa kigeni hapa nchini inaanza kubadilika. Taratibu tunaanza kuona Wachezaji wa kigeni wenye uwezo. Wazee wanaanza kupungua.

Tunaanza sasa kupata watu wa kazi. Nzengeli ni mtu wa kazi kwelikweli. Anafanya kazi za mawinga kuwa nyepesi. Anafanya kazi za viungo wa chini kuwa nyepesi pia. Nadhani huyu ndiye alistahili kupewa jezi namba sita iliyonadiwa na Yanga kipindi chote cha dirisha la usajili. Mchezaji aina ya Nzengeli ni kazi sana kumdhibiti dimbani. Haeleweki anakuja kwa staili gani. Ile spidi aliyonayo inahitaji mtu mwingine wa aina yake kumkaba.

Inahitaji beki mwenye maarifa ya haraka sana kumdhibiti. Ukichelewa kidogo tu, utamkuta kwenye kona ya kibendera anashangilia. Nzengeli sio mbadala wa moja kwa moja kwa Mayele, lakini ana balaa zito. Anajua mpaka anajua tena.

Pale Yanga kwa sasa kuna mtu anaitwa Miguel Gamondi. Ana balaa sana. Ni kocha mpya wa Yanga. Hapa ni sawa na kusema ameondoka Nabi amekuja Nabi. Ni moto juu ya moto. Yanga wamekuwa na pumzi sana kipindi cha pili.

Ni kama wafukuza upepo. Raundi za kwanza ni kama hawana mwendo ila kwenye kumalizia mbio, mwendo ndiyo unachanganya.

Wachezaji wa Yanga wanaonekana kuwa fiti zaidi chini ya Gamondi. Karibu kila mchezaji amekuwa na mapafu ya mbwa. Ni kweli mashabiki wa Yanga bado watamkumbuka Nabi?

Jibu ni ndiyo kwa sababu ameshinda mataji akiwa klabuni na kuwapa burudani. Ni kweli Yanga wanainjoi chini ya Gamondi? Jibu ni ndiyo. Maana ameondoka Nabi, amekuja Nabi.

Gamondi ana kazi ya kubadilisha tu wachezaji, lakini burudani iko palepale. Kushinda mechi tatu mfululizo sio jambo kubwa. Kufunga mabao matano kwenye mechi tatu mfululizo ndiyo ufundi wa Gamondi ulipo.

Yanga ya Gamondi haishindi tu, inaburudisha pia. Hapa ndipo Yanga walipoanza kupiga bao. Kila shabiki anataka kuona watakuwa na mwendelezo wa aina hii kwa muda gani? Watakuwa na raha kwa muda gani? Ni nguvu ya soda? Mimi na wewe hatuna majibu ya moja kwa moja, lakini muda utaamua.

Baada ya mechi ya pili tu ya ligi, Yanga wamerudi kileleni. Alama sita, mabao 10 ya kufunga. Hawajaruhusu bao hata moja langoni mwao. Ni mwanzo mzuri sana kwa timu inayotaka kutetea ubingwa.

Kama Gamondi atawapeleka hata robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu jina lake litaimbwa sana kwenye zama zake.

Kama kuna mtihani wa kihistoria kwa Yanga, basi ni kufanya vizuri kimataifa. Yanga kihistoria sio wa kimataifa. Ufalme wao uko kwenye soka la ndani.

Ubabe wao ni wa hapahapa tu. Kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itawaanzishia safari mpya ya kimataifa. Tayari msimu uliopita walifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni hatua kubwa sana.

Sasa ni zama ya Ligi ya Mabingwa na mikoba yote ipo kwa Gamondi. Huyu ndiye mbeba maoni ya Jangwnai msimu huu. Mpaka sasa ni sawa na kusema ameondoka Nabi amekuja Nabi. Gia ni ileile ya kupandisha mlima.

Ni kweli Nzengeli sio mbadala wa moja kwa moja wa Mayele, lakini ana balaaa. Ameleta utofauti mkubwa kikosini.

Ni kweli Gamondi sio Profesa, lakini spidi ni ileile. Yanga inaonekana kuwa kwenye mikono salama ya Nzengeli na Gamondi.

Ni muda wa kuwatazama na kuona kipi wanakipeleka Jangwani mwishoni mwa msimu. Hapo ndipo tutakapoona tofuati ya Mayele na Nabi na kule ni Nzengeli na Gamondi.

Columnist: Mwanaspoti
Related Articles: